Vigingi vya Nape hadi msamaha wa Rais

11Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Vigingi vya Nape hadi msamaha wa Rais

RAIS John Magufuli amesema amemsamehe Mbunge wa Jimbo la Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye na kueleza jinsi mbunge huyo alivyohangaika kumtafuta ili kuomba msamaha huo.

Rais John Magufuli akiagana na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye baada ya mazungumzo yao, Ikulu, jijini Dar es Salaam jana.

Kauli ya Rais Magufuli aliitoa jana baada ya mazungumzo mafupi na mbunge huyo, Ikulu jijini Dar es Salaam. Akielezea njia alizopitia mbunge huyo kuomba msamaha huo, Rais Magufuli alisema Nape alikwenda kwa Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula, bosi wa zamani wa Usalama wa Taifa, Apson Mwang'onda na Mke wa Baba wa Taifa, Maria Nyerere.

"Nimeshamsamehe kwa dhati, Nape amekuwa hata akiandika 'message' (ujumbe) nyingi tu, ameshaandika message kuomba msamaha, saa nyingine anaandika saa nane za usiku, unamuona kabisa huyu mtu anaomba msahama," alisema na kuongeza:

"Leo kaniomba aje anione na saa zingine wasaidizi wangu wamekuwa wakipata hiyo habari, alienda kwa Mzee Mangula, amefika mpaka kwa Apson na Mama Nyerere, amehangaika kweli."

"Ni katika hiyo hiyo, sisi tumeumbwa kusamehe na leo mmemuona asubuhi amekuja hapa, nikaona siwezi kumzuia kumuona, ngoja niache shughuli zangu nimuone kwanza, nilikuwa na shughuli nyingi za vikao," alieleza.

"Kusamehe kunaumiza, lakini nasema kwa dhati kabisa nimemsamehe. Ameeleza yaliyokuwa yanamsibu, ameeleza baadhi ya watu aliokuwa wanamuhubiri, wengine wapo kwenye chama, lakini nimesema yote tunasamehe, huyu bado ni kijana mdogo ana 'future' (maisha baadaye), nikiendelea kumshikilia kwenye moyo wangu ni dhambi kubwa kwa Mungu, tumefundishwa tusamehe saba mara sabini," alisisitiza.

Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), alimtaka Nape kwenda kufanyakazi zake vizuri ikiwamo kulea familia yake na kukitumikia Chama na wananchi wa jimbo lake.

Kwa upande wake Nape alimshukuru Rais Magufuli kwa kukubali kuonana naye na kumsamehe.

"Nilikuja kumuona kama baba yangu, lakini Mwenyekiti wa chama changu, rais wangu kwa sababu wote mnajua mambo yaliyopita yametokea mengi hapa katikati, nami kama  mtoto wa CCM kama mwanaye, nilisema vizuri niongee na baba yangu," alisema Nape.

Baada ya mazungumzo yao, Nape alimshukuru Rais Magufuli kwa kumpa fursa ya kumuona na kumsamehe ikiwamo kumpa ushauri na kwamba aliyompa ni fursa na nafasi kubwa ya kumsikiliza.

"Mheshimiwa Rais kama baba yangu, mzee wangu nakushukuru sana kwa fursa uliyonipa ya kunisikiliza, kunisamehe, kunishauri na kunielekeza ninafanyeje huko mbele ninakokwenda," alisema Nape.

Nape ambaye amewahi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, kwenye Serikali ya Awamu ya Tano, aliondolewa kwenye nafasi hiyo Machi 23, mwaka 2017.

Mbunge huyo anakuwa watatu kwenda kuomba msahama wa Rais na taarifa zake kutangazwa kwa umma.

Wengine waliokwenda kuomba msamaha ni Mbunge wa Bumbuli, January Makamba, ambaye aliwahi kuwa Waziri wa Mazingira na Muungano. Aliondolewa kwenye nafasi hiyo, Julai 21, mwaka huu.

Mwingine aliyetajwa kuomba msamaha ni Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.

Msamaha huo unafuatia kuvuja kwa mawasiliano ya sauti zinazodaiwa kuwa ni za kwao kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutoka kwa waraka ulioandikwa na waliowahi kuwa makatibu wakuu wa CCM, Yusuph Makamba na Abdulrahman Kinana, kwenda kwenye Baraza la Ushauri la Wazee wakimtuhumu mwanaharakati mmoja kuwachafua.

Mawasiliano kati ya Nape na Kinana, yanadaiwa kujadili maandalizi ya waraka huo ulioelekezwa kwa Baraza hilo ambalo Mwenyekiti wake ni Rais wa Awamu wa Pili, Ali Hassan Mwinyi.