Kuelekea uchaguzi serikali za mitaa

11Sep 2019
Reubeni Lumbagala
Nipashe
Kuelekea uchaguzi serikali za mitaa
  • Vijana na wanawake msibaki nyuma kuwania uongozi

KIPENGA cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kimepulizwa tayari na uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika Novemba 24 mwaka huu.

Wananchi wakipiga kura kuchagua viongozi wa serikali za mitaa mwaka 2014.

Kwenye uchaguzi huo, Watanzania wenye sifa ya kupiga kura watawachagua viongozi wa vijiji, vitongoji na mitaa watakaowaongoza kwa muda wa miaka mitano ijayo hadi mwaka 2024.

Akitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) Selemani Jafo, alizitaja nafasi zitakazogombewa.

Nafasi hizo ni pamoja na Mwenyekiti wa Kitongoji katika Mamlaka za Miji Midogo, Mwenyekiti wa Mtaa na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake) na Wajumbe wa Kamati ya Mtaa (Kundi la Wanawake) katika Mamlaka za Miji.

Nafasi zingine ni; Mwenyekiti wa Kijiji, Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Mchanganyiko la Wanaume na Wanawake), Wajumbe wa Halmashauri ya Kijiji (Kundi la Wanawake) na Wenyeviti wa Vitongoji katika Mamlaka za Wilaya.

Vijana na wanawake ni makundi muhimu katika jamii ambayo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kuwania nafasi mbalimbali za uongozi wa serikali za mitaa, ili kupata nafasi ya kushiriki moja kwa moja kuzitafutia ufumbuzi kero za wananchi katika maeneo wanayoishi.

Vijana wa kike na wa kiume ni vyema wakawa mstari wa mbele kuwania nafasi za uongozi, badala ya kubaki nyuma na kuwa wapigadebe wa wagombea wengine.

Vijana ni kundi linalokabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinapaswa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.

Kutokana na hali hiyo, vijana wanatakiwa kuingia katika ulingo wa kisiasa kuwania nafasi hizo.

Pamoja na kwamba wana ndoto za kushika nafasi kubwa za uongozi kama vile udiwani, ubunge na hata urais, lakini ni vyema vijana wakaanza kuzichangamkia fursa za uongozi katika ngazi ya serikali za mitaa.

Hiyo itawawezesha kujijenga, kupata uzoefu na hatimaye kuja kushika nafasi zingine kubwa.

Vijana wakishika nafasi za uongozi katika vijiji, vitongoji na mitaa yao, watakuwa chachu ya kuzitafutia ufumbuzi kero za vijana na jamii yote kwa ujumla.

Kutokana na mahesabu yasiyowiana kati ya wanaume na wanawake kwenye ulingo wa siasa, wanawake wana kila sababu ya kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi.

Aidha, kuna nafasi nyingi maalum kwa wanawake za Wajumbe wa Kamati ya Mji na Halmashauri ya Kijiji.

Hivyo basi, kujitokeza kwa wingi kwa wanawake kutachochea kuongezeka kwa idadi ya wanawake katika siasa na pia wanawake watapata jukwaa (platform) la kusemea changamoto zao na za jamii na hivyo kupata ufumbuzi wake kwa ustawi na maendeleo ya maeneo yao.

CHANGAMOTO ZINAZOWAKABILI VIJANA NA WANAWAKE

Ziko za aina mbalimbali, lakini kubwa kwa ujumla ni pamoja na changamoto ya ajira. Vijana na wanawake wanakabiliwa na tatizo la ajira.

Viongozi wanayo nafasi ya kushirikiana na wananchi wao katika kutafuta ufumbuzi wa changamoto hizo.

Endapo vijana na wanawake watakuwa viongozi katika serikali za mitaa, watakuwa mstari wa mbele kupigania mikopo inayotolewa na Halmashauri zao ili kuwakopesha vijana na wanawake.

Hilo likifanyika, litatengeneza fursa za kujiajiri kwa kufanya shughuli za ujasiriamali na biashara, hatua ambayo itawasaidia vijana na wanawake kukuza vipato vyao na kushiriki moja kwa moja katika ujenzi wa uchumi wa nchi yao na maendeleo kwa ujumla wake.

Ipo vilevile changamoto ya huduma bora za kijamii. Mathalani, vijana wanahitaji elimu ili kuweza kujenga mustakabali wa maisha yao. Kama watapata fursa ya kuwa viongozi, watakuwa kichocheo kikubwa cha kupigania ujenzi wa shule za msingi na sekondari ili watoto na vijana wengi wapate elimu bora.

MAJI

Ipo changamoto ya maji ambapo wanawake wamekuwa waathirika wakubwa kwani hutembea umbali mrefu kutafuta maji, hali inayohatarisha maisha yao na hata ndoa zao.

Ni dhahiri viongozi wanawake katika serikali za mitaa watakuwa mstari wa mbele kupigania usambazaji wa maji kwa wananchi.

Vilevile, wanawake watapigania uboreshaji wa huduma za afya kwa kushiriki ujenzi wa zahanati, na uwepo wa dawa katika zahanati hizo ili wao na jamii yote kwa ujumla wapate huduma bora za afya.

Aidha, kuna changamoto ya ukatili wa kijinsia kwa vijana na wanawake katika jamii. Ukatili huu utapungua kama makundi yanayofanyiwa ukatili, ikiwa ni pamoja na vijana na wanawake, watakuwa viongozi katika serikali za mitaa.

Vilevile watakuwa watetezi wa watoto ambao pia ni waathirika wa ukatili wa kijinsia katika jamii.

Muda wa vijana na wanawake kuwa watazamaji katika nyadhifa za serikali za mitaa umepitwa na wakati . Wanapaswa kuwa mstari wa mbele kwenye uchaguzi huu, ili nao wawe sehemu ya ujenzi na maendeleo ya nchi yetu.

Habari Kubwa