Kagere aanza na tuzo TFF, Ajibu atoa neno

11Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kagere aanza na tuzo TFF, Ajibu atoa neno
  • ***Agosti yawa tamu kwa Mnyarwanda baada ya kufungua msimu kwa mafanikio, huku makocha Simba wakianza kumsuka...

WAKATI mshambuliaji wa Simba, Meddie Kagere, akianza na tuzo Ligi Kuu Bara msimu wa 2019/20, straika aliyerejea nyumbani hapo mtaa wa Msimbazi jijini Dar es Salaam, Ibrahim Ajibu, amewataka mashabiki wa timu hiyo kutulia huku akiahidi kufanya vizuri.

Jana Kamati ya Tuzo ya Ligi Kuu Bara, ilimtangaza Kagere kuwa Mchezaji Bora wa mwezi Agosti hiyo ikitokana na kiwango kikubwa alichokionyesha kwenye mechi yao ya ufunguzi dhidi ya JKT Tanzania.

Kagere ambaye katika mechi hiyo iliyopigwa Uwanja wa Uhuru alihusika katika mabao yote matatu wakati Simba ikishinda 3-1, amepewa tuzo hiyo akiwashinda wachezaji wenzake Lukas Kikoti wa Namungo FC na Seif Karihe wa Lipuli, aliofika nao fainali.

Katika mechi hiyo dhidi ya JKT Tanzania, Kagere alifunga mabao mawili na kutoa pasi ya mwisho kwa bao lililozamishwa nyavuni na Miraji Athumani.

Kwa upande wa Ajibu ambaye katika mechi hiyo aliingia dakika za mwisho akitokea benchi, baada ya kuwa katika wiki ngumu ya mazoezi na timu hiyo, jana aliwataka Wanasimba kuwaamini na kuwa pamoja nao huku akiahidi kufanya vizuri.

“Nawaomba Wanasimba watuamini, sisi tupo pamoja na wao wawe pamoja na sisi. Nawaahidi nitafanya vizuri. Nawapenda sana- @ibrahimajibu23," alitupia katika mtandao wa klabu hiyo.

Kwa muda wa siku tatu mfululizo Kocha Mkuu wa Simba, Mbelgiji Patrick Aussems, ameonekana kuna kitua anataka kukitengeneza kutoka kwa Ajibu kutokana na namna anavyopewa mazoezi.

Katika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea kwenye viwanja vya Gymkhana jijini Dar es Salaam, kocha wa viungo wa klabu hiyo, Adel Zrane amekuwa akibeba jukumu la kudili na mshambuliaji huyo aliyerejea Simba msimu huu akitokea kwa mahasimu wao, Yanga.

Ajibu, ambaye ana kipaji cha hali ya juu ya kutandaza soka, amekuwa akielezwa ni mvivu wa kufanya mazoezi na inadaiwa kocha haridhishwi na namna anavyojifua katika kuhakikisha analinda kipaji chake.

Kwa mujibu wa chanzo chetu cha uhakika kilichopo karibu na makocha hao, kilieleza si kwamba Ajibu hafanyi mazoezi bali kocha haridhishwi na kiwango chake cha kujifua na anataka kumtengeneza kuwa bora zaidi.

"Aussems amemfuatilia na kugundua hilo, hivyo ametoa jukumu kwa Zrane kudili naye katika mazoezi na uzuri Ajibu ni mwelewa mambo yatakuwa mazuri tu," kilieleza chanzo chetu.

Simba itashuka dimba la Uhuru keshokutwa, Ijumaa kuikaribisha Mtibwa Sugar iliyotoka kupoteza mechi yake ya ufunguzi ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mabao 3-1 dhidi ya Lipuli FC.

Habari Kubwa