Ndege kuzuiwa Afrika Kusini kulikoni?

11Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ndege kuzuiwa Afrika Kusini kulikoni?

‘KWELI kikulacho kinguoni mwako’ ingawa ni usemi lakini kuna ukweli ndani yake.

Rais John Magufuli (katikati), akisalimiana na mmoja wa marubani walioleta ndege mpya zilizonunuliwa na serikali kwa ajili ya Shirika la Ndege nchini (ATCL), nyuma yake ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Haiji akilini kwa Mtanzania anayefahamu historia kati ya Tanzania na Afrika Kusini ulivyo akaweza kuamini kilichotokea Johannesburg!

Tusemeje juu ya hilo, maana inabaki kuwa kitendawili kinachotakiwa kuteguliwa haraka iwezekanavyo.

Je, ni matokeo ya Ibilisi anayehangaika duniani kutaka kuleta mafarakano na kutokuelewana kinyume na mapenzi ya Mungu?.

Naamini kuwa Mungu wetu tunayemcha na kumwabudu ni mwema sana na mwenye upendo mwingi kwetu, hivyo ataendelea kuitakia mema nchi yetu.

Hata hivyo, ni wajibu wetu kumshukuru kwa kila jambo ikiwemo hili la Amri ya Mahakama Kuu ya Gauteng, Johannesburg kuizuia Ndege yetu isitoke na baadaye kuiachia baada ya hoja za msingi za kisheria zilizowasilishwa na Serikali yetu kwenye Mahakama hiyo.

Kwa mara ya kwanza nilisikia taarifa ya kukamatwa ndege yetu kupitia idhaa ya Kiswahili ya Radio Dutch-Welle (DW) ya Ujerumani saa 12 asubuhi, Agosti 26, 2019.

Kupitia taarifa ya habari nikasikia Ndege ya Tanzania imezuiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliva Tambo Jijini Johannesburg.

Kilichonishitua zaidi ni pale niliposikia kuwa imekataliwa kuondoka kwa sababu Taifa linadaiwa mamilioni ya fedha kutoka kwa mtu ambaye mali zake zilitaifishwa miaka ya nyuma.

Kwamba Mahakama Kuu-Gauteng Jijini Johannesburg, iliamuru Ndege ya ATCL ikamatwe.

Vilevile, Agosti 27, 2019 Gazeti Mwananchi Toleo Na.6960 liliandika: “Siri ya miaka 37 iliyoiponza ndege ya ATCL, Afrika Kusini”.

Kusema kweli hii ni dalili ya aina fulani ya “figisufigisu” kutoka kwa baadhi ya watu wasioitakia mema Tanzania.

Kudaiwa siyo dhambi, lakini kwa nini ndege yetu ikamatwe kwa kisingizo cha deni? Cha kusikitisha zaidi ni kuibuka madai hayo mwaka 2019.

Ingawa huwa tunasema kila kitu ni wakati lakini tujiulize deni lilisubiri Tanzania inunue ndege halafu itakapokwenda Afrika Kusini ikamatwe?

Kipindi cha miaka 37 siyo kifupi je, aliona hakuna kitu cha thamani cha kukamata ila sasa ndege zipo ikawa fursa kwenda mahakamani ili ndege izuiwe? 

Sasa tusemeje juu ya hayo ni dalili kwamba wapo maadui ndani na nje ya Tanzania.

Hili la kuzuiwa ndege ya ATCL ni kiashiria kwamba tukae chonjo mambo siyo shwari hasa baada ya kuona kwamba Rais John Magufuli amedhamiria kuiinua Tanzania kiuchumi.

Lakini pia kuongeza fursa nyingi za ajira pamoja na kuboresha hali ya maisha kwa kuutokomeza umaskini. 

Zaidi amekuwa akisema taifa letu siyo maskini ni tajiri, naamini wapo ambao hawapendi kusikia kauli kama hiyo.

Sasa ni mwaka wa nne kwa Serikali ya Awamu ya Tano lakini miradi inayotekelezwa inatia moyo na matumaini makubwa kwamba kwa kasi hii nchi itasonga mbele kiuchumi na kijamii. 

Kuizuia ndege isifanye kilichokusudiwa siyo dalili njema kwa maendeleo ya uchumi wetu. Ni vyema kwamba juhudi za makusudi zilifanyika na hatimaye ndege yetu ikaachiwa.

Kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kufanyika, Watanzania wengi tulipenda kuwepo mabadiliko ya uongozi maana hali ilikuwa tete kiasi cha kusema yatosha (enough is enough).

Hata marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika moja ya hotuba zake alisema:

“Watanzania wanahitaji mabadiliko na iwapo hawatayapata ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM)-watayatafuta nje ya CCM.”

Vilevile aliamini kuwa mabadiliko ya kweli yatapatikana ndani ya CCM.  Hivi ndivyo ilivyokuwa mwaka 2015 baada ya Dk. Magufuli kupendekezwa kuwa mgombea wa Urais kwa tiketi ya CCM.

Nithubutu kusema kuwa mwaka 2015 Wapinzani wa CCM walikuwa na fursa nzuri kuongoza Tanzania, shida ilianza pale waliposema wanaongeza nguvu kwa kubadilisha “gea-gear” angani.

Kumbe wenzao wa CCM wakabadilisha gea ardhini hivyo wakawa na mwendo kasi zaidi kwa kutumia “katapila” badala ya gari au ndege.

Kwa kufanya hivyo ukawa ni mwanzo kwa fikra za Baba wa Taifa, kwamba mabadiliko ya kweli yatapatikana ndani ya CCM, kuwa sahihi.

Kwa muda mfupi sana tumeshuhudia mengi yakifanyika kuiletea maendeleo endelevu nchi yetu.  Rais Magufuli anasisitiza sana umuhimu wa uchumi wa viwanda na taifa kufikia kipato cha kati ifikapo 2025.

Ndiyo maana amejikita kujenga miundombinu muhimu ya barabara; reli mwendokasi (SGR); kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere ili kupata umeme wa uhakika kupitia maji ya Mto Rufiji (Stigler’s gorge); kuimarisha umwagiliaji; kuongeza nguvu katika huduma za afya na elimu kwa mantiki ya kuwapo nguvukazi ya kutosha ili kuzalisha malighafi kwa matumizi ya viwanda lakini pia kupata wataalamu waliobobea wenye ujuzi stahiki.

Tulijitawala kukiwepo fikra za “ubeberu” yawezekana baada ya kuona juhudi hizo zitaifanya Tanzania isonge mbele hasa kwa kutumia zaidi rasilimali zilizopo; fikra kama hizo zikaibuka tena.

Hawakosi wenye mtazamo wa “tukose wote” hivyo tuwe macho huenda yakaibuka mengine zaidi.

Wapo ambao hawapendi tuwe kitu kimoja au waone kuna kasi kubwa ya kujiletea maendeleo endelevu.

Kutakuwapo na mabeberu na maadui ndani na nje ya nchi yetu. Watatamani mengine mabaya yotokee tukwame kiuchumi lakini Mungu atafanya kweli maana anajua fikra zetu na ukweli ulivyo ila mapenzi yake yatimizwe.

Naamini hatatuacha tuhangaike bali atatufanyia njia pasipo na njia na wabaya wetu wataaibika wakati Tanzania ikisonga mbele ipasavyo.

Na kwa kuwa kabla ya Uchaguzi Mkuu 2015 kulifanyika maombi ya nguvu tukimlilia Mwenyezi Mungu atuinulie Kiongozi Mkuu wa nchi mwenye dhamira ya kweli kuondoa dhuluma, rushwa, ufisadi/wizi wa mali za umma, dawa za kulevya, uzembe na hatimaye kurejesha nidhamu na heshima kwa taifa letu tusikate tamaa yatakwisha. 

Nathubutu kusema kuwa maombi yetu Mungu aliyasikia akatuinulia Rais ambaye 2015 hakuwa mgombea mtarajiwa na sasa juhudi zake tunaziona. 

Anakazana usiku na mchana ili Tanzania ifanikiwe kiuchumi na kijamii na kwa manufaa ya wengi siyo tu kwa watu wachache (elite).

Mimi napongeza sana juhudi zake na Wasaidizi wake katika Serikali ya Awamu ya Tano.

Jipeni moyo songa mbele wanaobeza na kuitakia mabaya Tanzania tumwachie Mwenyezi Mungu atashughulika nao.

Muhimu tuendelee kumwomba Mungu ambaye sikio lake siyo zito asiweze kutusikia.

Kwanza, tumshukuru kwa kutuinulia Rais Magufuli; pili, tuombe aendelee kutujalia amani na utulivu ndani ya mioyo yetu na kwa taifa letu.

Tatu, amjalie Rais wetu hekima na busara ili aiongoze Tanzania kwa faida yetu na Afrika kwa ujumla.

Kama ambavyo amekuwa akisisitiza uchumi wa viwanda na kujali maslahi ya wanyonge ambao wengi wameghubikwa na umaskini; muhimu Tanzania itumie rasilimali zilizopo: ardhi, madini, watu na maliasili zote kwa faida yetu wote.

 

Mungu ibariki Tanzania na Watu wake.

Habari Kubwa