Rivacu yakataa zuio la stakabadhi ghalani

11Sep 2019
Jaliwason Jasson
MANYARA
Nipashe
Rivacu yakataa zuio la stakabadhi ghalani

CHAMA Kikuu cha ushirika mkoani Manyara (Rivacu) kimekataa zuio la Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini ya kuzuia vyama vya ushirika kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani kununua mazao ya biashara.

mazao ya biashara.

Mwenyekiti wa Rivacu, Michael Tsaxara, imelikataa zuio hilo wiki iliyopita alipozungumza na Nipashe.

Alisema Tume ya Ushirika imeweka zuio kwa vyama vya ushirika kuanzia Septemba 3, kwa madai havina maghala ya kutosha, hivyo alisema kuweka zuio ni kukiuka waraka wa mrajisi namba 1 wa mwaka 2019 kwa biashara za mazao ya  dengu, choroko, ufuta, soya na mbaazi msimu wa 2019/2020 kupitia mfumo wa vyama vya ushirika.

Tsaxara alisema viongozi walioweka zuio la wakulima kuuza mazao yao

kwa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa kisingizio kwamba hamna maghala ya kutosha hawajasema kweli.

Mkoani  Manyara kuna maghala ya kutosha na  kila kijiji kina ghala.

Aidha, alisema iwapo watazuia mfumo huu Rivacu itapata hasara ya zaidi ya Sh. milioni tano ambazo zilitumiwa kununulia vifungashio.

"Kinachotushangaza  aliyeweka zuio  mfumo huu usiendelee kutumika

hajatushirikisha sisi wa vyama vya ushirika," alisema Tsaxara.

Alisema kusitishwa kwa mfumo huu kutasababisha hasara kwenye vyama vya msingi na halmashauri maana zilikuwa zinapata ushuru na

Rivacu yenyewe itapata hasara kwa kuwa wanunuzi hawataendelea kufanya kazi wakati Rivacu imeishaingia mkataba.

"Sisi hatuna tatizo la maghala hata kidogo kusema hakuna  si kweli na waliosema hawajui labda wanajua walichopewa,” alisisitiza Mwenyekiti wa Rivacu.

Msimamizi huyo wa ushirika alisema wao waliohamasisha mfumo huo kwa zuio hilo watashindwa kurudi kuutetea kwa wananchi maana maghala yapo halafu waambiwe hamna ni kitendo cha aibu.

Ofisa Shughuli wa Rivacu, Vivian Mahuto, alisema kusitishwa kwa mfumo wa stakabadhi ghalani ni kuwanyima ajira vijana ambao wanafanya kazi kwenye maghala na si kweli kwamba hamna maghala.

Alisema mfumo huu ni mzuri na kwa wakulima wa ufuta umezaa matunda kwa wakulima maana wameuza kwa Sh. 2,790 mpaka 3,000 na Rivacu ilitaka kuzindua mfumo huu Septemba 5, ila zuio hilo likawa kikwazo ambapo bei ya mbaazi ingetegemea soko linasemaje.

Lilian Macha, mkulima kutoka Masakta, alisema serikali isikubali zuio hilo kwa kuwa ni uongo na kwamba wana maghala ya kutosha.

Habari Kubwa