Lissu kukimbilia Mahakama ya Rufani

11Sep 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Lissu kukimbilia Mahakama ya Rufani

SIKU moja baada ya Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam kutupilia mbali maombi ya mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, mwenyewe amezungumza na kusema mapambano bado yanaendelea.

Mbunge wa zamani wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.

Lissu alisema mlango mmoja ukifungwa mingine inafunguliwa.

Akizungumza juzi nchini Ubelgiji na chombo kimoja cha habari baada ya hukumu hiyo, alisema kauli ya mwisho ya mgogoro wa kisheria ni Mahakama ya Rufani Tanzania ambako ndiko wanakoelekea.

Juzi, Mahakama Kuu ya Dar es Salaam ilitupilia mbali maombi ya Lissu ya kibali cha kutaka kufungua kesi kupinga uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai, kumvua ubunge wa jimbo hilo.

Mahakama iliyoketi chini ya Jaji Sirilius Matupa, ilisema kwamba maombi hayo yangesikilizwa hadi mwisho na Lissu kushinda, Jimbo la Singida Mashariki lingekuwa na wabunge wawili kinyume cha Katiba.

Vilevile alisema maombi ya Lissu yamechelewa kufunguliwa mahakamani hapo na hayatekelezeki kwa sababu mleta maombi alitakiwa kufungua kesi ya kupinga uchaguzi badala yake ameleta maombi ya kutaka kupinga maamuzi ya Spika.

Akizungumza na chombo hicho Lissu alisema kwa maoni yake jaji amekosea aliposema alipaswa kufungua kesi ya uchaguzi.

"Kufungua kesi ya uchaguzi maana yake ni kwamba nina ugomvi na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) au huyo aliyesemekana amechaguliwa au ameteuliwa kuwa mbunge," alisema.

Lissu alifafanua kuwa, kisheria hakuwa na ugomvi na Tume wala aliyechukua nafasi yake ya ubunge Singida Mashariki.

"Kisheria sina ugomvi nao kwa sababu Tume imeitisha uchaguzi kutokana na uamuzi wa Spika, huyu aliyechukua nafasi yangu aligombea kwa sababu Tume ilitangaza uchaguzi, Tume haina mamlaka ya kumkatalia Spika, akisema kiti kiko wazi.

"Kwa hiyo nisingeweza kufungua kesi ya uchaguzi kwa sababu sina ugomvi na Tume ya Uchaguzi wala huyo aliyechukua nafasi yangu. Ugomvi wangu ni yule aliyefanya uamuzi wa kunifuta ubunge, huo ndio ugomvi wangu kisheria.

Kuhusu hoja ya pili ya Jaji kuwa angeendelea na shauri jimbo lingekuwa na wabunge wawili kinyume cha Katiba, Lissu alisema, hoja hiyo haina maana wala mantiki yoyote.

"Mahakama Kuu ikitamka kwamba Spika ulikuwa batili maana yake Tume haikuitisha uchaguzi kihalali na maana yake ni kwamba aliyechukua nafasi yangu hakuichukua kihalali, hakuwezi kuwa na wabunge wawili kwenye nafasi moja, haiwezekani kisheria wala katika hali ya kawaida," alisema.

Alisema Jaji alitakiwa aseme alichofanya Spika kama ni halali au siyo halali, na angesema siyo halali mengine yote yangekuwa batili.

Kuhusu nini kitakachoendelea, Lissu alisema hapo siyo mwisho wa mapambano kwa sababu kwa utaratibu wa kikatiba mahakama yenye kauli ya mwisho kuhusiana na migogoro ya kisheria ni Mahakama ya Rufani Tanzania.

"Ndiko tunakoelekea kwa sababu hiyo, mapambano bado yanaendelea, mlango mmoja ukifungwa mingine inafunguliwa," alisema.

Kuhusu lini atarejea nchini baada ya kuahirisha ya awali, Lissu alisisitiza kuwa atafahamu baada ya Oktoba 8, mwaka huu, atakapokutana na madaktari wake kwa mara ya mwisho.

Habari Kubwa