Bocco atamani kuanza kuijaribu Mtibwa Ijumaa

11Sep 2019
Shufaa Lyimo
DAR ES SALAAM
Nipashe
Bocco atamani kuanza kuijaribu Mtibwa Ijumaa

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara, Simba, wamezidi kuimarika safu yao ya ushambuliaji baada ya straika John Bocco kurejea kujifua na wenzake huku akieleza kwa sasa hali yake inaendelea vizuri na yupo tayari kupambana.

Straika John Bocco

Bocco aliumia mguu wakati wa mechi ya marudiano ya raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya UD Songo ya Msumbiji iliyopigwa Uwanja wa Taifa mwezi uliopita, na aliukosa mchezo wa ufunguzi wa Ligi Kuu dhidi ya JKT Tanzania ambao Simba ilianza kwa ushindi wa mabao 3-1. 

Akizungumza na Nipashe jana, Bocco alisema yupo tayari kupambana katika mechi dhidi ya Mtibwa Sugar Ijumaa wiki hii, kama kocha atampa nafasi.

"Kwa sasa nashukuru naendelea vizuri, nikipata nafasi ya kupangwa nitacheza," alisema mshambuliaji huyo.

Alisema anaupa umuhimu mkubwa mchezo huo kwa kuwa malengo yao ni kushinda katika kila mchezo.

"Lengo langu ni kuipa mafanikio timu yangu na kutetea kombe letu la ubingwa msimu huu,"alisema.

Aliongeza kuwa Ligi Kuu msimu huu imeanza kwa ushindani mkubwa, huku akiwataka mashabiki wao kuendelea kuwapa ushirikiano ili waweze kufanya vizuri na hatimaye kutetea ubingwa wao.

Aidha, alisema licha ya kutolewa mapema katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika Mashabiki wasikate tamaa na kuwaahidi watajipanga upya mwakani.

Habari Kubwa