KMKM, Jang'ombe kukata utepe Ligi Kuu Z'bar

11Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
ZANZIBAR
Nipashe
KMKM, Jang'ombe kukata utepe Ligi Kuu Z'bar

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Zanzibar, Mabaharia wa KMKM, Ijumaa watashuka katika Uwanja Amaan majira ya saa kumi alasiri kufungua pazia la ligi hiyo dhidi ya timu ya Jang'ombe Boys.

Pazia la Ligi Kuu Zanzibar linatarajia kufunguliwa rasmi Ijumaa ambapo zitapigwa mechi tatu katika viwanja vya Mau, Amaan na Gombani kisiwani Pemba.

Awali ligi hiyo ilipangwa kuanza Septemba 6, mwaka huu, lakini ilisogezwa mbele kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kutoa muda kwa klabu shiriki kupitia pingamizi za usajili.

Akizungumza na gazeti hili juzi, Rais wa Jang'ombe, Ali Othman maarufu Kibichwa, alisema katika kujiandaa na mchezo huo wamepiga kambi ya wiki moja ili kuhakikisha wanatoka na alama tatu.

Alisema msimu huu watahakikisha timu ya Jang'ombe Boys inafanya vizuri tangu mwanzo mwa ligi hiyo ili kuepuka kufanya vibaya kama msimu uliopita ambao walishindwa kumaliza ligi wakiwa nafasi za juu.

"Tumeweka kambi hapa hapa visiwani Zanzibar na lengo letu ni kuhakikisha wachezaji wanakuwa imara kuelekea mchezo huo wa ufunguzi ambao tunahitaji kushinda," alisema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mashindano wa Shirikisho la Soka Zanzibar (ZFF), Ali Mohamed, aliliambia gazeti hili kuwa klabu zote zinapaswa kufuata ratiba za ligi hiyo kama zilivyopangwa ikiwamo kwa timu ambazo zinapaswa kusafiri kuelekea kisiwani Pemba kufanya hivyo kama ratiba hiyo inavyoonyesha ili kuepuka changamoto ya usafiri.

Ligi Kuu ya Zanzibar ambayo bado haijapata mdhamini, inashirikisha jumla ya timu 16 ambazo ni KMKM, Mafunzo, JKU, KVZ, Polisi, Zimamoto, Chuoni, Malindi, Mlandege, Selem View, Mwenge, Chipukizi, Jamuhuri, Jang'ombe Boys, pamoja na timu mbili zilizopanda msimu huu, Kipanga kutoka Unguja na Machomane ya Pemba.

Habari Kubwa