Ikulu Z’bar kusomesha zaidi

11Sep 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Ikulu Z’bar kusomesha zaidi

SERIKALI ya Zanzibar, itaongeza nafasi za masomo kwa wanafunzi bora wa kidato cha sita  wanaodhaminiwa na serikali.

Mwaka jana ilitoa nafasi 30 na kwamba mwaka huu zimeongezwa hadi 60 na wanufaika ni  wanafunzi bora wa kidato cha sita wenye viwango vya juu  vya ufaulu.

Akizungumza Ikulu katika hafla ya kuwapongeza wanafunzi bora wa kidato cha nne na cha sita waliofanya vizuri katika mitihani ya taifa, Rais wa Zanzibar Ali Mohamed Shein,  alisema  idadi hiyo aliyoiongeza mwaka huu ni mara mbili ya nafasi za ufadhili wa masomo ambazo alizitoa mwaka jana kwa wanafunzi bora wa kidato cha sita.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inaendelea na utaratibu wa kuwapa udhamini wanafunzi bora wenye viwango vya juu vya kufaulu kwa masomo ya sayansi na sanaa.

Alisema kuwa mwaka huu ameongeza nafasi hadi kufikia 60 badala ya 30 za mwaka jana kwani aliahidi kuendeleza utaratibu huo ili kupata wataalamu wa fani mbali mbali watakaoendelea na masomo yao ndani na nje ya nchi.

Rais Shein  alisema: “Pia natoa pongezi kwa wanafunzi 187 waliofaulu kwa daraja la kwanza katika mtihani wa kidato cha nne mwaka jana pamoja na shule bora  10 ambazo ufaulu wa mwaka jana ulikuwa ni wanafunzi 135.”

Aidha, aliwapongeza wanafunzi wote 188 wa kidato cha sita hasa vijana wanne waliofaulu kwa alama  nne kila mmoja na kuonyesha uwezo mkubwa walionao.

Dk. Shein alieleza kuwa kwa mara nyingine tena wanafunzi wa kike wameonyesha uwezo mkubwa wa kufanya vyema katika mitihani ya taifa na hasa kwa masomo ya sayansi na kuwapongeza wanafunzi hao.

“Wazee walisema mcheza kwao, hutunzwa na chanda chema, huvikwa pete. Kauli zote hizo za wazee wetu zinasibu kwenu. Kwa hivyo, tumeamua kuwaandalia hafla hii kwa ajili ya kuwaenzi kwa sababu mmecheza vyema kwa ajili yenu na kwa ajili ya nchi yenu,” alisema Dk. Shein.

Kadhalika aliwataka walimu wasiozingatia vyema majukumu yao na kuyakiuka maadili ya ualimu wajirekebishe kwani kazi hiyo ni ya watu wenye heshima kubwa katika jamii.

Aidha, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali, Riziki Pembe Juma, alieleza mafanikio yaliopatikana katika sekta ya elimu na kutumia fursa hiyo kutoa pongezi za pekee kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi zake za makusudi za kuimarisha sekta ya elimu hapa nchini.

Waziri Pembe alieleza kuwa Rais Shein anaendeleza nyayo za waasisi wa taifa Mzee Abeid Karume pamoja na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere za kuimarisha sekta ya elimu na kukuza sekta zote za maendeleo kwa watu wote.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara Dk. Idrisa Muslim Hijja alieleza kuwa mafanikio yote yaliopatikana katika sekta ya elimu ni juhudi za Rais Dk. Shein katika kuhakikisha anaweka mazingira bora kwenye sekta ya elimu.

Habari Kubwa