Askofu Ruwa’ichi afanyiwa upasuaji

11Sep 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Askofu Ruwa’ichi afanyiwa upasuaji

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi, anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI).

ASKOFU Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi.

Ofisa Uhusiano wa MOI, Patrick Mvungi, alisema katika taarifa yake jana kuwa Askofu huyo alipokewa juzi saa 5:00 usiku akitokea katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya KCMC, Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema baada ya kupokewa, wataalamu wa MOI walimfanyia uchunguzi na vipimo na kubaini alihitaji upasuaji wa dharura.

"Jopo la madaktari bingwa pamoja na wauguzi wa MOI walimfanyia upasuaji mkubwa kwa muda wa saa tatu kuanzia saa 7:00 usiku hadi saa 10:00 alfajiri. Upasuaji huo ulifanyika kwa mafanikio makubwa," alisema Mvungi katika taarifa hiyo.

Alisema baada ya upasuaji hali ya Askofu Mkuu Ruwa’ichi inaendelea vyema na bado yuko kwenye chumba cha uangalizi maalum (ICU).

"Taasisi ya MOI inawatoa hofu Watanzania wote hususani waumini wa Kanisa Katoliki kwamba hali ya Mhashamu Askofu Ruwa’ichi inaendelea vizuri na tumwombee ili apone mapema na kurejea kwenye majukumu yake ya utumishi," alisema Mvungi.

Hadi sasa ni siku 26 tangu Askofu Mkuu Ruwa’ichi ashike wadhifa huo baada ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kung'atuka madarakani Agosti 15, mwaka huu, baada ya Kiongozi Mkuu wa Kanisa hilo duniani, Papa Francisco, kuridhia ombi lake.

Habari Kubwa