Kagame, Museveni kuyaheshimu makubaliano ya nchini Angola?

11Sep 2019
Mashaka Mgeta
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kagame, Museveni kuyaheshimu makubaliano ya nchini Angola?

MARAIS Paul Kagame wa Rwanda na Yoweri Museveni wa Uganda, walifikia hatua ya kutoa matamshi yenye vitisho, na hatua kali ikiwamo kufunga mipaka ya nchi mbili hizo kutokana na mgogoro uliokuwapo kati ya wawili hao.

Nchi hizo zimekuwa na mgogoro wa kidiplomasia kwa nyakati tofauti, lakini zaidi baada ya kuibuliwa madai kwamba Uganda ilikuwa inawakamata na kuwaweka ndani Wanyarwanda waliokuwa wanaingia nchini humo.

Hali hiyo ilikuwa ni sehemu ya historia ya migogoro ya mara kwa mara kwa nchi hizo, kama ilivyowahi kutokea katika miaka ya 1990 ziliponusurika kuingia kwenye vita kutokana na mapigano ya majeshi yao huko DRC.

Majeshi hayo yalikuwa yanashiriki katika mapigano ya kumuondoa aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, wakati huo ikijulikana kama Zaire, Mobutu Sese Seko.

Mgogoro mwingine ni wa hivi karibuni ambapo Uganda iliishutumu Serikali ya Rais Kagame kwa kuzuia malori ya mizigo na magari mengine kutoka nchini mwake kuingia Rwanda.

“Utawala wa Rwanda uliyazuia maroli na magari mengine kutoka Uganda kuingia nchini humo,” Msemaji wa Serikali ya Rais Museveni, Ofwono Opondo, akawaambia waandishi wa habari.

Kwa mujibu wa Opondo, maroli ya mizigo yanayofikia 129 kutoka Uganda yalikuwa ‘yamekwama’ kwenye mpaka wa Gatuna kwa wakati huo.

Hata hivyo, serikali ya Rais Kagame kupitia kwa Waziri wa Mambo ya Nje ya Nchi, Richard Sezibera, ilikanusha shutuma hizo na kufafanua kwamba magari hayo yalielekezwa kupitia mpaka wa Kagitumba uliopo Kaskazini mwa nchi hiyo ili kupisha ujenzi wa barabara yenye shughuli nyingi katika mpaka wa Gatuna.

Zipo tuhuma nyingi zilizotolewa kwa kila upande dhidi ya mwingine, kiasi cha kusababisha kukua kwa tofauti kati ya nchi hizo zilizo wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Agosti 21, mwaka huu, marais hao waliowahi kukumbwa na migogoro ya kidiplomasia na majirani zao kwa nyakati tofauti, wakaingia katika historia mpya, wakijaribu kufunga mipaka ya uhasama wao kupitia makubaliano waliyowekeana saini jijini Luanda, Angola.

Walifikia makubaliano hayo katika mkutano wa pili huko Luanda mbele ya marais Joao Lourenco wa Angola, Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Denis Sassou Nguesso wa Congo.

Mtaaluma wa sayansi ya siasa, John Mkorya, anasema makubaliano ya viongozi hao kama yatatekelezwa, yatasaidia kushusha joto la mzozo wa kidiplomasia lililokuwapo kati yao na kuathiri wananchi wa mataifa hayo.

Viongozi hao wawili wamekubaliana kutilia mkazo kutatua mzozo wowote baina ya mataifa yao kwa njia Amani, kwa mujibu wa Shirika la Habari la Angola (Angop).

ASILI YA MGOGORO

Mnamo Machi mwaka huu katika hotuba kwenye mkutano wa kitaifa, Kagame akaelezea kuwa chimbuko la mgogoro baina ya nchi yake na nchi ya Uganda ni la tangu miaka 20 iliyopita nchi ya Uganda ikitaka kuangusha utawala wake.

Kagame akasema mgogoro huo ulishika kasi hivi karibuni kufuatia wananchi

wa Rwanda wanaoingia nchini Uganda au kufanya kazi nchini humo kukamatwa na kuzuiliwa sehemu ambazo hazijulikani, kisha kufanyiwa vitendo vya mateso kwa madai kuwa ni mashushushu.

Lakini Uganda nayo mara kadhaa, imeishutumu Rwanda kuwatuma majasusi na kufanyia vitendo vya ujasusi kwenye ardhi yake. Kwa upande wake, utawala wa Rwanda umekuwa ukikanusha kama ilivyo kwa utawala wa Uganda.

Wakati swali likibaki kuwa, ikiwa Kagame na Museveni watatekeleza makubaliano ya Luanda kwa vitendo, wawili hao wanaonyesha hatua za awali za kushukuru hatua iliyofikiwa.

Museveni anamshukuru Rais Lourenco wa Angola, kwa kufuatilia utekelezaji wa mchakato uliofanikisha nchi mbili hizo kusaini makubaliano ya kuboresha uhusiano wa kisiasa na kidiploasia.

“Ninawashukuru marais Lourenco na Tshisekedi kwa kuja wao, kwamba tutashirikisha taarifa tulizonazo na kuhakikisha tunatoa tamko la pamoja na Rwanda,” akasema Museveni.

Hata hivyo, Museveni akasema alishawasiliana na Kagame kutafuta suluhu ya mzozo uliokuwapo kati yao wakati Lourenco na Tshisekedi walipomwalika.

“Nilishawasiliana na Kagame kupitia njia zetu za mawasiliano, lakini suala hili limekuja kama uimarishaji wa kufikia lengo letu. Tunathibitisha namna tulivyokuwa wakuu wa Umoja wa Afrika,” akasema Museveni.

Viongozi wa Angola and DR Congo ni wawezeshaji wa mpango wa kufikia suluhu kwa Kagame na Museveni kusaini makubaliano ya kuondoa mvutano uliokuwapo kati yao.

MAKUBALIANO

Makubaliano waliyoyafikia ni pamoja na kila upande, kuheshimu mamlaka ya taifa jingine na zile za nchi majirani zao.

Walikubaliana kutoshiriki vitendo vinavyochangia kudhorotesha utulivu ama kuchochea uhasama kwa taifa jingine ama mataifa jirani.

Pia walikubaliana kuondoa viashiria vyote vinavyoweza kuibua hisia hizo ikiwa ni pamoja na ufadhili, mafunzo ama kuingiza vikundi vyenye kuathiri utulivu kwa nchi husika.

Viongozi hao watatakiwa kuheshimu na kulinda haki na uhuru wa watu wa taifa jingine watakaoingia ama kupitia kwenye mipaka ya nchi zao kwa mujibu wa sheria za nchi husika.

Makubaliano hayo yakagusia pia suala la nchi hizo kurejesha shughuli za biashara na muingiliano wa watu mipakani, ili raia wapite na mizigo kusafirishwa.

Ili kutekeleza suluhu hiyo, Kagame na Museveni wakakubaliana kuanzisha kamati maalum ya muda itakayoongozwa na mawaziri wa mambo ya nje wa mataifa hayo na kuwajumuisha mawaziri wa mambo ya ndani, watawala na wakuu wa intelijensia watakaofanya ufuatiliaji.

Viongozi hao waliwahi kuwa marafiki wa karibu katika harakati tofauti za kutafuta fursa za kuyatawala mataifa yao, lakini mara kadhaa wamejikuta katika mizozo na migogoro inayohatarisha utulivu na uhusiano wa kiuchumi, hasa kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Museveni anasema makubaliano hayo yatarejesha uhusiano mwema wa kisiasa na kiuchumi kati ya Uganda na Rwanda.

“Tumekubaliana mambo mbalimbali yatakayotekelezwa na nchi zetu mbili hizi, kwa sehemu kubwa ikimaanisha kuboresha usalama, biashara na uhusiano wa kisiasa. Uganda tupo tayari kabisa kutekeleza makubaliano haya,” akasema.

Wakati Museveni akisema hayo, Kagame anabainisha, "Itachukua muda kiasi kwa nchi zetu hizi kuelewana kila mmoja, lakini ninafikiri tumetoka mbali.”

Mpatanishi wa waliokuwa ‘mahasimu wa kisiasa’, Rais wa Angola, Lourenco akapongeza hatua hiyo yenye kutoa tafsiri kwamba Kagame na Museveni wapo tayari kusuluhisha mgogoro uliokuwepo.

Pamoja na utayari huo wa maneno, bado inaendelea kusubiriwa kuona ikiwa makubaliano ya Angola yataleta mageuzi ya uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo.

Habari Kubwa