Wahofiwa kukatisha masomo kisa vyoo

12Sep 2019
Jaliwason Jasson
BABATI
Nipashe
Wahofiwa kukatisha masomo kisa vyoo

WANAFUNZI wa Shule ya awali na Msingi Dudumera katika Halmashauri ya Babati mkoani Manyara, wapo hatarini kukatiza masomo kwa sababu ya uhaba wa matundu ya vyoo na wengine kutokuwa rafiki na matundu
yaliopo.

Hayo yalisemwa juzi  na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Mussa Mkumbo, alipozungumza na Nipashe juu ya ubora wa matundu ya vyoo walivyo navyo, kama yanafaa kwa matumizi ya wanafunzi wa awali.

Alisema shule hiyo ina matundu 10 ya vyoo ambayo yanatumiwa na wanafunzi 95 wa awali na wanafunzi wengine 518, kuanzia darasa la kwanza hadi la saba.

“Sasa kutokana na upungufu wa matundu haya, kunahitajika jitihada za makusudi kwa serikali na wadau wa elimu katika halmashauri ili wanafunzi wetu  wasikatize masomo sababu ya ukosefu wa vyoo,” alisema.

Mkumbo alisema matundu ya vyoo yaliyopo ni machache na hayaendani na umri wa watoto wanaosoma elimu ya awali kwa kuwa ni vyoo vya shimo ambavyo watoto wa awali wanaweza kutumbukia.

"Kama shule haina vyoo vinavyofaa wanafunzi wa awali, wanaweza kuogopa na kuacha shule maana watakuwa wanawaza jinsi wanavyojaribu kuingiachooni na kushindwa kujisaidia," alisema na kuongeza:

"Wanafunzi wengine wa awali wakiona hakuna vyoo wanavyoweza kutumia wengine wanaenda kujisaidia vichakani kwa sababu ya ile hofu ya kuogopa vyoo kuwa vikubwa."

Aidha, alisema katika shule yake wameshindwa kuwa na matundu ya vyoo ya kutosha na vinavyofaa kwa matumizi ya wanafunzi wa awali kutokana na mvutano wa wanakijiji walio nao wa zaidi ya miaka miwili ambao unawafanya miundombinu ya vyoo iendelee kuwa tatizo shuleni hapo.

Pia alisema ukosefu wa ujenzi wa vyoo rafiki kwa wanafunzi wa awaliuna madhara kwa wanafunzi kwa kuwa wanaweza kukata tamaa kwenda shuleni wakihofia vyoo hivyo na kuchukia shule sababu mazingira si rafiki.

Naye Mwalimu wa Shule ya Awali, Jemima Njidile, alikiri kuwa shule hiyo haina vyoo vizuri vya wanafunzi wa awali, kwani kwao inakuwa changamoto na inawalazimu kuwasindikiza chooni wanapohitaji kwenda. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Hamisi Malinga, alikiri kuwapo kwa mvutano wa wazazi ambao umesababishwa na masuala ya kisiasa, kutokana na Kijiji cha Mawemailo kuongozwa na upinzani ambao unapinga kila kitu cha maendeleo.

Malinga alisema jukumu la ujenzi wa miundombinu ya vyoo ni la wananchi kwa asilimia 100 na serikali haiwezi kuchangia kila kitu.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Mawemairo, JumanneMustafa alisema wao hawavutani juu ya ujenzi wa vyoo, bali walisitisha kuchangia vyoo kutokana na michango kuwa mingi, hivyo wanasubiri uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike ili viongozi watakaopatikana walisimamie suala hilo.