Kundi la WhatsApp ladaiwa  kutumiwa mitihani darasa 7 

11Sep 2019
Na Waandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Kundi la WhatsApp ladaiwa  kutumiwa mitihani darasa 7 

WATAHINIWA 947,221 wanatarajia kufanya mitihani ya darasa la saba leo na kesho, kundi la mtanndao wa kijamii linalohusisha walimu na wadau wa elimu, limebainika wilayani wilayani Chemba mkoani Dodoma.

Kutokana na kubainika kwa kundi hilo, uongozi wa halmashauri huyo umekemea na kutaka kundi hilo livunjwe mara moja. Katika mitihani ya mwaka jana, lilijitokeza kundi kama hilo lililokuwa likitumiwa na walimu na waratibu kupeana majibu ya mitihani.

Barua ya Agosti 19, mwaka huu, iliyoandikwa na Josephat Ambikilile kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chemba, iliwataka waratibu wa kata 26 zilizoko wilayani humo kuvunja makundi yote ya WhatsApp yaliyojihusisha na mawasiliano kwa walimu.

Katika barua hiyo, waratibu wameelezwa kuvunja makundi hayo yaliyojihusisha kutoa au kupokea taarifa zozote zinazohusiana na utendaji wa taaluma na utaalam zinazomgusa mwalimu wa Chemba katika utendaji wake wa kila siku hadi hapo watakapojulishwa vinginevyo.

"Ofisi imebaini kuwapo kwa makundi ya WhatsApp katika halmashauri yetu yanayotoa na kupokea taarifa mbalimbali za kielimu na kijamii kama vile walimu wakuu wanaovuliwa madaraka na walimu wakuu wapya, walimu wakuu walioko madarakani, maofisa elimu kata na walimu wakuu ngazi ya kata na wilaya na mengineyo yanayofanana na hayo," ilisema.

Barua hiyo iliwaeleza waratibu hao kuwa hatua kali za kinidhamu na kisheria zitachukuliwa dhidi ya kiongozi wa kundi la WhatsApp na wanachama wa kundi husika.

Akitolea ufafanuzi wa barua hiyo jana mara baada ya kupigiwa simu na Nipashe, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Semistatus Mashimba, alikiri barua hiyo iliandikwa lakini si kwa lengo la kutolewa hadharani.

Alisema kwa sababu barua hiyo haikulengwa kutolewa hadharani, wanaendelea kumsaka aliyeivujisha kwenye mitandao ya kijamii ili achukuliwe hatua za kinidhamu.

NECTA YAONYA

Wakati hayo yakibainika, Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (Necta) limesisitiza kuwa vituo vilivyofanya udanganyifu mwaka jana katika mtihani huo vinaendelea na kifungo.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alitangaza hayo jana jijini Dar es Salaam huku akisema watahiniwa katika vituo hivyo watafanyia mitihani yao katika vituo vilivyotangazwa mwaka huo na baraza.

"Vituo vilivyofanya udanganyifu katika mitihani ya mwaka jana vinaendelea na vifungo mpaka pale baraza litakapojiridhisha vipo salama kuendesha mitihani katika maeneo yao. Vituo hivi vilipokuwa vikirejea kufanya mitihani vilipewa vituo vingine vya wao kufanyia mtihani ambavyo tulivitangaza mwaka jana.

"Baadhi ya vituo kwa mfano cha Hazina tulisema watafanyia Oysterbay, kituo cha Atlas walifanyia kituo cha Bongoyo, Ubungo Fort of Joining walifanyia kituo cha Mbezi," alisema.

Dk. Msonde alitoa wito kwa shule zote nchini zijiepushe na kufikiria, kupanga na kutekeleza njama za kuhujumu mtihani huo.

"Kamati zote za mikoa, halmashauri na jiji wamefundishwa vilivyo mwaka huu wataangalia kwa upana namna ya uzingativu wa kanuni za mitihani. Wamiliki wa shule binafsi wasiingilie shughuli za mitihani waache vituo vyao ambavyo kwa sasa ni vya baraza ili mitihani ifanyike vizuri,” alisema.

Kuhusu watahiniwa 947,221 waliosajiliwa mwaka huu kufanya mtihani huo wa darasa la saba, Dk. Msonde alisema wanatoka katika shule 17,051 Tanzania Bara. Alisema kati yao wavulana ni 451,235 sawa na asilimia 47.64 na wasichana ni 495,986 sawa na asilimia 52.36.

Alisema watahiniwa 902,262 watafanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 44,959 wataufanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia.

"Watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 2,678 kati yao 81 ni wasioona, 780 wenye uoni hafifu, 628 wenye ulemavu wa kusikia, 325 ni wenye ulemavu wa akili na 864 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwilini," alisema.

Dk. Msonde alisema katika mtihani huo, masomo matano yatatahiniwa ambayo ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi, Hisabati na Maarifa ya Jamii.

"Wasimamizi wahakikishe wanalinda haki ya watahiniwa wenye mahitaji maalum. Haki hizi ni pamoja na kupata mitihani yenye maandishi ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu.

"Watahiniwa wote wenye mahitaji maalum waongezewe muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine, kama mwongozo wa baraza ulivyoelekeza," alisema.

WAONYWA UDANGANYIFU

Wasimamizi wa mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi (darasa la saba) mkoani Shinyanga, wameonywa kufanya udanganyifu kwenye mitihani hiyo na kwamba  atakayebainika atachukuliwa hatua kali ikiwamo kufukuzwa kazi.

Wanafunzi wa darasa la saba hapa nchini wanafanya mtihani wao wa kuhitimu elimu ya msingi leo na kesho. Katika Mkoa wa Shinyanga, wanafunzi 30,764 wanafanya mtihani huo.

Akizungumza na Nipashe jana, Ofisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Kahundi, alisema maandalizi ya mtihani huo wa darasa la saba yako vizuri na kuwatahadharisha wasimamizi wasije wakafanya udanganyifu na kusababisha wanafunzi kufutiwa mitihani pamoja na wao kufukuzwa kazi.

Imeandikwa na  Romana Mallya na Agnes Shayo (Tudarco), DAR na Marco Maduhu, SHINYANGA.

Habari Kubwa