Chama chasotea hati ya ardhi miaka 13

11Sep 2019
Godfrey Mushi
ROMBO
Nipashe
Chama chasotea hati ya ardhi miaka 13

WAKATI Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, akiwa ametoa ofa ya kupelekewa majina ya maofisa ardhi wanaochelewesha hati za ardhi, mambo ni tofauti kwa Chama cha Ushirika wa Mazao (Amcos) cha Tarakea kilichoko  Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi.

Chama hicho kinalia kukwamishwa na Idara ya Ardhi ya wilaya hiyo na Serikali ya Kijiji cha Kibaoni kupata hati miliki ya ardhi ya eneo lao kutokana na kufuatilia kwa miaka 13 sasa bila mafanikio.

Bodi ya chama hicho, imeweka wazi kwamba tatizo liko kati ya serikali ya kijiji na ofisi ya ardhi ya wilaya ya Rombo.

Kaimu Mwenyekiti wa Tarakea Amcos, Adam Sudi, alisema walianza mchakato wa kutafuta hati hiyo mwaka 2006 na mwaka 2007 walilipa ada ya upimaji katika idara ya ardhi ya Sh. 700,000 na kuwekewa alama za mipaka (beacons) na kisha kupewa fomu ili kuipeleka ofisi ya kijiji kupata baraka, lakini mpaka sasa  hawajawahi kurejeshewa fomu hiyo, licha ya kuulizia kila mara.

"Tumehangaika sana mpaka tumemwandikia barua yenye kumbukumbu namba TRCS/HW/R/B/5/32 ya Desemba 19, mwaka jana, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rombo kukumbushia barua yetu ya Oktoba 5, 2018 inayohusu jambo hili, lakini hadi sasa hatujapata jibu. Tunamwomba Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa Lukuvi aje atusaidie kumaliza utata huu, tujue tunakwama wapi.

Katibu wa Tarakea Amcos, Bertha Shirima, alisema nia yao ya kutaka Waziri Lukuvi kuingilia kati ni kutimiza maagizo yake aliyoyatoa ya kutaka kufikia Februari, mwaka huu, maeneo yote nchini yawe yamepewa hati miliki ili wahusika walipe kodi.

"Sisi tunataka kuanzisha duka kubwa la pembejeo na ‘hardware’ (vifaa vya ujenzi) ili kuwasaidia wakulima, kama tutapata mkopo kutoka benki lakini tunakwama kuendelea na mchakato kwa sababu ya kukosa hiyo hati. Tunamshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agness Hokororo, alipokuja hapa na alitoa amri kwa idara ya ardhi kutoa hati hiyo ndani ya siku 14, lakini hadi leo watendaji wa idara hiyo hawajatii agizo hilo," alisema Shirima.

“Agosti 10, 2006 tulipata barua kutoka Ofisi ya Ardhi Wilaya ikituonyesha gharama, upimaji, upitishaji kibali wizarani, ulipaji na upatikanaji wa hati miliki na Novemba 11, chama hiki kilikabidhi hundi namba 062643 yenye thamani ya Sh.  700,000 ambayo ilikabidhiwa kwa ofisa ardhi," aliongeza.

Mmoja wa wakulima wanaotegemea chama hicho, Didas Kireti, alieleza masikitiko yake kuhusu njama za makusudi za kukwamishwa kwa mchakato wa kuiendeleza Tarakea Amcos, akisema hatima yao hivi sasa iko mikononi mwa Waziri Lukuvi na Rais John Magufuli ambao wanaweza kuwahoji wahusika na kuchukua hatua.

Alipotafutwa Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kibaoni, Mathew Matoli, kutoa ufafanuzi kuhusu madai ya ofisi yake kukwamisha mchakato huo, simu yake ilikuwa ikiita bila majibu.

Hata hivyo, juhudi za kumtafuta kujibu madai hayo zinaendelea lakini pia gazeti hili limechukua hatua ya kwenda kumtafuta Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Rombo kupata kauli yake kuhusu kukwama kwa hati hiyo.

Habari Kubwa