Zahera: Dawa Zesco Taifa tu

11Sep 2019
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Zahera: Dawa Zesco Taifa tu

ZIKIWA zimebaki siku tatu kabla ya mchezo wao wa awali wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco ya Zambia, Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera, ameweka wazi kuwa mechi hiyo itakuwa ngumu, lakini ni lazima kazi waimalizie Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera.

Akizungumza kabla ya mchezo wa jana wa kirafiki dhidi ya Toto African ya Mwanza, Zahera alisema wamejipanga 'kumalizia kazi' Uwanja wa Taifa kwa kuwa anaamini mchezo wa marudiano nchini Zambia utakuwa mgumu zaidi.

"Unajua lazima tupambane sana kwenye mchezo wa nyumbani, ushindi mzuri utatupa nafuu kuelekea kwenye mechi ya marudiano na utatupa nafasi ya kujipanga zaidi na kujua nini tunatakiwa kwenda kufanya ugenini," alisema Zahera.

Alisema hana hofu na timu yake na yapo mambo aliyoyafanyia kazi ambayo anaamini yatawasaidia kwenye mchezo huo utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa.

"Kila mchezo una mipango yake, tumemaliza mchezo wa kwanza dhidi ya Township Rollers, hatutacheza kwa namna tulivyocheza... mchezo huu una mipango yake na tunaendelea kuifanyia kazi hatua za mwisho," aliongeza kusema Zahera.

Zahera, amesema kikubwa anataka kuona wachezaji wake wote wanakuwa kwenye afya nzuri mpaka siku ya mchezo ili kumpa wigo mpana kwa kuona wachezaji wa kuwatumia kutokana na mbinu atakazotumia kwenye mechi hiyo.

Katika hatua nyingine, winga wa timu hiyo, Issa Bigirimana anaendelea kupata nafuu kutokana na maumivu ya paja yanayomkabili.

Nyota huyo wa Yanga hakuweza kuungana na wenzake kwenye kambi mkoani Mwanza kutokana na maumivu hayo.

Baada ya mchezo huo wa Jumapili, Yanga itarudiana na wapinzani wao hao wiki mbili baadaye nchini Zambia.

Habari Kubwa