Faru tisa warejeshwa nchini  kutoka ‘Sauzi’

11Sep 2019
Godfrey Mushi
HAI
Nipashe
Faru tisa warejeshwa nchini  kutoka ‘Sauzi’

FARU tisa kati ya 10 wenye vinasaba vya faru wanaopatikana Tanzania, wamerejea nchini  wakitokea Afrika  Kusini.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Costantine Kanyasu, alisema wakati faru hao wakirejeshwa  jana katika maeneo yao ya asili, mmoja kati yao alikufa katika purukushani za kusafiri na hakufika.

Kanyasu alikuwa akizungumza jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), baada ya faru hao kuwasili kwa ndege ya mizigo aina ya Boeing 747-400 (F), mali ya Kampuni ya Magna ya Uingereza.

“Tunashuhudia kupokelewa kwa faru tisa, faru hawa walikuwa 10, lakini kwa taarifa tulizokuwa nazo mmoja katika purukushani za kusafiri hakufika. Tumetaarifiwa kwamba alikufa, lakini tisa tunakiri kuwapokea wako hai,” alisema na kuongeza:

“Hii ni mara ya kwanza kwa nchi yetu kupokea idadi kubwa sana ya faru kwa mara moja ambao ni  wenye vinasaba vya nchi yetu.”

Wakati wa halfa fupi ya mapokezi na makabidhiano ya faru hao kati ya serikali na Kampuni ya Grumeti Fund iliyotoa faru hao, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Prof. Adolf Mkenda, aliapa akisema:

"Tutawalinda faru hawa na tutalinda maliasili zetu kufa na kupona, na yeyote ana mawazo ya kujaribu kuja kufanya ujanja ujanja tutamdaka. Sasa hivi hakuna namna tutampata, tutawalinda usiku na mchana na kwa kila mbinu.”

Pia Prof. Mkenda alitangaza mpango mpya wa serikali wa kukabiliana na wanyamapori hatari na waharibifu ambao wamekuwa wakivamia maeneo mbalimbali  nchini.

"Nimemwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Wanyamapori kuanza rasmi operesheni maalum ya kupambana na wanyama hatari na waharibifu wanaovamia maeneo mbalimbali na kuleta hatari," alisema Katibu Mkuu huyo.

Makabidhiano ya wanyama hao yamefanyika katika karakana ya ndege uwanjani hapo, kati ya Naibu Waziri Kanyasu na Mkurugenzi wa Kampuni ya Grumeti Fund, Stephen Cunliffe.

Mapema akitoa taarifa kuhusu mpango wa kuwarejesha faru hao katika hifadhi za Taifa, Mkurugenzi wa Wanyamapori nchini, Dk. Maurus Msuha, alisema tukio hilo ni utekelezaji wa mpango wa kuhifadhi faru wa mwaka 2019/ 2023.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Hifadhi ya Wanyamapori (TAWA), Meja Jenerali mstaafu, Khamisi Semfuko, aliwasilisha salamu za Rais John Magufuli akisema, mkuu wa nchi anaishukuru sana Kampuni ya Grumet Fund kwa kuweza kurejesha hali ya hifadhi ziwe katika kiwango kikubwa cha faru.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro,  Anna Mghwira na  wa  Arusha, Mrisho Gambo, kila mmoja kwa nyakati tofauti walipongeza jitihada za serikali katika uhifadhi.

Habari Kubwa