Rais Shein aupongeza ushirikiano na China

12Sep 2019
Rahma Suleiman
ZANZIBAR
Nipashe
Rais Shein aupongeza ushirikiano na China

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein, ameipongeza China kwa kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha maendeleo ikiwamo kuipatia wataalamu kwa ajili ya kuwafunza Wazanzibari.

RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alisema hayo Ikulu mjini Zanzibar wakati alipokutana na kuzungumza na Katibu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) Dong Weihong, ambaye ni Makamu Mkuu wa Taasisi ya China National Research Institute of Food Fermentation Industries ya China.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa Jamhuri ya Watu wa China na Zanzibar zina historia ya muda mrefu katika kushirikiana.

Alisema China inaleta wataalamu na wakufunzi wake Zanzibar katika sekta mbalimbali zikiwamo afya, kilimo, viwanda na  elimu.

Aidha, Dk. Shein alieleza kuwa Tanzania Bara na Zanzibar zinafurahishwa na juhudi za nchi hiyo za kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa kufikia maendeleo.

Alisema kuwa juhudi hizo zina manufaa makubwa kwa sasa na baadaye kwani ni kivutio kimoja wapo cha kupanua wigo wa masuala ya kuvutia watalii.

“Ni jambo la kufurahisha sana kwani Jamhuri ya Watu wa China walianza kutusaidia kwa kutuletea wataalamu wa afya, kilimo, viwanda, elimu, lakini leo inatuletea waatalamu wa mapishi na ukarimu kwa kweli ni jambo la kupongezwa sana,” alisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa kufanyika mafunzo hayo Zanzibar kunatoa nafuu ya gharama za uendeshaji na utoaji nafasi kubwa zaidi kwa watendaji watakaopata fursa ya mafunzo hayo.

Pia, alieleza kuwa mafunzo hayo yataimarisha uhusiano na ushirikiano katika kuimarisha sekta ya elimu na utalii kwa kupitia Chuo cha Maendeleo ya Utalii Zanzibar kilichopo Maruhubi ambacho hivi sasa kimeunganishwa na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).

Balozi mdogo wa China, Xie Xiaowu, alisema kuwa Jamhuri ya Watu wa China inathamini uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na kuahidi kuendelea kutoa nafasi za masomo nchini humo sambamba na kuleta wakufunzi kuja kuwafundisha Wazanzibari.

Balozi Xie Xiaowu alisema kuwa urafiki wa Jamahuri ya Watu wa China na Zanzibar ni wa miaka 55 hadi hivi sasa, hivyo unaonyesha wazi kuwa una historia kubwa na kuna kila sababu ya kuendelezwa na kudumishwa kwa nguvu zote.

Kwa upande wake Katibu wa Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) na Makamu Mkuu wa Taasisi ya ‘China National Research Institute of Food Fermentation Industries’ kutoka China Dong Weinhong alimpongeza Dk. Shein kwa juhudi zake za kuhakikisha mafunzo hayo yanafanyika.

Kiongozi huyo alieleza kuwa juhudi hizo za Rais Dk. Shein ni lazima ziungwe mkono kwani zinaonyesha wazi kuwa ana hamu na nia ya kuwasaidia wananchi wake katika sekta zote za maendeleo na kuahidi kuwa taasisi hiyo itasimama bega kwa bega na yeye.

Aliongeza kuwa hatua hiyo inazidi kujenga uhusiano na ushirikiano mwema kati ya Jamhuri ya Watu wa China na Zanzibar.

Habari Kubwa