Unajua Chekechea ilivyobeba siri mahali elimu inakosusasua nchini?

10Sep 2019
Jaliwason Jasson
Babati
Nipashe
Unajua Chekechea ilivyobeba siri mahali elimu inakosusasua nchini?
  • Kila zana darasani, sawa maneno maelfu
  • NGO Manyara yawaletea mapya wafugaji
  • Majaribio tu, wasiojua kusoma nao adimu
  • Mwalimu  ‘afunguka’ mazito yake darasani
  • “…mchango mkubwa katika ukuaji ubongo wa mwanafunzi, kwani matumizi yake yanamsaidia kujenga kumbukumbu ya kudumu, pia yanamjenga milango yote ya fahamu na inawasaidia wanafunzi kulipenda somo husika…”

KATIKA mustakabali wa sera za kitaaluma, ubora wa elimu unaanzia ngazi ya awali.

Mwanafunzi wa awali akionyesha zana zake

Hiyo iko bayana na ndio maana kuna wakati serikali ilitoa mwongozo wa ulazima wa elimu kuanzia ngazi ya awali. Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuna wakati ilitoa maelekezo kwa shule za msingi nchini kujiboresha katika eneo hilo.

Msingi wake kufanikisha hayo ni kwamba elimu katika ngazi hiyo ya awali inaboreshwa kwa kuwa na walimu makini, wanaokuwa chachu ya kuwatengeneza vyema, kuanza darasa la kwanza wakimudu kinachoitwa ‘KKK’ kwa maana ya; Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.

Hitaji hilo ndilo linaloibua changamoto mpya ya kuwa na zana sahihi za kufundishia, ili iwe rahisi kuelewa kwa mtoto anayejifunza.

KUTOKA BABATI

Ofisa Elimu Taaluma wa Halmashauri ya Wilaya Babati mkoani Manyara, Joyce Oronu, anasema sera ya elimu ya zamani ilimhitaji mwanafunzi wa darasa la awali awe mwenye umri kati ya miaka mitano hadi sita.

Anaeleza mabadiliko kwamba, hivi sasa mahitaji ni miaka minne, kwa maana ya kusoma miaka miwili, kwani anapofikisha umri wa miaka sita, anapaswa kuanza darasa la kwanza.

Oronu anasema katika kuhakikisha walimu wa awali wanatumia zana sahihi, mkoani Manyara, kuna asasi ya Literacy and Numeracy Education Support Programme (LANES) waliwapa mafunzo ya kutumia zana za kufundishia watoto awali.

Hiyo ilitoa mwanya kwa walimu wa awali 138 katika halmashauri hiyo, kila shule kukiwapo mwalimu mmoja aliyepatiwa mafunzo hayo, ili kumsaidia kuandaa zana na kuzitumia kuwafundisha watoto wa awali.

Anafafanua kwamba, zana zinatakiwa ziendane na umri wa mwanafunzi, pia nyenzo za mwalimu ziendane na somo analofundisha kukidhi vigezo vya kufundisha darasa la awali.

Mtaalamu Oronu, anaziweka zana tajwa kwenye makundi matatu: Zana za kutengeneza, mfano kiti, meza, jembe; jingine, zana za kununua kama mpira na kikombe, ambazo mwalimu anaweza kuwaagiza wanafunzi kuja nazo kutoka nyumbani; mwisho ni zana za kuunda kama vile vyungu na midori, ambavyo wanafunzi wanaweza kutengeneza kwa udongo wa mfinyanzi.

ZINAWASAIDIAJE?

Ofisa mtaalamu huyo, anasema hizo zina mchango mkubwa katika ukuaji ubongo wa mwanafunzi, kwani matumizi yake yanamsaidia kujenga kumbukumbu ya kudumu, pia yanamjenga milango yote ya fahamu na inawasaidia wanafunzi kulipenda somo husika.

Pia, anataja manufaa ya kumrahisishia mwalimu kufundisha, huku mwanafunzi akiwa mbunifu, anayejiamini na kujielekeza.

Ofisa Elimu Msingi wa Halmashauri ya Wilaya Babati, Getrude Kavishe, anasema walimu wanaotumia zana katika kuwajulisha watoto kujua kusoma, kuhesabu na kuandika, kunawapa uhakika wanajifunza kwa vitendo.

Getrude anasema katika mwaka wa kwanza wa darasa la awali, mwanafunzi zaidi anajifunza mazingira na kiasi kidogo cha masomo, kwani kwa asilimia kubwa wanakuwa wametawaliwa na michezo na hawajielewi

Anataja baadhi ya mambo wanayojifunza katika ngazi ya awali ni nyimbo, michezo mazingira ya shule.

“Mwaka wa pili unamuandaa mwanafunzi wa awali kuingia darasa la kwanza na kujifunza kwa michezo na nyimbo . Kwao ni vizuri zaidi na inamjenga mtoto aweze kujiamini na kuwa mbunifu,” anasema Getrude.

 “Kwanza watoto wale wanatakiwa wapewe ule upendo, hivyo kwenye michezo mwalimu anawapa upendo na anatakiwa kucheza nao michezo yao na shule ni  mahali pazuri pa watoto kuchezea na kujifunza,’’anasisitiza

Anafafanua kuwa mwalimu wa awali anatakiwa awe rafiki wa watoto na kushiriki kila mchezo wao na darasa likitawaliwa na vitu mbalimbali vya mchezo.

KUWAPO VIBOKO?

 Getrude anaendelea: “Yule mtoto wa awali ukimpiga atachukia shule, hataipenda tena, lakini ukijenga naye urafiki, mtoto huyo atakupenda na atakuwa rafiki wa mwalimu, mpaka kuja shule anakuwa hasukumwi na mtu yeyote na ukimzuia, lazima achukie.”

Anasema, mwalimu wa ngazi hiyo hapaswi kuwaelekeza wanafunzi darasani kwa fimbo, akisema inamuogopesha na kumuondolea upendo.

Kuhusu mustakabali wa ulinzi na usalama wa wanafunzi hao wa awali wanapotoka na kwenda shuleni, Getrude anasema ni jukumu la jamii nzima kuhakikisha usalama na haki zao za kisheria.

Anasema, watoto hao washauriwe kutembea kwa makundi, ili kukwepa uovu dhidi yao na anaelekeza wito kwa walimu na walezi kuwajibika kwa hilo ipasavyo.

Sambamba na asasi ya Lanes, shirika la kimataifa la World Vision, nalo limeungana kubeba jukumu la kutoa mafunzo ya kuandaa zana za kufundishia watoto wa awali. Kila mwezi walimu wawili kutoka tarafa ya Mbugwe wanapewa mafunzo.

Oronu anafafanua, mafunzo hayo yana msaada mkubwa, kwa kuongeza idadi ya watoto wanaojua kusoma, kuandika na kuhesabu na World Vision, imekuwa ikisaidia kununua vifaa vya kutengeneza zana kwa shule za ukanda wa Mbugwe.

WALIMU

Mwalimu wa darasa la awali katika Shule ya Msingi Dudumera, Jemima Njidile, kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Babati, ni mnufaika wa mafunzo ya ualimu wa darasa la awali.

Anashauri darasa hilo kutochanganywa na eneo jingine la shule, maana watoto hao hawatakiwi kuchanganywa na wenzao wa shule ya msingi.

“Wakichanganywa watoto hawa na wanafunzi wa shule ya msingi, wanashindwa kufanya vitu vinavyoendana na mtaala wao,” anasema Jemima.

Anaeleza kwamba umuhimu wa zana za kufundishia, ndizo zinamfurahisha na kumtengenezea mtoto kumbukumbu na atapenda mazingira ya kufundishia.

Analimwagia sifa shirika la World Vision, kuwa mafunzo yaliyomsaidia kutengeneza zana zinazomtosheleza kufanya vizuri.

HULKA YA UFUNDISHAJI

Kuhusu hili Jemima anaeleza: “Mwalimu wa awali inabidi awe anawapenda watoto na asitumie lugha ya ukali badala yake atumie lugha ya upole.”

Anaongeza mfano: “Siku moja mtoto alimpiga mwenzake mpaka akatokwa na damu. Sikumpiga, ila nilimwambia atafute maji amnawishe mwenzake, ili wenyewe wapeane msamaha.”

Mwalimu Jemima anasema, mbadala wa adhabu kwa mwanafunzi anayekosa anatumia mbinu ya kuwaelekeza na walio wasumbufu zaidi, anawaita wazazi wao kushauriana cha kufanya ili wajirekebishe.

Pia, anazungumzia mzigo wa wingi wa wanafunzi alio nao kwamba, darasa lake lina wanafunzi 95, hivyo fursa ya kumpitia kila mwanafunzi ni ngumu.

Mwalimu Jemima anasema kati ya Januari hadi Juni, huwa anawafundisha kucheza, kuimba na matendo, akiwachanganya mwaka wa kwanza na wa pili.

Anasema, kuanzia Julai hadi Desemba, ndipo anapoanza kuwafundisha ‘namba matendo’ akimaanisha kujumlisha na kutoa na kadri muda unavyosonga, anawachambua wanaoelewa kuingia darasa la kwanza.

Je zana zinamsaidiaje mtoto kujua kusoma, kuhesabu na kuandika? Mwalimu anafafanua kwa kauli “zaidi ya asilimia 90 inampa wepesi mwanafunzi.”

CHANGAMOTO

Anataja changamoto inayomkabili katika shule yake yuko peke yake kwa darasa hilo na ndio maana analazimika kuwachanganya wanafunzi wa mwaka wa kwanza na pili.

Anasema hata kipindi anapotaka kwenda likizo inakuwa changamoto, kwani mwalimu mkuu huteua mwingine kufundisha darasa hilo, wakati hana mafunzo ya kufundisha wanafunzi wa awali.

Ni hoja ambayo Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Dudumera, Mussa Mkumbo, anakiri mapungufu kwa shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1956, akieleza darasani pia wanafunzi wanalazimika kuandika wakiwa wamesimama, kutokana na urefu ukubwa wa madawati.

Anaainisha shule yake yenye wanafunzi 578, ina uhaba wa walimu. Kwamba mbali na mmoja wa darasa la awali, katika shule ya msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba, wapo walimu 10, kati yao saba wa kike na watatu wanaume.

Jemima anataja changamoto nyingine, ni ufinyu wa eneo la kuweka zana nyingi alizo nazo.

Anaiomba serikali kutenga maeneo ya kutosha kwa  wanafunzi wa awali ili wafunzwe tofauti kimazingira, akitaja mfano wa aina za mahitaji yao ya kipekee; hisabati inayojumuisha vifaa vyake kama vile ‘vihesabio’ na picha za namba kuanzia moja mpaka tisa.

Jingine ni ‘kona ya sayansi’ anayosema inatakiwa kuwe na michoro, mfano mbwa, ndizi au machungwa; vivyo hivyo sanaa inayojumuisha ngoma na filimbi; ‘kona nyumbani’ inayojumuisha kitanda, jiko, chupa ya chai, mdoli, fagio, sahani, sabuni na kitana.

Pia, anazitaja ‘kona ya michezo’ mfano mpira, kamba, bembea; mwisho ni ‘kona ya dukani’ mfano chumvi, sukari, viberiti, madaftari, juice na kalamu anazosema zinahitaji maeneo yake, ili walimu wa awali wafundishe vizuri.

Mwalimu Mkuu Mkumbo, anashukuru msaada wa World Vision kuwezesha wanafunzi wake kumudu haraka kujua kusoma, kuandika na kuhesabu na imekuwa vigumu kumkuta mwanafunzi darasa la tatu asiyejua kusoma na walimu wanafanya kazi kwa kujiamini.

WANAVYONENA WADAU

Mratibu wa Mradi wa Magugu Area Programu kutoka Shirika la World Vision, Majid Mfinanga, anasema wanatekeleza mradi katika kata tano za Tarafa ya Mbugwe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati, katika vijiji 22.

Mtaalamu huyo anayejitambulisha, aliwahi kuwa mkufunzi wa vyuo vya ualimu nchini, anasema matumizi ya zana za kufundishia yanasaidia kujenga kumbukumbu ya kudumu kwa kutumia milango ya fahamu na yanamfanya mwanafunzi kuelewa haraka.

“Mwalimu akitumia zana, anapunguza maneno na matumizi ya zana moja, inawakilisha maneno 10,000 ambayo mwalimu angezungumza…akitumia zana ni rahisi mwanafunzi kuelewa na zana ni mbadala wa yale maneno ya mwalimu,’’anasema.

Mfinanga anafafanua kwamba, walimu waliopatiwa mafunzo ya elimu ya awali kupitia mradi huo jumla yao wako 75 na waliofanyiwa maendeleo ya wanafunzi wa awali kwenda mpaka darasa la tatu kujua kusoma, kuandika na kuhesabu, wanafika kati ya asilimia 51 na 87.

Mkufunzi huyo anasema, zana za kufundishia ni kichocheo cha kuchakata taarifa haraka na mtoto kuelewa ujumbe uliokusudiwa, akisifu zana hizo siyo jambo la kumfikirisha mtoto.

Kuhusu walimu wa awali kutoa adhabu, Mfinanga anasema dhana ya adhabu kuwa sehemu ya ufundishaji ndiyo inayopaswa kulengwa na isiwe kulazimisha mambo kama uchapaji viboko, matusi na kauli kali kwa wanafunzi, maana watajisikia vibaya na kuogopa masomo

“Watoto wanatakiwa wafundishwe kwa upendo mkubwa na walimu wao, ili waweze kuwaamini walimu wao… mwalimu anatakiwa aangalie nini cha kufanya ili asitoe adhabu,’’anasema.

Meneja Program ya Elimu kutoka shirika la So They Can, Delfina Reuben, anasema wana shule 26 wanazozisimamia katika kata nne, ambazo ni Mamire, Endakiso, Gallapo na Qash.

Reuben anataja orodha kwamba, wako wanafunzi wa awali 2563, mgawanyo wao kijinsia kuna wasichana 1217 na wavulana 1346.

Anasema, katika shule hiyo watoto wamepangiwa umri wa kujiunga ni miaka mitano, ikilenga wasome miaka miwili.

Meneja huyo anasema, walipoanza kusimamia mradi wa elimu mwaka 2016, walikuta shule tisa hazina madarasa ya awali, kitu kilichowafanya watoto wasivutiwe kuja shule maana hapakuwepo madarasa.

MATUMIZI YA ZANA JE?

Anakiri zinasaidia darasa kuzungumza, kwa kuwa hata pasipokuwapo mwalimu darasani, mwanafunzi anaweza kutumia zana za kujifunza kusoma, kwa kuunga herufi moja baada aya nyingine au kufahamu vitu mbalimbali kwa kuangalia michoro ya zana aliyoiweka mwalimu.

Reuben anaungana na wadau wenzake, kuwa zana hizo zinasaidia ukuaji ubongo na wanafunzi wanakuwa washiriki na siyo wapokeaji, huku wakimpenda mwalimu.

Anasema, hapakuwapo mafunzo ya kutosha kwa walimu na sasa mwitikio wa kutumia zana ni mkubwa, ukisaidia wanafunzi kujua kusoma, kuhesabu na kuandika.

WAZAZI JE?

Halima Ramadhani, ni mkazi wa Babati, anayekiri kwamba walimu hivi sasa wanafanya vizuri katika kutumia zana na wanafunzi wengi wamejua kusoma haraka, tofauti na zamani.

Pia, Godfrey Sanka mkazi wa Bushnet, anaishauri serikali kuwekeza katika ufundishaji wa walimu wa awali namna ya kuandaa zana na kuzitumia kwa wanafunzi, ili nchi iweze kuandaa wataalamu kuanzia ngazi za chini na kuwa na kizazi cha wasomi.

Anasema, ni vizuri serikali ikazijengea shule miundombinu ya madarasa na madawati, ili wanafunzi wasirundikane kwenye darasa moja, jambo ambalo ni kero kwa walimu na wanaosoma.

Mkazi wa Endasaki, John Samo, anaishauri serikali hasa katika ngazi za vijiji na kata, kuhakikisha watoto wa awali wanaandikishwa kwa wakati, hasa katika maeneo ya wafugaji, ambako kuna matatizo ya uandikishaji watoto kwa umri sahihi.

Maoni ya mwisho, ni ya Mustapha Rwamcho, mkazi wa Bagara, anayeeleza adhabu kwa watoto wawapo masomoni, ziendane na umri na isizidi kiasi, maana hilo likiachwa linageuka tatizo katika jamii.

Habari Kubwa