Mwalimu mbaroni tuhuma za kumcharanga mapanga mpenzi

10Sep 2019
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Mwalimu mbaroni tuhuma za kumcharanga mapanga mpenzi

MWALIMU Joseph Msafiri anayefundisha Shule ya Msingi Namagubu iliyopo Ukerewe mkoani Mwanza, anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, kwa tuhuma za kumkata mapanga mpenzi wake, Neema Kabulu (19) mkazi wa Ukerewe na kumjeruhi vibaya.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Richard Abwao.

Tukio hilo lilitokea juzi usiku maeneo ya Old Shinyanga mjini hapa, wakati mwalimu huyo, ambaye ni mkazi wa Kata ya Iselamagazi Shinyanga Vijijini akiwa na mpenzi wake wamelala kwenye nyumba ya wageni ili kesho yake kwenda kumtambulisha ukweni Iselamagazi Shinyanga Vijijini, ndipo ukatokea ugomvi kati yao.

Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga, Richard Abwao, alisema kwamba mwalimu huyo alimkata mapanga mpenzi wake maeneo ya usoni, tumboni, na mkono wa kulia, hivyo kukimbizwa kupatiwa matibabu kwenye hospitali ya rufani ya mkoa huo, na kuwa hali yake si ya kuridhisha.

Abwao alisema Mwalimu Msafiri alikwenda na mpenzi wake  kwa ajili ya kumtambulisha kwa wazazi wake, lakini ukatokea ugomvi kati yao.

“Kwenye eneo la tukio yalipotokea mapigano hayo, tulikuta panga lililokuwa limetumika kumshambulia mwanamke huyo pamoja na nguo zenye damu,” alisema Abwao.

Alisema chanzo cha ugomvi huo ni wivu wa kimapenzi, kutokana na mwalimu huyo kumtuhumu mpenzi wake kuwa siyo mwaninifu kwenye mahusiano yao.

Aidha, alisema Jeshi la Polisi mkoani humo linamshikilia mwalimu huyo na kwamba taratibu zingine zikishakamilika atafikishwa mahakamani.

Habari Kubwa