Walimu wezi wa mitihani waonywa

11Sep 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Walimu wezi wa mitihani waonywa

WAKATI leo wanafunzi wa darasa la saba wakitarajia kuanza mtihani wao wa mwisho wa kuhitimu elimu ya msingi, walimu wametakiwa kuwa waaminifu katika usimamizi ili kuondokana na udanganyifu (uvujishaji) wa mtihani.

Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu nchini (CWT), Mwalimu Deus Seif.

Rai hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu nchini (CWT), Mwalimu Deus Seif, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu  mtihani wa darasa la saba.

Alisema walimu wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha mtihani huo unafanyika katika hali ya uaminifu wa hali ya juu ili wanafunzi kila mmoja afaulu kutokana na uwezo wake na siyo njia ya udanganyifu.

"Walimu tunatakiwa kufanya uaminifu wetu kwa asilimia kubwa sana ili kuzuia vitendo vyote vya udanganyifu ambavyo vitafanyika katika mtihani huu unaoanza nchini kote kesho (leo)," alisema Seif.

Alisema walimu wanatakiwa kuwa waaminifu ili kurejesha imani iliyokuwapo ya kusimamia bila ya kuwapo na mgambo wala Jeshi la Polisi.

"Natamani sana hali ya usimamizi wa mitihani irudi kama ilivyo kuwa zamani, uaminifu ulikuwa katika hali ya juu sana walimu tulisimamia mitihani sisi wenyewe, lakini hivi sasa tumepewa mgambo hali ikiendelea hivi siku moja tutalindwa na vifaru vya kivita," alisema.

Alisema pamoja na kuwa CWT ni kwa ajili ya kuwatetea walimu, lakini kwa yule ambaye atashiriki katika vitendo vya udaganyifu atakumbana na mkono wa sheria hivyo ni lazima wakatimiza wajibu wao.

"CWT ni kwa ajili ya kuwatetea walimu, lakini ili kuondoa adha ya kutumia gharama katika kuwatetea watakao jiingiza katika vitendo vya udanganyifu wa mitihani, ipo haja sasa kutimiza wajibu ili kukisaidia chama chetu kuondokana na usumbufu," alisema.

Alizitaka shule binafsi kuacha tabia ya kununua mitihani na kuwapatia majibu wanafunzi wao kwa kuwa hali hiyo inashusha hadhi yao.

Katibu mkuu huyo alizitaka mamlaka husika za serikali ambazo zinahusika na mtihani huo kutimiza majukumu yake ili kuondoa usumbufu utajitokeza kwa walimu.

"Ni imani yangu kuwa serikali imejipanga na yale malalamiko ya walimu pia hayatakuwapo wakati huu kama ambavyo imekuwa kipindi kilichopita, Tamisemi pamoja na Baraza la Mitihani najua wamejipanga kuwezesha mtihani huu muhimu wa darasa la saba," alisema Seif.

Habari Kubwa