Kauli za viongozi kuhusu kuua majambazi zashutumiwa vikali

11Sep 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kauli za viongozi kuhusu kuua majambazi zashutumiwa vikali

WAKATI kauli za viongozi mbalimbali za kuwataka wananchi kuchukua sheria mkononi kuua na kujeruhi, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimekosoa matamko hayo na kusema jambo hilo ni kinyume cha utawala wa sheria.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga.

Hivi karibuni, kumekuwa na kauli mbalimbali kutoka kwa baadhi ya watendaji wa serikali wakishinikiza wananchi kuvunja sheria za nchi na kuua wenzao.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga, alipoulizwa kuhusiana na kauli hizo jana, alisema chombo chenye mamlaka ya kutambua mtu ni kibaka, jambazi ni mahakama pekee.

"Ndiyo maana akikamatwa na polisi tunamwita mtuhumiwa. Hatumwiti jambazi au kibaka. Nchi yenye utawala wa sheria inatambua mahakama ndiyo yenye mamlaka ya kumtambua jambazi.

"Kauli hizi ni za kukemewa kwa sababu zikiachiwa zitasababisha watu kuchukua hatua za kisheria mikononi," alisema.

Jana, Kamanda wa Polisi wa mkoa wa kipolisi Kinondoni, Musa Taibu, jana aliwataka wananchi wanaomiliki silaha wanapokutana na majambazi, wawaue.

"Ndugu zangu wananchi pale inapotokea kwamba kuna jambazi na wewe una bunduki, tumia akili za kuona ni namna gani unaweza kukabiliana na jambazi huyo. Mtandike  risasi hakuna atakayekulaumu.

"Na bunduki yake ichukue tuikute, tukikuta ni mwili hakuna tatizo lolote. Huyo ni jambazi na alichokitaka kufanyiwa ndicho hicho alichostahili kupewa," alikaririwa kamanda huyo akisema.

Hivi Karibuni, Waziri Maliasili na Utalii, Dk. Khamis Kigwangallah, alisema angekutana na mmoja wa majangili waliokamatwa Septemba 3, angempiga risasi na kumwua.

Dk. Kigwangallah alitoa kauli hiyo baada ya vipande 339 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Sh. bilioni 4.4 kukamatwa maeneo ya Chamazi ambavyo idadi yake ni sawa na tembo 117.

Kauli zenye viashiria vya uvunjifu wa sheria ni pamoja na iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, ambaye aliagiza: “Anayeingia nyumbani kwako kwa nguvu, amechagua kifo, hivyo mhusika hana budi kumwua.”

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni, Sarah Msafiri, alisema anajua kuna watu wanaishi kwa kutegemea wizi huku wakiamini kuwa wakipelekwa mahakamani wanapewa dhamana.

"Sasa nawaambia siku zao zinahesabika, watapigwa na kupewa ulemavu kwa kuvunjwa miguu," alisema mkuu huyo wa wilaya.

Habari Kubwa