Waziri atahadharisha kuhusu mabomu

11Sep 2019
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Waziri atahadharisha kuhusu mabomu

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, amewataka wananchi wa Kagera na mikoa mingine nchini kuendelea kuchukua tahadhari wanapoona vitu vyenye asili ya chuma ili wasikumbwe na milipuko ya mabomu.

WAZIRI wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi.

Dk. Mwinyi alisema hayo jana bungeni mjini hapa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Nungwi (CUF), Yussuf Haji Khamis, ambaye alisema kumekuwa na matukio ya watoto kuokota mabomu wakidhani ni vyuma chakavu na kisha kuwalipukia na kusababisha madhara makubwa ikiwamo vifo.

"Hivi karibuni watoto watano wamepoteza maisha na zaidi ya watoto 40 kujeruhiwa katika Shule ya Msingi Kihanga iliyoko mkoani Kagera. Je, serikali ina mpango gani wa kudhibiti na kukomesha tatizo hili?" alihoji.

Akijibu swali hilo, Waziri Mwinyi alisema maeneo mengi duniani yanakabiliwa na changamoto ya kutapakaa kwa silaha ndogo ndogo yakiwamo mabomu ya kutupwa kwa mkono.

"Pamoja na Tanzania kuwa nchi yenye amani, baadhi ya nchi zinazotuzunguka zimejikuta zikitumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe,"alisema.

Waziri huyo alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya wakimbizi kukimbia na silaha yakiwamo mabomu ya kutupwa kwa mkono na kuyateketeza baada ya kujiona wako salama au kuwauzia wahalifu jambo ambalo limechangia kuwapo kwa mabomu hayo katika badhi ya mikoa, Kagera ikiwamo.

"Baada ya vita vya Kagera, Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) lilitoa elimu kwa wananchi kutokuokota vitu vinavyong'ara, vifaa vya chuma na pindi wanapoona vitu hivyo watoe taarifa vituo vya polisi au kambi ya jeshi iliyo karibu," alisema.

Dk. Mwinyi alisema kwa maeneo yaliyotiliwa shaka, wananchi walipewa tahadhari ya kutolima,  kutopita au kulisha mifugo.

" JWTZ lilipeleka wahandisi wa medani kukagua maeneo hayo na kujiridhisha kama yako salama kwa wananchi kuendelea na shughuli zao za kawaida, hivyo inashauriwa wananchi katika mkoa huo na mingine kuendelea kuchukua tahadhari wanapoona vitu vyenye asili ya chuma," alisisitiza.