Simulizi ya aliyenusurika kuozeshwa ndoa ya utotoni

10Sep 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Simulizi ya aliyenusurika kuozeshwa ndoa ya utotoni
  • Baba yake alishapokea mahari ya ng’ombe watano na Sh. 300,000

MTOTO Nchambi mwenye umri wa miaka 17 (si jina lake halisi), mkazi wa Kata ya Maganzo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, amesimulia alivyonusurika kuozeshwa ndoa ya utotoni na Baba yake mzazi kwa mahari ya ng’ombe watano pamoja na fedha taslimu Sh. 300,000 kwa mwanamume ambaye hata hamjui.

Mtoto Nchambi (si jina lake halisi) mkazi wa Kata ya Maganzo wilayani Kishapu Mkoani Shinyanga, akisimulia namna alivyotaka kuozeshwa ndoa ya utotoni na wazazi wake, ambao tayari walikuwa wamechukua mahari ya ng'ombe watano na Sh.300,000 ili kumuozesha kwa mwanaume ambaye hata hakuwa anamjua.

Akielezea tukio hilo Septemba 5, mwaka huu kwa mwandishi wa makala haya anasema aliona ng’ombe watano wameletwa nyumbani kwao, akajua kwamba baba yake amewanunua, kumbe haikuwa hivyo bali ni mahari iliyotolewa ili yeye aolewe.

Anasema ng’ombe hao waliletwa kwao Juni mwaka huu na baada ya kupita takribani mwezi mmoja, ndipo siku moja akaitwa na wazazi wake na kuelezwa kwa nini ng’ombe hao wako kwao.

Alijulishwa na Baba yake mzazi kwamba amechukua mifugo hiyo kama malipo ya mahari yake, hivyo anapaswa kuolewa ili familia yao ipate mali (mifugo).

Anafafanua kuwa aligoma kuolewa, tena na mwanamume ambaye hata hamjui, kwani nia yake ni kuendelea na masomo baada ya kuwa amemaliza elimu ya msingi mwaka 2017.

“Baada ya kugoma, wazazi walianza kunishawishi nikubali tu kuolewa, na kwamba endapo nitakataa, nitaleta mkosi kwenye familia yetu kwa kuwa kwa mujibu wa mila na desturi za kabila letu la Kisukuma, muoaji huwa hakatiliwi,” anasema.

Nchambi anabainisha kwamba wamezaliwa mapacha kwa wazazi wao na mwenzake alifaulu kuendelea na masomo ya Sekondari, na sasa yuko kidato cha pili wakati yeye hakufaulu.

Anasema kila alipowaeleza wazazi wake wampeleke chuo akasome hata kozi ya ufundi cherehani, wamekuwa wakimueleza kwamba  hawana uwezo.

“Hivyo niliamua kukaa tu nyumbani, lakini kumbe ninavyoendelea kubaki nyumbani naonekana kero kwa wazazi wangu, na ndipo wakaamua kunitafutia mwanamume wa kunioa,” anasema na kuongeza:

“Mimi bado mdogo, siwezi kumudu masuala ya ndoa…vilevile nafahamu madhara ya kuolewa katika umri mdogo kutokana na elimu tuliyokuwa tukipewa shuleni.”

Anasema wazazi wake waliendelea kumrubuni ili akubali kuolewa kwa kuwa tayari wameshachukua mahari hiyo na kwamba endapo ataendelea kugoma kwa kutotii amri yao, watakosa mali hizo, hivyo kutouepuka umaskini walionao.

ASAIDIWA

Nchambi anafafanua kuwa wakati mvutano ukiendelea nyumbani kwao na kuonekana kama mkosi ndani ya familia, ndipo siku moja akaona wanakuja wasaidizi wa kisheria nyumbani kwao.

Wasaidizi hao wanatoka Shirika la PACESH linalojishughulisha na masuala ya kijamii.

“Wasaidizi hao waliwaelimisha juu ya   Sheria ya Mtoto na madhara ya ndoa za utotoni…waliwaelimisha pia kuhusiana na madhara ya kumuozesha mtoto mdogo, kwani ni ukiukaji wa Sheria ya Mtoto.

“Hatua hiyo iliniokoa kwani wazazi waliamua kusitisha suala la kuniozesha na wakaamua kurudisha ng’ombe za watu walizochukua kama mahari yangu,” anasema.

BABA MZAZI

Naye Baba mzazi wa mtoto huyo, Lyuba Seif, anakiri kutaka kumuozesha binti yake huyo, kwa madai amekaa nyumbani kwa muda mrefu baada ya kufeli masomo yake ya elimu ya msingi.

“Tatizo sina uwezo wa kifedha wa kumsomesha hata kwenye vyuo vya ufundi, na ndiyo maana nilichukua uamuzi wa kumtafutia mwanamume ili aolewe, nipate mali,” anasema.

Seif anabainisha kwamba kutokana na binti yake kukaa nyumbani kwa muda mrefu, anahofia asije kupata ujauzito na hivyo kuzalia nyumbani, kitendo ambacho ni mkosi kwenye familia, pamoja na kuwakosesha utajiri (mifugo), hivyo kuendelea kuwa maskini.

“Nilishapanga kumuozesha binti yangu huyu kwenye kijiji cha jirani, ambapo tayari nilishachukua mahari ya ng’ombe watano pamoja na pesa taslimu Sh. 300,000 ili kujihami asije akapewa ujauzito akiwa nyumbani, na kutuletea mkosi kwenye familia,” anasema na kuongeza:

 “Lakini baada ya wasaidizi hawa wa kisheria kutoka PACESH kufika kwangu, na kunifafanulia juu ya Sheria ya Mtoto pamoja na madhara ya kumuozesha mtoto mdogo, ikanibidi niahirishe uamuzi wangu na kurudisha ng’ombe za watu…pia niliwaeleza ilivyokuwa nao wakanielewa.”

ATOA OMBI

Mzazi huyu anaomba wadau wajitokeze kumsomesha binti yake huyo chuo chochote cha ufundi ili apate kutimiza ndoto zake, kutokana na yeye kutokuwa na uwezo wa kifedha.

Anabainisha kwamba endapo atakosekana mtu wa kumsaidia, itabidi mwakani amuozeshe kwenye familia hiyohiyo, kwa sababu atakuwa ameshafikisha umri wa miaka 18.

“Ieleweke nimeahirisha suala hili la kumuoza binti yangu baada ya kubanwa tu na hawa wasaidizi wa kisheria… tayari nimesharudisha ng’ombe za watu, lakini nina deni la Sh. 300,000 ambazo nilizitumia,” anasema na kuongeza:

“Ninasubiri mwakani atakapofikisha miaka 18, umri wa mtu mzima kama atakuwa hajapatikana msamaria mwema wa kumlipia masomo ya chuo, basi nitampleleka akaolewe huko huko nilikochukua pesa ya watu.”

PACESH

 

Kwa upande wake msaidizi wa kisheria kutoka Shirika hilo la PACESH Maganzo wilayani Kishapu, Fatuma Katabalo, anasema taarifa za kuozeshwa kwa binti huyo ndoa ya utotoni walizipata kwa majirani zao.

“Ndipo tulipoamua kwenda kwenye familia hiyo kuwapatia elimu ya sheria ya mtoto na madhara ya kuozesha mtoto mdogo,” anasema.

Fatuma anabainisha kwamba baada ya kufika kwenye familia hiyo walikaa na wazazi wa binti huyo, na kuwaeleza kwamba kitendo hicho wanachotaka kukifanya ni ukiukwaji wa sheria ya mtoto.

“Tukawafafanulia kwamba wanaweza pia kumsababishia madhara makubwa iwapo ataolewa katika umri mdogo, ikiwamo kupoteza maisha wakati wa kujifungua kutokana na viungo vya uzazi kutokuwa vimekomaa,” anasema na kuongeza:

“Aidha, tuliwaonyesha kwamba wanaweza hata kufungwa sababu ni kosa kumuozesha mtoto mdogo pamoja na kukiuka haki za binadamu…wakaogopa na kuamua kusitisha uamuzi wao, wakarudisha mahari ya ng’ombe waliokuwa wamepokea.”

MENEJA

Meneja Mradi wa Huduma na Msaada wa Kisheria kutoka Shirika hilo la PACESH Mkoani Shinyanga, John Shija, anakubaliana na uamuzi wa wazazi wa mtoto huyo wa kusitisha ndoa hiyo.

“Ninatoa ahadi ya kumsomesha binti yao huyo chuo cha ufundi ili apate kutimiza ndoto zake alizonazo za kielimu,” anasema.

Anabainisha kwamba tatizo la mimba na ndoa za utotoni mkoani Shinyanga haliwezi kwisha, endapo wazazi wenyewe watashindwa kujitambua, na kuacha kuendekeza mila potofu za kutomthamini mtoto wa kike, kwa kumchukulia kama kitega uchumi kwenye familia.

Anatoa wito kwa wazazi mkoani humo kuacha tabia ya kuwaozesha mabinti wakiwa katika umri mdogo.

“Watimize wajibu wao kwa kuwasomesha ili taifa liwe na wataalamu wa kutosha, lakini pia watoto hawa ndio watakaokuja kuwasaidia na kuwanunulia mifugo mingi zaidi ambayo wanaitaka baadaye,” anasema.

TAKWIMU

Takwimu za kitaifa za mwaka 2012 zinaonyesha kwamba mkoa wa Shinyanga unaongoza Tanzania kwa tatizo la mimba na ndoa za utotoni kwa asilimia 59, ukifuatiwa na Tabora asilimia 58 na Mara asilimia 55, ambapo watoto wa kike wamekuwa wakiolewa chini ya umri wa miaka 18.

Habari Kubwa