Utoroshaji maliasili kiholela wapata dawa

11Sep 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Utoroshaji maliasili kiholela wapata dawa

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema kuwapo kwa kanuni bora za sheria za wanyama na miti asilia kutasaidia kupunguza usafirishaji haramu wa rasilimali hizo nje.

Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri

Hayo yalisemwa na Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Mmanga Mjengo Mjawiri, wakati aliposhiriki mkutano wa kuweka kanuni za sheria kuhusu udhibiti wa usafirishaji wa wanyama asilia na miti nje ya nchi.

Alisema lengo la kuweka kanuni hizo si kuzuia moja kwa moja biashara ya aina hiyo, lakini ni kuweka mwongozo utakaosaidia udhibiti wake.

Alieleza kuwa sheria na kanuni kama hizo zipo kwa upande wa Tanzania Bara ambazo zimesaidia kudhibiti wanyama wakiwamo walio katika hatari ya kutoweka.

''Kanuni za udhibiti wa wanyama pamoja na miti ni muhimu ili kuona rasilimali hizo zinalindwa kwa mujibu wa sheria na kuepuka kutoweka ,'' alisema Mjawiri.

Mkurugenzi wa Idara ya Maliasili na Mali Zisizorejesheka, Soud Mohamed, alisema katika siku za hivi karibuni kumejitokeza matukio mbalimbali ya kutaka kusafirisha miti maarufu nje ya nchi.

Aliitaja miti ambayo ilikuwa ikitaka kutoroshwa kuwa ni mibuyu iliyokusudiwa kupelekwa nje ya nchi kwa matumizi mbalimbali.

''Tumezuia usafirishaji wa mibuyu kwa sababu ya hofu ya kutoweka kwa miti hiyo hadi hapo uchunguzi zaidi utakapofanyika,'' alisema Mjawiri.

Alisema udhibiti wa miti na wanyama unafanyika kwa mujibu wa sheria Namba 10 ya mwaka 1996 ambayo mikakati yake ni kulinda rasilimali za taifa zisivunwe kiholela.

Baadhi ya wanyama wanaochukuliwa na kusafirishwa kinyume na sheria ni pamoja na kobe na kima punju ambao hawapatikani kokote duniani isipokuwa Zanzibar.

Habari Kubwa