Wenye ulemavu wataka usajili magari

12Sep 2019
Paul Mabeja
DODOMA
Nipashe
Wenye ulemavu wataka usajili magari

MWENYEKITI wa Kamati ya Taifa ya Usalama Barabarani kwa Watu wenye Ulemavu, Jutoram Kabatele, amesema wamepeleka mapendekezo kwa serikali kuanzisha utaratibu wa vyombo vya moto vinavyoendeshwa na watu wenye ulemavu kuwa na namba tofauti za usajili.

MWENYEKITI wa Kamati ya Taifa ya Usalama Barabarani kwa Watu wenye Ulemavu, Jutoram Kabatele.

Kabatele aliyasema hayo jana wakati wa utoaji wa elimu kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kuhusu alama sita mpya maalumu za usalama barabarani za kuwalinda makundi ya watu wenye ulemavu.

Alisema katika alama hizo sita za usalama barabarani, moja ni kwa ajili ya utambuzi wa vyombo vya moto vinaendeshwa na watu wa kundi hilo.

Kabatale alisema pamoja na kubuni alama hizo ambazo zitawasaidia watu wenye ulemavu katika kuwalinda na ajali, iko haja vyombo vya moto vinavyoendeshwa na watu wenye ulemavu kuwa na namba tofauti na zile za kawaida.

"Tumeshapeleka mapendekezo yetu serikali na sasa tunazungumza na watu wa TRA kuwa ni lazima sisi tuwe na namba tofauti na watu wengine wa kawaida. Inaweza  kuwa hata WT AZT 801, ikimaanisha ‘Walemavu Tanzania’. Hili suala ni la kisheria si kama tunaomba hisani," alisema Kabatele.

Akizungumza kuhusu alama tano kwa ajili ya kuwalinda watu wenye ulemavu barabarani, alisema amezibuni ili kuwasaidia watu wa kundi hilo kuepukana na changamoto ambazo wamekuwa wakizipata maeneo mbalimbali nchini.

"Kama leo hii mnyama anazo alama zake barabarani kwa nini mimi mlemavu nikose. Alama hizi zitawasaidia makundi ya watu wenye ulemavu wa viungo, wenye ualbino, viziwi, walemavu wa akili pamoja na wenye ulemavu wa macho," alisema.

Pia alisema sheria na sera za walemavu zinaeleza wazi kuwa watu wenye ulemavu wanatakiwa kupata huduma za usafiri katika mazingira ya usalama.

"Mlemavu anatakiwa anaposafiri asipate usumbufu wowote kwa mujibu wa sheria yetu, lakini hivi sasa ukienda katika vituo vya mabasi unakutana na changamoto nyingine ikiwamo mabasi kuwa na ngazi ndefu, lakini wakati watu wanapokwenda kuchimba dawa mimi kama mlemavu siwezi kwenda nabaki ndani ya basi kama mlinzi," alisema.

Aidha, alisema mafunzo hayo ya alama sita mpya za usalama barabarani kwa watu wenye ulemavu yatatolewa katika mikoa ya Dar es Saalam, Dodoma na visiwani Zanzibar, kwa ufadhili wa shirika lisilo la kiserikali la The Foundation For Civil Society (FCS).

Habari Kubwa