Serikali yaonya mila zinazonyanyasa wajane

11Sep 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Serikali yaonya mila zinazonyanyasa wajane

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu, amesema mila na dini zisizo na hitilafu haziwezi kuruhusu wajane kunyanyaswa katika jamii.

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii, Dk. John Jingu

Dk. Jingu aliyasema hayo jijini Dodoma kwenye kongamano la tisa la wajane lilioandaliwa na Taasisi ya 'Amazing Grace' la kuwajengea uwezo wajane ili waweze kupambana na changamoto mbalimbali katika jamii.

Alisema jamii ina wajibu wa kumlinda mjane na vitendo vyote vya unyanyasaji dhidi yake kwa kuwa hata vitabu vya dini vimeipa jamii jukumu hilo la kuwasaidia na kuwalinda wajane dhidi ya unyanyasaji wowote.

Dk. Jingu alifafanua kuwa hakuna mila wala dini zilizo nzuri zinazoruhusu wajane kunyanyaswa, kunyang'anywa nyumba zao na kudhulumiwa haki zao za msingi kama ardhi, nyumba, magari na mali nyingine na hata wakati mwingine kunyang'anywa watoto.

"Hakuna mila inayosema mjane apokonywe vitu alivyochuma na mwenzi wake hiyo dhana potofu iliojengeka machoni mwa jamii," alisema Dk. Jingu.

Alisema kuwa wajane ni kundi maalum katika jamii ambalo serikali, jamii na mtu mmoja mmoja tuna wajibu wa kuwalinda na hivyo serikali imejizatiti katika kuwasaidia wajane kutatua changamoto zinazowakabili.

Dk. Jingu aliainisha mambo yanayopaswa kuwasaidia ni utoaji wa elimu bure na watoto wengi ambao ni yatima kutoka familia za wajane wamepata fursa ya elimu ya msingi, sekondari na hata kufikia vyuo vikuu, uwapo wa mifuko ya uwezeshaji wananchi kiuchumi inayosaidia kuwapa wajane mikopo inayowawezesha kujikwamua.

"Hakuna mila wala dini inayoruhusu wajane wanyanyaswe ila kama zipo basi zitakuwa na hitilafu na hazifai katika jamii hivyo zinapaswa kuangaliwa," alisema Dk. Jingu.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Amazing Grace, Paulo Mwanga, alitoa wito kwa jamii kuacha kuwafanyia wajane vitendo vya kikatili vya uonevu ili waweze kuishi kwa kuwa mama mjane akipoteza amani jamii nzima inakosa.

"Na tutakuwa na familia legelege kiuchumi, kijamii na kiutamaduni maana wajane ni sehemu ya jamii ambayo ni nguvu kazi ya jamii na wanatakiwa kutendewa haki ili kujenga taifa imara," alisema.

Kwa upande wake Beatrice Muinuka kutoka Mkoa wa Mbeya, ambaye ni mjane alisema kongamano hilo limewasaidia kutambua haki zao kama wajane na wanaishukuru serikali kwa hatua mbalimbali ikiwamo fursa katika maeneo yao ya kupata mikopo itakayowawezesha kujikwamua kiuchumi na kuendesha maisha yao.

Alisema wajane wanapaswa kujitokeza kuchangamkia fursa hizo ambazo wanaamini zitawasaidia kuendesha maisha yao ya kila siku ikiwamo kujikwamua kiuchumi.