Utamaduni sasa kuvutia watalii

12Sep 2019
Renatha Msungu
DODOMA
Nipashe
Utamaduni sasa kuvutia watalii

SERIKALI imewataka Watanzania kutumia rasilimali ya urithi wa utamaduni walio nao kama bidhaa katika soko la utalii nchini.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Tamasha la Urithi,  Profesa Martine Mhando.

Hayo yalisemwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Tamasha la Urithi,  Profesa Martine Mhando, wakati akizungumza kuhusiana na tamasha hilo ambalo litatanguliwa na lile la ‘Jamafest’ linalotarajia kufanyika mwezi mzima kutangaza vivutio vya utalii.

Prof. Mhando alisema utekelezaji wa tamasha la urithi utafungua ukurasa mpya katika kuongeza wigo wa mazao ya utali, hivyo ni vyema jamii ikatumia nafasi hiyo kwenda kuonyesha bidhaa za asili walizo nazo.

Alisema tamasha la urithi linapaswa kuwa na tija kwa jamii kutokana na kujumuisha wadau kutoka sehemu mbalimbali ambao wataona utalii uliopo ndani ya nchi katika mikoa ambayo tamasha litafanyika kwa lengo la kutangaza utalii uliopo ndani ya mkoa husika.

Mwenyekiti huyo alisema kwa kuzingatia wingi na ubora wa vivutio vya utalii, watalii wa kigeni wanaotembelea nchini wamefikia milioni 1.5 na kuna uwezekano wakaongezeka iwapo jitihada za kila mkoa zitafanyika kutangaza utalii katika eneo husika.

Alisema ni vyema jamii ikatumia fursa ya tamasha la urithi na lile la Jamafest kupanua wigo wa kutangaza bidhaa zilizopo jambo ambalo itasaidia kuongeza idadi ya watalii kutembelea nchini.

Prof. Mhando alisema sekta ya utalii ni kichocheo cha kukua kwa sekta zingine za uchumi hususani uchukuzi, viwanda na biashara, kilimo, kazi za ufundi wa mikono ambazo huchangia katika kuongeza ajira.

Aliongeza kuwa pamoja na Tanzania kuwa na vivutio vingi vya urithi vya kitamaduni, utalii unapaswa kupewa kipaumbele cha kuendelezwa na kutangazwa vya kutosha ili kushawishi watalii kuja kuangalia uwekezaji katika vivutio vilivyopo.

Habari Kubwa