NMB kuendelea kuibeba gofu TPDF

10Sep 2019
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
NMB kuendelea kuibeba gofu TPDF

KATIKA kusapoti harakati za kimichezo na kiuchumi kwa timu za Majeshi ya Ulinzi na Usalama Tanzania (TPDF), Benki ya NMB imeahidi kuendeleza udhamini wao kwao.

Ahadi hiyo imetolewa wakati ikipongezwa kwa mchango uliobadili taswira ya mchezo wa gofu nchini kiasi cha kuvutia wengi miongoni mwa Watanzania.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi wa Michuano ya Gofu ya Mkuu wa Majeshi Tanzania (CDF Cup 2019), Mkuu wa Kitengo cha Wafanyabiashara Wakubwa wa NMB, Filbert Mponzi, alisema benki yake itadumisha kadri iwezavyo ushirikiano na sapoti kwa TPDF.

Hafla hiyo ilifanyika katika Viwanja vya Gofu Lugalo, ilikofanyika michuano ya siku mbili ya CDF Cup 2019, iliyodhaminiwa na Benki ya NMB, ikiwa na lengo la kuadhimisha Siku ya Majeshi ya Wananchi wa Tanzania (JWTZ), ambayo hufanyika Septemba Mosi ya kila mwaka.

Mponzi alisema Maajeshi ya Ulinzi na Usalama nchini ni miongoni mwa taasisi nyeti zilizo na wateja wengi katika benki yake na kwamba hicho ndicho huwapa msukumo wa kusaidia michezo na timu zao kulingana na mahitaji.

“NMB, tunaahidi kuendelea kudhamini CDF Cup, lakini pia kusapoti timu za Majeshi Tanzania, na hii inatokana na sera ya kusapoti michezo ya benki yetu, ambayo pia tulidhamini ushiriki wa Jeshi la Tanzania katika Mashindano ya Majeshi kwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki nchini Kenya,” alisema Mponzi.

NMB CDF Cup ni michuano inayoratibiwa na Klabu ya Gofu Lugalo na kudhaminiwa na benki hiyo, ambako mwaka huu iliwakutanisha washiriki wengi zaidi na kuvunja rekodi, kati yao 127 wa ridhaa, 19 wa kulipwa na 25 watoto (Juniors), huku Ally Mcharo wa TPC Moshi akiibuka mshindi wa jumla.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa taji la jumla la michuano hiyo na Mnadhimu Mkuu wa Jeshi,  Mohamed Yakubu, Mcharo aliipongeza NMB kwa sapoti iliyobadili taswira ya mchezo na kuufanya kuwa mmoja kati ya michezo pendwa nchini, kauli iliyoungwa mkono na Mnadhimu Mkuu, Yakubu.

Mcharo aliiomba benki hiyo kutouacha njiani mchezo huo, badala yake iendelee kuusapoti na kudhamini mashindano mbalimbali ya gofu, ili kuzalisha wakali watakaolitangaza taifa nje ya mipaka ya Tanzania na Afrika kwa ujumla.

NMB imeidhamini CDF Cup 2019 kwa kitita cha Sh. milioni 21.7. Benki hiyo imekuwa mdau mkubwa wa gofu na mshirika mzuri wa timu za majeshi, ambako mwaka huu iliidhamini timu ya Tanzania iliyoshiriki michuano ya Majeshi Afrika Mashariki, kwa Sh. milioni 15.

Habari Kubwa