Wapata mafunzo uzalishaji vyakula lishe

12Sep 2019
Grace Mwakalinga
MBEYA
Nipashe
Wapata mafunzo uzalishaji vyakula lishe

WAKULIMA 825 kutoka Kata za Inyala, Itewe na Utengule Usongwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, wamepatiwa mafunzo ya uzalishaji wa vyakula vyenye virutubisho vya mboga na matunda kwenye skimu za umwagiliaji ili kuimarisha afya ya mama na mtoto.

Akizungumza juzi, Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Damas Massawe, alisema lengo ya kutoa mafunzo hayo ni kuongeza uzalishaji wa virutubisho ambavyo vitasaidia kuondoa udumavu kwa watoto.

Massawe alisema idara yake katika utekelezaji wa shughuli za lishe kipindi cha robo ya kwanza ya Julai hadi Septemba 2018/19 imesimamia uzalishaji wa vyakula vyenye virutubisho ili kuimarisha afya ya mama na mtoto.

Alisema katika kuongeza uzalishaji idara hiyo ilitumia maofisa ugani kutoka ngazi za vijiji na kata kutoa elimu kwa kushirikiana na mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile Feed the Future.

"Tulibaini baadhi ya sababu ambazo zinachangia udumavu kwa watoto kuwa ni kukosa viini lishe kutoka kwenye matunda na mboga, hivyo idara ya kilimo katika kupunguza tatizo hilo, tuliandaa mafunzo kwa wakulima kujua namna ya kuongeza virutubisho kwa watoto hao," alisema Massawe.

Alisema katika kukabiliana na udumavu kwa watoto, idara hiyo inakabiliana na changamoto mbalimbali ikiwamo uhaba wa vitendea kazi kama vile pikipiki kwa maofisa kilimo kwenye kata na vijiji pamoja na ubovu wa gari la idara hali inayosababiha kutofanya kazi kwa ufanisi.

Alisema idara imejipanga kuongeza jitihada za kuwezesha uzalishaji wenye tija kwenye kilimo cha mboga na matunda kwa kuwa ndicho chenye vyakula muhimu vya lishe kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa sekta zisizo za kiserikali zilizoko ndani ya halmashauri hiyo.

Mmoja wa wanufaika hao, Mbukwa Mwasandube, kutoka kata ya Ijombe, alisema sababu iliyochangia udumavu kwa watoto ni mtindo wa maisha kutokana na wazazi kuwa na shughuli nyingi za uzalishaji na ujasiriamali na kusahau wajibu wao kwa watoto.

Alisema ili kukabiliana na tatizo la udumavu kwa watoto, serikali kwa kushirikiana na taasisi zingine inapaswa kutoa elimu ya umuhimu wa malezi kwa watoto hasa kwenye lishe.

"Serikali kupitia idara mbalimbali imejitahidi kutoa elimu ya wazazi na walezi kuzingatia milo kamili na kuzalisha vyakula vyenye virutubisho, lakini wamesahau elimu ya malezi kwa watoto," alisema Mwasandube.

Habari Kubwa