Waafikiana kuanzisha mnada wa mahindi

12Sep 2019
Grace Mwakalinga
MBOZI
Nipashe
Waafikiana kuanzisha mnada wa mahindi

WADAU wa Kilimo katika Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe wamekubaliana kuanzisha mnada wa pamoja ambao utatumika kuuzia mazao yao hususan mahindi ambayo soko lake si la uhakika.

Makubaliano hayo yaliafikiwa hivi karibuni wilayani humo wakati wa kikao cha kujadili changamoto ya masoko kwenye zao hilo.

Baadhi ya wadau wa kilimo walisema ili mzalishaji anufaike lazima kuanzisha mnada ambao utawakusanya wakulima wa kutoka maeneo mbalimbali.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA), mkoani Songwe, Charles Chenza, alisema ni wakati mwafaka wa kumsaidia mkulima ili anufaike kwa kuhakikisha anatengenezewa mazingira rafiki ya kuuzia mazao yake.

Chenza alisema kuwapo kwa mnada wa pamoja kutawasaidia wakulima kuuza mazao  kwa bei ya pamoja na kuiomba serikali kusimamia suala hilo ili kuwazuia madalali ambao huwanyonya wakulima.

Aliitaka serikali kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko pamoja na Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuwa wateja wakubwa kwenye minada hiyo ambayo alishauri kuwekwa kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo ili kuwasaidia pia wakulima wanaokaa kwenye maeneo yasiyofikika kirahisi.

"Tukiweka minada kwa kila kata katika wilaya hii hakika tutakuwa tumewasaidia sana wakulima kunufaika na kilimo cha mahindi kwani watauza mazao yao kwa pamoja na kwa bei waliyokubaliana. Tuzidi kuiomba serikali kupitia NFRA kununua kwa wingi mazao yetu," alisema Chenza.

Ofisa Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika Wilaya ya Mbozi, Richard Sirili,alisema ili kupata wateja wa uhakika na kuuza mazao yao bila shida ni muhimu wakulima kuzingatia kilimo cha kisasa ambacho kinazingatia mbegu bora, kulima kwa wakati na kufuata ushauri wa maofisa kilimo.

Diwani wa Idiwili, Christopher Ntandala, aliishauri serikali kuanzisha kituo kikubwa cha ununuzi wa zao hilo (one stopcentre) ambacho kitakuwa kinakusanya mahindi ya wakulima wote wa Mbozi na kuuza kwa pamoja.

Alisema kituo hicho kitakuwa chini ya serikali na kitakuwa na jukumu la kukagua ubora na kutafuta soko la uhakika na kwamba wakati wa kuuza na kununua kuwe na utaratibu wa upashanaji habari.

Mkulima Julius Mwampashe, kwa upande wake aliitaka serikali kurejesha mfumo wa zamani wa ugawaji mbolea za ruzuku, kwa madai kuwa mabadaliko ya sasa yanamkandamiza mkulima kutokana na kuwapo kwa mawakala wasiozingatia bei elekezi.

Habari Kubwa