Waziri Mwakyembe ataka Watanzania kujifunza ukalimani

11Sep 2019
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Waziri Mwakyembe ataka Watanzania kujifunza ukalimani

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, amewata Watanzania kujifunza taaluma ya ukalimani ili waweze kujiwekea wigo mpana wa kupata ajira ndani na nje ya nchi.

WAZIRI wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe.

Alisema hapa nchini kuna idadi ndogo ya wakalimani kulinganisha na mahitaji yaliyopo, na hivyo kusababisha changamoto kwa baadhi ya taasisi au ofisi zinazowahitaji.

Waziri Mwakyembe alitoa rai hiyo alipokuwa mgeni rasmi kwenye mahafali ya 15 ya wanafunzi wa darasa la saba wa shule ya Bethel Mission jijini Dar es Salaam na kueleza licha ya ukalimani kuwa na soko zuri la ajira duniani, bado kuna uhaba wa wataalamu wa fani hiyo nchini.

Alisema idadi ya wakalimani nchini haizidi 20 hali inayoashiria kuwapo kwa kiwango kidogo cha wataalamu hao kuliko uhalisia wa mahitaji.

"Ninawaasa wazazi kuendelea kuwalea watoto wao katika maadili mema kama ambavyo shule hii ya Bethel Mission imekuwa ikifanya ili kujenga taifa la watu waadilifu," alisema Waziri Mwakyembe.

Pia, Dk. Mwakyembe aliimwagia sifa shule hiyo kwa kuwa mstari wa mbele wa kuwalea na kuwajenga kimaadili watoto hasa katika kipindi hiki cha utawandawazi ambao maadii yameharibika.

Mkurugenzi wa shule hiyo, Emmanuel Mshana, alisema mbali na shule hiyo kujivunia kwa matokeo mazuri kwa wanafunzi katika mitihani ya kitaifa, pia wamekuwa wakiwajenga nidhamu bora ili kuwa na kizazi bora.

Alisema shule hiyo imekuwa na ushirikiano wa karibu na wazazi ili kuhakikisha wanaosoma katika shule hizo wanahitimu wakiwa na ufaulu mzuri ili kuwafanya waweze kupata nafasi za kuendelea na ngazi za juu katika masomo yao.

"Mikakati ya baadaye ya shule hii ni kujenga sekondari ili kuwawezesha kuwaendeleza kimasomo wanafunzi wanaoanza nao kuanzia ngazi ya shule za msingi na awali," alisema Mshana.

Habari Kubwa