Wawili wapoteza maisha kwa vurugu nchini Afrika Kusini

11Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Wawili wapoteza maisha kwa vurugu nchini Afrika Kusini

WATU wawili wamepoteza maisha kutokana na vurugu mpya zilizofanywa na magenge ya watu nchini Afrika Kusini.

Raia wa Afrika Kusini, wakiwa na magongo tayari kuwashambulia Waafrika wenzao wanaowatuhumu kuchukua fursa zao za ajira nchini mwao.

Vurugu hizo zilianza baada ya hotuba iliyotolewa mjini Johannesburg na mwanasiasa mkongwe Mangosuthu Buthelezi, dhidi ya vitendo vya chuki kwa wageni.

Buthelezi alizomewa na kundi la watu Jumapili, ambapo vikosi vya usalama viliingilia kati.

Watu 10 wakiwamo wageni wawili, waliuawa mjini humo juma lililopita, baada ya makundi ya watu kuvamia biashara zinazomilikiwa na raia wa kigeni.

Vurumai hizo zimesababisha mvutano wa kidiplomasia na nchi nyingine za kiafrika, hasa Nigeria.

Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amekemea vitendo vya vurumai za siku ya Jumapili, akisema mamlaka hazitaruhusu.

“Vurugu hizo na vitendo vya uvunjaji sheria zinahatarisha usalama wa mamilioni ya raia wa Afrika Kusini na raia wa kigeni nchini mwetu ambao wana haki kwa mujibu wa sheria kuishi na kufanya biashara kwa amani.”

Siku ya Jumapili watu kadhaa wakiwa wamebeba marungu waliandamana mjini Johannesburg wakiimba:

“Wageni ni lazima warudi walikotoka,” kilieleza chombo cha habari cha Soweten.

Kundi hilo lilielekea kwenye bustani ya Jules jijini Johannesburg mahali ambapo Buthelezi, Kiongozi wa zamani wa upinzani wa chama cha Inkatha Freedom na waziri wa serikali ya umoja baada ya ubaguzi wa rangi alikuwa akitarajiwa kutoa hotuba kuhusu mashambulizi ya hivi karibuni.

Alisema alifika kama msuluhishi na kwamba amekuwa akijisikia vibaya kutokana na machafuko nchini mwake ambayo yameharibu sifa ya Afrika Kusini barani Afrika.

Hata hivyo, alizomewa wakati wote na video iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter ilionyesha makundi ya watu wakitoka nje ya mkutano wake.

Kisha watu walianza kushambulia magari na majengo, na kuchoma moto. Mkuu wa idara ya polisi jijini Johannesburg, David Tembe, alikieleza chombo cha habari cha Eyewitness.

“Nafikiri ni uhalifu kabisa kwa sababu baadhi ya maduka yaliyochomwa si mali ya raia wa kigeni, yanamilikiwa na raia wa Afrika Kusini,” alinukuliwa.

Juma lililopita, polisi walisema kuwa waliwakamata watu zaidi ya 240 na fujo hizo zilipungua.

Mamlaka ziliwakamata watu 16 baada ya fujo za siku ya Jumapili kwa mujibu wa  taarifa ya Rais wa nchi hiyo.

Machafuko yalianza juma moja lililopita baada ya madereva wa malori raia wa nchi hiyo kuanzisha mgomo wakipinga ajira zinazotolewa kwa raia wa kigeni.

Nchi hiyo imekuwa ikiwavutia wahamiaji kutoka sehemu mbalimbali za Afrika kwa kuwa ni moja kati ya nchi zilizo na maendeleo makubwa ya kiuchumi.

Hata hivyo, kuna changamoto kubwa ya ukosefu wa ajira nchini humo na baadhi ya watu wanahisi raia wa kigeni wanachukua ajira zao. BBC

Habari Kubwa