Robert Mugabe, 1924-2019

11Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Robert Mugabe, 1924-2019
  • *Kama Gaddafi, aliichanganya dunia kwa kupendwa, kuchukiwa kwa kiwewe

MPIGANAJI Robert Mugabe hatimaye amejisalimisha na kuaga dunia wakati viungo vikiwa vimedhoofu kwa muda, kwa miezi kadhaa akawa anatibiwa katika hospitali jijini Singapore.

Marehemu Robert Mugabe, Rais wa zamani wa Zimbabwe.

Ni hospitali aliyokuwa amechagua na kuizoea, iwe ni kutokana na masuala ya kitaaluma au urafiki binafsi, kwani alikuwa rafiki mkubwa wa Jamhuri ya Watu wa China, ambayo ina uhusiano wa kijadi na Singapore, ila hawana itikadi moja.

Wakati anatibiwa mara kadhaa zilitangazwa taarifa potofu za kifo chake, kuanzia alipoondolewa rasmi madarakani na jeshi mwezi Novemba 2017, taarifa za kifo zikaanza Machi 2018 na kuendelea tu.

Hulka ya kuwa mpiganaji ndiyo inayoweza kujumuisha maisha na kazi ya hayati Mugabe, kwa sababu kwa vipindi virefu vya maisha yake alikuwa katika mapambano.

Kuna wakati kulikuwa na kipindi kirefu cha amani bila mapambano ya wazi, na wengi walitazamia kuwa hali ingeendelea hivyo lakini ilikuwa ni taswira danganyifu, kwani masuala ya msingi ya mapambano yalikuwa hayajatatuliwa bado.

Ni kipindi cha miaka 10, au labda tuseme 20 kuanzia kupatikana kwa uhuru mwaka 1980 hadi mwisho wa karne, yaani Nelson Mandela alipoondoka madarakani Afrika Kusini 1999, Zimbabwe ikafumuka punde tu.

Mazingira ya amani yalitokana na kukubaliwa katika mkutano wa Lacanster House nchini Uingereza mwaka 1979 wa misingi ya Katiba ya Zimbabwe, ambako Wazungu nchini humo walipewa viti 20 kati ya 100 na hakuna mabadiliko ambayo yangetokea katika mfumo wa umiliki ardhi kwa muda wa miaka 10.

Hadi kufika mwaka 1990 muda huo ukawa umeisha kwa hiyo suala hilo lingeleta utata kama ufumbuzi muafaka kati ya Zimbabwe na Uingereza usingefikiwa.

Lakini Mugabe akalazimika kusimama wima asiguse kitu, kwani wakati huo Mandela ndiyo alikuwa ametolewa jela na yuko katika mazungumzo ya kuunda serikali ya wengi.

Ina maana Mugabe angeifumua Zimbabwe kubadili mfumo wa umiliki ardhi baada ya kipindi cha miaka 10 kikatiba kupita, angeingiza hitilafu katika majadiliano nchini Afrika Kusini, hivyo akatoa mchango wake wa kuzuia kutumia uhuru wa nchi hiyo hadi suala hilo nyeti limalizike kwanza.

Na hata Mandela alipoingia madarakani 1994, ilibidi Mugabe aendelee ‘kukanyaga mafiga’ ili Mandela afaulu katika jitihada ya kujenga kuaminiana katika utawala mpya wa walio wengi.

Ni pale Mandela alipomaliza muhula wake mmoja aliojipangia na kustaafu, ndiyo sasa Mugabe akawa huru, akawaambia Waingereza ni muda sasa wa kumaliza suala la ardhi, watoe fedha ili Waafrika wanunue sehemu kubwa ya mashamba ya Wazungu.

Ndicho kilichofanyika Kenya wakati wa uhuru mwaka 1963 Desemba, kuwa Uingereza iliingiza fedha katika benki, ikatumika kuwakopesha Waafrika kwa riba ndogo wanunue mashamba ya Wazungu waliokuwa tayari kuondoka.

Na kimsingi ndicho kilichokubaliwa kwenye mkutano wa Lacanster mwaka 1979, lakini Uingereza ikaanza kutoa visingizio kwanini isitekeleze makubaliano hayo.

Katika akili ya watawala wa Uingereza, suala hilo limegeuka sura baada ya miaka 20, yaani imekuwa ni hali ya kawaida nchini humo ambayo wanatakiwa waizoee.

Na kama ni mikopo kununua mashamba, benki zipo huko.

Msimamo huo wa Waziri Mkuu Tony Blair ulimrudishia Mugabe roho ile ya uanaharakati na upiganaji. Kwa jumla ilikuwa imefifia, huku akijaribu kujenga taifa lisilo na ubaguzi au chuki za kikabila. Ila kuna tukio ambalo liliweka doa utawala wa Mugabe katika miaka ya awali, linaitwa Operesheni Gukurahundi.

Lilitokana na ‘uvinjari madaraka’ (Kiingereza, adventurism) kwa upande wa aliyekuwa kiongozi mwenza wa ZANU-Patriotic Front, mkongwe Joshua Nkomo ambaye alitaka kuwa Makamu wa Rais mwenye mamlaka makubwa, kama walivyotaka kina Dk. Riek Machar wa  Sudan Kusini au Dk.Jonas Savimbi wa Angola.

Iliposhindikana kuwa na madaraka hayo inaelekea aliandaa uasi, zikapatikana silaha nyingi zimefichwa kwenye shamba moja ambako Nkomo anahusika, ila kwa vile hapakuwa na uchunguzi halisi ulio huru na kuthibitisha, huwezi kusema hapakuwa na ‘false flag operation.’ Ni kutegewa kitu ili vita vitangazwe.

Operesheni hiyo ilifanywa na jeshi la nchi hiyo lililosheheni wapiganaji wa chama cha ZANU cha Mugabe huku wapinzani wao wakiwa ni kundi la Nkomo la Patriotic Front, iliyokuwa inaitwa ZAPU awali. 

Ilielezwa kuwa jeshi la Zimbabwe lilikuwa likishauriwa au kusimamiwa kwa mafunzo ya wahenyeshaji kutoka Korea Kaskazini, ambayo unaweza kusema ilipewa nafasi hiyo ili China isiingie kwa nguvu katika Afrika kijeshi, hali ambayo ingeweza kuleta matatizo kati ya Zimbabwe na nchi za Magharibi.

Watu wengi wa kabila la Ndebele (au Matebele) waliuawa, na maelfu wengine wakakimbia.

Suala hilo hata hivyo halikuwa linasikika katika siasa za Zimbabwe miaka ya baadaye hasa baada ya Mandela kutolewa kifungoni kwani hili la mashamba ya Wazungu lilichukua nafasi kubwa na ndiyo hasa limekuwa ‘suala la maisha’ kwa uongozi wa Mugabe.

Alipoona kuwa Uingereza haitatekeleza sehemu yake katika makubaliano ya Lacanster, Mugabe alijua hakuna njia nyingine ila Wazungu kunyang’anywa ardhi hiyo na Waafrika waipate bure au kwa malipo kidogo serikalini kwa sababu ni yao.

Ni hoja ambayo ilikuwa haina ubishi kwa mamilioni ya Waafrika, iwe ni Zimbabwe au kwingineko, Mugabe akapata sifa.

Ila hatua hiyo iliambatana na kuporomoka kwa uchumi wa Zimbabwe kwa vile mfumo wa amana za benki na kwa maana hiyo thamani ya fedha na upatikanaji wa fedha kuendesha shughuli za kilimo na viwanda kuendana na mahitaji yaliyopo, kulitegemea uwepo wa Wazungu na amana zao benki.

 Kuondolewa kwa sehemu kubwa kulifanya Zimbabwe iwe ni nchi ya wakulima wa jembe la mkono, serikali inayohitaji gharama kubwa kuiendesha, na madini ya hapa na pale kusaidia kununua mafuta kutoka nje.

Siyo tena kilimo cha tumbaku na hata mazao ya chakula yalisuasua, au kuweka ng’ombe wa kisasa, waanze upya.

Unaweza kusema kuwa sababu ya Mugabe kuchukua hatua hiyo ni ‘ulevi tu’ wa siasa ya Ujamaa kwa jumla, kuwa alikuwa hajui matokeo yake, kama ambavyo nchi nyingi zilizofanya mapinduzi kuwaondoa ‘wanyonyaji’ au ‘mabepari na makabaila’ waliishia kuvuna mabua uchumi ukiporomoka.

Hatua ya Mugabe ilifanana na Jenerali Idi Amin ambaye hatua yake ya kuwafukuza Wahindi na kuchana hati zao za kusafiria mwaka 1972, kulileta mporomoko wa jumla wa uchumi wa nchi hiyo, kuparaganyisha sekta za biashara na fedha.

Na kuunda tabaka la walanguzi (Mafuta Mingi) lililotawala hadi akaanguka 1979.

Unaweza kusema kuwa maisha ya Mugabe na uongozi wake yalikuwa kielelezo cha Uamsho wa kizalendo na kimapinduzi katika Afrika kwa kipindi cha kufikia uhuru, halafu mapambano ya jumla ya ukombozi, kung’oa ukoloni mkongwe au madhira yake katika suala la ardhi. 

Licha ya tabu ambayo Zimbabwe ilipata, Mugabe aliendelea kuungwa mkono na watu wengi, hata kudiriki kufanya uchaguzi ambao licha ya vizuizi maridhawa kwa upinzani, ulienda vyema kiasi, ikaundwa serikali ya pamoja lakini Mugabe akatumia katiba na ‘uamirijeshi mkuu’ kuwabana wapinzani.

Wakajivuruga, wakasahaulika...

Habari Kubwa