Ni upuuzi wanavijiji kumsujudia chatu

12Sep 2019
Mhariri
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ni upuuzi wanavijiji kumsujudia chatu

HUKO mkoani Geita katika Kijiji cha Kasara, wananchi kutoka maeneo mbalimbali wamekusanyika kushuhudia na kumletea zawadi na sadaka  chatu aliyeonekana kwa wiki kadhaa.

Taarifa za kumpelekea mnyama huyo zawadi na kumfurahia kwa madai kuwa ameleta neema zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii,simu na TV mitandao.

Suala hili linadhihirisha kuwa jamii zetu bado ziko nyuma kwenye utambuzi na uelewa wa masuala ya msingi.

Wananchi wengi wanaendelea kuonyesha kuwa wana uelewa  mdogo na hasa pale wanapothubutu kusema kuwa nyoka anawaletea neema.

Kwa mfano wa kumsujudia  chatu huyo ambaye huenda amemeza mnyama mkubwa au amejeruhiwa ndiyo maana anashindwa kutembea, inadhihirisha kuwa wananchi wengi wako gizani.

Kumpelekea nyoka huyo zawadi na sadaka, kama mbuzi, kafara,mtama na vyakula kwa imani kuwa ujio wake unatoa majibu ya matatizo yao ni kurudi nyuma zaidi kimaendeleo katika zama hizi za sayansi na teknolojia.

Katika madai yao viongozi wanadai nyoka huyo atakapokula sadaka zao ni jibu la matatizo yao  kwani wanasumbuliwa na presha, VVU na Ukimwi, kisukari na saratani lakini pia kuna changamoto za upungufu wa mvua  na mavuno mashambani.

Kuamini kuwa nyoka ni jawabu la matatizo makubwa ya njaa, maradhi na umasikini ni matokeo ya athari za kukosa elimu, kuwa na uelewa mdogo na ujinga miongoni mwa Watanzania wengi.

Ujinga unasababisha wana vijiji kuendelea kuathirika katika maisha yao ya kila siku na hata kutishia hatma ya maisha yao ya siku za usoni.

Kuwa na elimu duni ndiko kunakowafanya watu kuamini kuwa nyoka analeta neema na tiba kwa matatizo yao. Imani hizo ndizo zinazoathiri  uchumi,  afya na namna ya kufikiria.

Tunaona kuwa kuamini kuwa nyoka analeta neema ni matokeo ya kuwa na uelewa duni pamoja na kujikita zaidi katika masuala ya kiutamaduni badala ya kujishughulisha na mambo muhimu kama kujifunza na kuujua ukweli.

Ni wazi kuwa kama jamii zingekuwa zinajishughulisha kusoma machapisho kama  magazeti, vipeperushi na kupata taarifa za muhimu kwa ajili ya maisha watu wangefahamu kuwa magonjwa kama VVU, Ukimwi, saratani na kisukari chanzo chake ni kipi.

Aidha, watu  wangeweza kufahamu kuwa mabadiliko ya tabia nchi yanayotokea zama hizi ni chanzo cha uhaba wa mvua, mavuno duni na pia wangefahamu jinsi uharibifu wa mazingira unavyohusika na kujua namna ya kuachana na mambo hayo.

Wakati mwingine jamii hizi zinathibitisha kuwa  Watanzania tunatoa umuhimu mdogo kwenye elimu badala yake tunaamini zaidi utamaduni na mila.

Tukumbuke ukosefu wa elimu unachangia kurithisha vizazi ujinga , maisha duni na matokeo yake ni kuwa na mwendelezo wa umaskini usiokoma na imani za kishirikina zinazodumaza maendeleo.

Uelewa mdogo na imani zisizokuwa na manufaa wakati mwingine umesababisha kutokujiamini na mara nyingi kuishi maisha ya kusaka mchawi na kuhisi kuwa kuna watu wanawaloga wenzao.

Yote hayo yamesababisha mauaji ya albino, wazee na hata watu wanaosingiziwa uchawi katika maeneo mbalimbali.

Imani hizo ndizo zinazoziingiza jamii kwenye fikra kuwa viungo vya wanadamu wenzao ni dawa ya utajiri na yote hayo ni ujinga  ambao unakwamisha jamii kuwa na utaalamu na kufanya mambo yanayochangia kujiletea maendeleo.

Tunawaomba wataalamu wa wanyama pori na mabingwa wa nyoka kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu nyoka huyo na chanzo cha kulala kwa siku kadhaa katika kijiji cha Kasara.

Habari Kubwa