Leseni 10,000 zaozea ofisi TRA

11Sep 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Leseni 10,000 zaozea ofisi TRA

MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kilimanjaro, imesema kuna zaidi ya leseni 10,000 za madereva wa magari ambazo zimekamilika, lakini wahusika wamezitelekeza bila kuzichukua kwa muda mrefu sasa.

Meneja wa TRA mkoani wa Kilimanjaro, Gabriel Mwangosi, alisema jana kuwa ziko leseni ambazo zilitelekezwa au kuachwa kwa muda mrefu hadi muda wake wa matumizi kwisha na maofisa wake kulazimika kuziteketeza kwa kuzichoma moto.

Mwangosi alisema hayo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, kwenda kukagua shughuli zinaziofanywa na maofisa wa TRA na kuzungumza nao kuhusu mambo mbalimbali.

"Mpaka sasa kuna zaidi ya leseni 10,000 ambazo zimeshakamilika lakini wahusika wenyewe hawajajitokeza kuchukua leseni zao, na zipo ambazo tumeziteketeza kwa kuchoma moto, baada ya muda wake kuisha bila wahusika wenyewe kuchukua," alieleza.

Kwa nyakati tofauti, baadhi ya watu wanaoomba leseni katika mamlaka hiyo, wamekuwa wakilalamikia kucheleweshwa kwa leseni hizo wakidai kwamba wanaambiwa hakuna karatasi ngumu za kutoa leseni hizo.

Akizungumza baada ya kufanya ukaguzi chumba kwa chumba, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk. Anna Mghwira, alisema mmlaka ya mapato nchini, ndiyo inaweza kuisaidia Wizara ya Viwanda katika kufikia malengo ya Tanzania ya viwanda kwa kuwaelimisha wananchi kufanya biashara halali.

Dk. Mghwira alisema jukumu la TRA si kuwekeza katika ukusanyaji wa kodi pekee bali pia ina jukumu kubwa la kuwaelimisha wananchi ili kuongeza wigo wa biashara kwa kufungua viwanda pamoja na kufanya biashara halali.

Pamoja na mambo mengine, Mkuu huyo wa mkoa alikitaka kitengo cha uwezeshaji wananchi kiuchumi katika mkoa huo, kufanya kazi na TRA upande wa forodha ili kuhakikisha wanawasaidia wafanyabiashara wanaofanya biashara za magendo kuachana na shughuli hizo.

Habari Kubwa