Wanasayansi kuchunguza Shimo Jeusi lililo angani

10Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wanasayansi kuchunguza Shimo Jeusi lililo angani

KUNDI moja la Wanasayansi lililopiga picha za kwanza za shimo jeusi lililo angani, limetangaza mipango ya kuchukua video yenye uasili wa shimo hilo linalopatikana katikati ya anga.

Profesa Heino Falcke ambaye mradi wa shimo jeusi ni pendekezo lake.

Setilaiti itazinduliwa kusaidia mfumo wa darubini nane zitakazotumika kuchukua filamu hiyo.

Watafiti wanasema kwamba uimarikaji wa mfumo huo utawezesha kuona jinsi shimo hilo linavyovuta na kuingiza ndani vitu vilivyo karibu yake.

Kundi hilo tayari limetuzwa tuzo ya ufanisi. Profesa Heino Falcke, kutoka Chuo Kikuu cha Raboud nchini Uholanzi ambaye alipendekeza wazo hilo la darubini, ameiambia BBC kwamba, hatua ya pili ni kuona vitendo vya shimo hilo.

Kama vile sayari, shimo hilo jeusi pia huzunguka, lakini lina maajabu ya kuizungusha anga, elimu ambayo inatakiwa sasa ifuatiliwe.

La kushangaza zaidi ni hatua ya kuchukua picha za rangi ya kitu ambacho uwezo wake ni mkubwa sana, kwamba hata mwanga hauwezi kuepuka.

Mapema mwaka huu kundi hilo la Wanasayansi lilichapisha picha za shimo kubwa jeusi lililokuwa katika sayari moja iliyo umbali wa kilomita bilioni 40, ikiwa ni mara tatu zaidi ya ukubwa wa dunia.

Picha hiyo inaonyesha gesi ya moto ikianguka kwenye shimo hilo katika rangi tofauti za machungwa.

Hata hivyo, ukweli ni kwamba shimo hilo jeusi halina rangi. Lakini kile ambacho wataalam wa angani wanaona ni vile vitu vinavyoingia ndani yake na kubadilika kuwa gesi ya moto.

Gesi hiyo inaonekana kubadilika rangi inapokaribia shimo hilo jeusi.

Kama jua linapokuwa nyuma ya mawingu jioni, mwanga kutoka kwa vitu hivyo vilivyobadilika na kuwa gesi moto unalazimika kusafiri kupitia gesi zaidi kuelekea duniani.

Hivyo basi, athari yake itakuwa kubadili rangi na umbo la vitu hivyo karibu na shimo hilo.

Kundi hilo la wataalam linatarajia kuongeza darubini katika eneo la Greenland, Ufaransa na maeneo kadhaa ya bara Afrika na tayari limewasilisha ufadhili kutoka kwa wakfu wa wanasayansi wa kitaifa nchini Marekani (NSF) kutuma setilaiti tatu ndogo angani ili kusaidia uchunguzi huo utakaofanyika kutoka ardhini.

Kulingana na Profesa Falcke, hatua hiyo itasaidia kujenga darubini kubwa yenye ukubwa zaidi ya dunia, itakayoweza kuchukua picha asili ya shimo hilo lililo katikati ya sayari.

Profesa Falcke ameiambia BBC News kuhusu mpango wa kundi hilo unaojulikana kama EHT, lenye wanasayansi 347 baada ya kupokea Dola za Marekani milioni tatu, kama tuzo kufuatia ufanisi wake.

Ijapokuwa Profesa Falcke ndiye aliyependekeza wazo hilo na kupigania kupata ufadhili, anasema kwamba tuzo hiyo inatambua juhudi zilizofanywa na kundi lote la wanasayansi hao.

Kundi hilo linashirikisha wanasayansi kutoka Ulaya, China, Afrika Kusini, Japan na Taiwan.

Habari Kubwa