Ma-RC, DC mikoa ya pamba, chukueni somo la Mtaka

11Sep 2019
Raphael Kibiriti
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ma-RC, DC mikoa ya pamba, chukueni somo la Mtaka

NIMEVUTIKA kuzungumzia habari iliyoandikwa na gazeti hili ukurasa wa 26 jana Septemba 10, iliyokuwa na kichwa cha habari kilichosomeka “Simiyu yauza pamba ya bil. 65/-“

Habari hiyo ilikuwa inarejea taarifa iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, baada ya kuwa amefanya ziara mkoani mwake ya kukagua hali ya maendeleo ya ununuzi wa pamba.

Kwa mujibu wa taarifa yake, mkoa huo ambao ni moja ya mikoa inayoongoza kwa kilimo cha zao hilo nchini, tayari umeshauza kilo 54,257,314.00 za pamba zenye thamani ya Sh. bilioni 65,108,775,600.00.

Aidha, taarifa inaendelea kubainisha kwamba pamba iliyokusanywa kwenye maghala ya Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS), ni kilo milioni 132 yenye thamani ya Sh. bilioni 159.3.

Na kati ya kilo hizo zilizokusanywa kwenye maghala ya AMCOS, kilo milioni 83 zenye thamani ya Sh. bilioni 100, tayari zimeshasafirishwa kwenda kwenye viwanda vya kusindika pamba.

Vilevile taarifa hiyo ikafafanua kwamba kati ya kilo hizo milioni 83 zilizosafirishwa, kilo milioni 54 zenye thamani ya Sh. bilioni 65, bado hazijalipiwa kwa maana kwamba, wakulima hawajalipwa fedha zao.

Muungwana anasema amevutiwa na taarifa hiyo ya Mtaka kwa sababu ni miongoni mwa wadau ambao wamepaza sauti kwa muda sasa, kuhusiana na kadhia zinazoambatana na ununuzi wa pamba msimu huu.

Kadhia ya kusuasua kwa ununuzi wa zao hilo tangu msimu wa ununuzi uzinduliwe mwezi Mei, ambayo iliambatana na kitu kama ‘kamgomo’ kutoka kwa wanunuzi dhidi ya bei elekezi ya Sh. 1200 iliyowekwa na serikali.

Ni msimamo imara wa serikali ndio kimsingi umesaidia wakulima wanunuliwe kwa bei hiyo, kwani kama isingeonyesha msimamo thabiti kulikuwa na uwezekano kwa kilo ya pamba, kununuliwa hata kwa Sh. 500 msimu huu.

Aidha, kadhia hii iliambatana pia na ahadi ya serikali ya kununua pamba yote ya wakulima kufikia mwishoni mwa mwezi Julai, ahadi ambayo ilishindikana kutokana na kampuni za ununuzi kutokwenda na kasi iliyokuwa inatakiwa na serikali.

Taarifa hiyo rasmi ya Mtaka walau imempa mwanga Muungwana juu ya hali ilivyo katika suala zima la ununuzi wa pamba hadi sasa.

Anasema imempa mwanga hususani katika maeneo matatu kimsingi. Kwanza ni kuwa bado takribani nusu ya wakulima ambao wameuza pamba yao hadi sasa hawajalipwa fedha zao.

Hilo linathibitishwa na taarifa hiyo kwamba kati ya kilo milioni 83 zenye thamani ya Sh. bilioni 100, kilo milioni 54 zenye thamani ya Sh. bilioni 65 hazijalipwa hadi sasa. 

La pili ambalo limempa mwanga Muungwana ni kwamba bado kuna pamba ambayo haijasafirishwa kutoka kwenye maghala ya AMCOS, kwenda viwandani.

Na la tatu ambalo Muungwana amelibaini kutoka kwenye taarifa ya Mtaka ni kwamba maelekezo ya serikali ya kuhakikisha wanunuzi wawe wameshainunua pamba yote kufikia sasa, hayajatekelezwa kikamilifu.

Ikumbukwe kwamba hapa tunazungumzia pamba ambayo tayari iko AMCOS, wakati kuna wakulima ambao bado hawapeleka pamba yao kuiuza kwenye vyama vya ushirika vya msingi, wakitaka wakiuza walipwe fedha zao palepale.

Kwa hali hiyo kuna ushauri ambao Muungwana anautoa katika kadhia hii ikizingatiwa kwamba huu ni mwezi Septemba.

Mwezi ambao kimsingi, wakulima wa zao hilo wanapaswa kuwa wanamalizia kuandaa mashamba yao, tayari kwa kilimo cha msimu ujao.

Muungwana anashauri wakuu wa mikoa katika maeneo yanayolima zao hilo kuweka hadharani taarifa ya ununuzi unavyoendelea hadi sasa.

Lakini kubwa anawasisitiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya kusimamia shughuli nzima ya ununuzi, usafirishwaji na kubwa zaidi wahakikishe wakulima wanalipwa fedha zao.

Muungwana anasema hili ni la muhimu kwa sababu mbali na mengine, wakulima wanazihitaji fedha hizi ili ziwasaidie msimu ujao wa kilimo.