Tanesco kudhibiti wezi na vishoka

11Sep 2019
Woinde Shizza
ARUSHA
Nipashe
Tanesco kudhibiti wezi na vishoka

SHIRIKA la Umeme (Tanesco), mkoa wa Arusha, limetangaza operesheni  ya kuwabaini wezi wa umeme na vishoka, wanaowadanganya wateja kwa kujifanya maofisa wa shirika hilo.

Ofisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Tanesco, mkoa wa Arusha, Lucas Kusare, aliwaambia wanahabari kuhusu changamoto mbalimbali zinazolikabili shirika hilo.

Kusare alisema mbali na vishoka pia shirika hilo litawakamata wateja  wanaoiba umeme, ikiwa ni pamoja na wale wote

wanaojihusisha na vitendo vya kuhujumu miundombinu ya shirika kwa kuiba nyaya na mafuta ya transfoma.

“Pia tuna taarifa kuwa kuna wafanyakazi wa Tanesco wasio waaminifu ambao wanashirikiana na vishoka katika kuhujumu

miundombinu ya shirika, nao tutawabaini na kuwachukulia hatua za kinidhamu na tutakaowakamata tutawafikisha mahakamani,” alisema Kusare.

Akizungumzia kukatikatika kwa umeme mara kwa mara, katika maeneo mbalimbali mkoani hapa, Kusare alisema kwa kiasi kikubwa inasababishwa na wateja wengi kutojua kutumia rimoti za mita za umeme. “Mita hizi za sasa zinatumia rimoti na tulizifunga juu ya nguzo lengo

likiwa ni kukabiliana na vishoka na wezi wa umeme na ndio maana mteja anaongeza umeme kwenye mita yake, kwa kutumia rimoti, lakini imebainika kwamba nyingi zimeharibika kutokana na wananchi kushindwa kutumia ipasavyo,” alisema.

Mkuu huyo wa mawasiliano alisema hali hiyo imekuwa ni changamoto kubwa sana kwao na kwamba kwa sasa wanawasiliana na Tanesco makao makuu, kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo.

Aliongeza kuwa mbinu zinazotumiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya kifaa hicho wanapoongeza umeme.

Alisema kwa siku wamekuwa wakipokea taarifa zaidi ya 50 juu ya kuharibika kwa vifaa hivyo, ambapo baadhi wamekuwa

wakivipokea na kuvifanyia matengenezo madogo na kuwapa mwongozo juu ya matumizi sahihi ya vifaa hivyo.

Pia alitoa wito kwa makandarasi wote waliopewa kazi na shirika hilo, kuhakikisha kuwa wanafanya kazi zao kwa kufuata masharti na taratibu walizopewa na kuepuka kuwatumia vishoka ili kuepuka kusitishiwa mkataba wa kazi.

Habari Kubwa