Hongera wanafunzi wa darasa la saba

11Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Hongera wanafunzi wa darasa la saba

KILA la heri  watoto wanaohitimu  darasa la saba ambao leo mnaanza mitihani yenu. Ndivyo tunavyoweza kuwapongeza kwa kufanikisha na kukamilisha safari ya elimu ya shule ya msingi.

Wanafunzi wa shule za msingi wanaoanza mitihani leo ambayo itakamilika mwisho wa wiki hii wanapitia changamoto nyingi, ndiyo maana si wakati wa kuwakumbusha mlivyoteseka wala mlivyohangaika hadi kufikia hatua hiyo, bali ni wasaa mwingine wa kuwafariji na kuwashauri kufanya  kile  taifa linachowategemea.

Serikali inawezeka mabilioni ya fedha kwa ajili ya kufanikisha  elimu ya msingi kwa hiyo si jambo jema wazazi na walezi kuwahimiza mabinti na wavulana kuandika majibu ‘feki’ ili kujaza vitabu vya mitihani.

Kwa mfano kuchora ‘zombi’  (misukule) kutukana matusi ya nguoni na kuchora michoro isiyoeleweka, huwasaidii wala taifa.

Fedha zinazotolewa na serikali kila mwezi ili kusomesha watoto na nyingine wazazi wanazowekeza kwenye chakula, mavazi, madfatari ,vitabu na nauli ni muhimu zikaleta matokeo.

Ndiyo maana tunategemea walezi na wazazi wasiwahimize mabinti kuandika majibu ya uongo ili wasifaulu kwenda sekondari, kisa wanataka warudi nyumbani wakaolewe.

Aidha, wapo wazazi wanaowatisha watoto wao kuwa ukifaulu shauri yako, mimi sina hela za kukusomesha zaidi, faulu utajua mwenyewe.

Kwa wasichana wapo wanaokataliwa kusoma kwa kuwa wazazi  au walezi wanawapendelea zaidi vijana wanaume kuliko mabinti nao na wanabaniwa kuwa wasijitahadi kwa kuwa shule kwao, darasa la saba ndiyo kikomo.

Tunawashauri wazazi wa Tanzania kubadilika ni wakati wa kuwaeleza watoto wetu haja ya kusoma. Tunatakiwa kuwafahamisha kuwa ni lazima kusoma kwani kila jambo katika dunia ya sasa ni lazima usome na uwe na utaalamu.

Wazazi wawahimize watoto kusoma na kufuatilia masuala ya taaluma si kuwakatisha tamaa na kuwarudisha nyuma kimasomo.

Kumwambia binti aache masomo ili akaolewe ni kama kumtia kitanzi. Kwanza ni uvunjaji wa sharia , lakini ni kumwingiza kwenye hatari za kupata matatizo ya uzazi ambayo wakati mwingine ni kifo.

Umri mdogo unaweza kuchangia vifo vya mabinti wakati wa kujifungua. Aidha , hata malezi ya mtoto anayelelewa na mama mwenye umri mdogo yanaweza yasiwe na manufaa kwani ni sawa na mtoto kumlea mtoto mwenzake.

Wazazi na walezi wafahamu kuwa maelezo kuwa elimu ni ufunguo wa maisha ni ukweli bila kipingamizi. Kwa elimu kijana anayopata ataweza kujiajiri, kumudu maisha yake na pia kuchangia uchumi wa familia na taifa.

Kwa hiyo huu uwe mwanzo wa wazazi na walezi kuwahimiza watoto wetu kusoma na kufanya vyema katika mitihani yao badala ya kuwahamasisha kutoa majawabu yasiyofaa kwenye mitihani.

Ikumbukwe utajiri pekee mzazi anaoweza kumpa na kumwachia mwanae ni elimu ambayo itamtengenezea taaluma na huo ndiyo ufunguo kwenye maisha yake.

Elimu ndiyo zawadi pekee ambayo hakuna wa kumnyang’anya. Ndiyo ambayo itainyanyua familia maskini , tena ndiyo barabara ya kuwatoa katika ujinga, umaskini na maradhi.

Kwa hiyo mtihani wa darasa la saba unaofanyika leo uwe mwanzo wa kuwahamasisha na kuwaandaa  watoto wetu wa kike na kiume kusoma zaidi na kupenda shule zaidi.

Wanapomaliza mitihani hii tuwahimize kusoma, kujifunza zaidi na kujiandaa kuwa wabunifu, wataalamu na mabingwa kwenye Nyanja mbalimbali.

Ndiyo wakati wa kuwaeleza kuwa bila elimu hakuna maisha bora na ukikosea kwenye kujifunza, kujipanga na kujiendeleza kielimu unaweza usiwe na maisha bora.

Tunawatakia kila la kheri wanafunzi wote wanaomaliza  darasa la saba leo.