Wodi mpya inayolamba Sh.mil 400 DC akilia na mabusha, ukosefu vyoo

12Sep 2019
Sabato Kasika
Nachingwea
Nipashe
Wodi mpya inayolamba Sh.mil 400 DC akilia na mabusha, ukosefu vyoo
  • Sep 30 kicheko kinamama, watoto
  • RC: Naagiza wanavijiji mbadilike
  • Mrisho Mpoto kuendesha kampeni 

KATIKA kuhakikisha changamoto za afya zinaendelea kupatiwa ufumbuzi Wilaya ya Nachingwea, inayoendelea na ujenzi wa jengo la wodi ya mama na mtoto baada ya kupokea Sh. milioni 400 kutoka serikali kuu.

Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango.

Jengo hilo litakapokamilika, linatarajiwa kuwa na chumba cha upasuaji, sehemu ya akina mama kusubiria kabla ya kujifungua, sehemu ya kuhudumia watoto wenye mahitaji maalum na vyumba vingine muhimu.

Hatua ya serikali kutoa kiasi hicho cha fedha inaelezwa na mkuu wa wilaya hiyo, Rukia Muwango kuwa inalenga kuboresha huduma ya afya kwa mama na mtoto wilayani Nachingwea.

"Serikali kuu imetuongezea kasi ya kuboresha huduma ya afya wilayani kwetu, hivyo sisi viongozi hatuna budi kusimamia ujenzi wa wodi na kuhakikisha unakamilika, kisha kuanza kutumika," anasema Muwango.

Mkuu huyo wa wilaya anasema, lengo la ujenzi ni kuhakikisha wananchi Nachingwea wanapata huduma kwenye mazingira bora na rafiki.

JENGO LIMEKAMILIKA

Msimamizi wa ujenzi wa jengo hilo, Mhandisi Khalifa Kimbendera, anasema ni mradi unaotarajiwa kukamilika tarehe 30 ya mwezi huu, iwapo ratiba itaenda kama walivyopanga. Ni ujenzi ulioanza Aprili mwaka huu na unaendelea vizuri, matarajio yaliyopo ni kukabidhi mradi kupisha hatua nyingine.

"Suala la kutumika siyo la kwangu, kwani hii inategemea kama vifaa vya kutolea huduma vitakuwepo, lakini suala la ujenzi ni kwamba tumepanga kukamilisha Septemba 30," anasema mhandisi huyo wa halmashauri.

Anafafanua kuwa, katika nafasi yake ya uhandisi anasimamia ujenzi tu na suala la kuanza kutumika, ni hatua iliyoko kwenye  mamlaka nyingine, akidokeza inategemea la uwekaji wa vifaa vya kutoa huduma mbalimbali, hasa za mama na mtoto.

 ZAHANATI ZILIZOPO

Kuhusu ujenzi wa zahanati, mkuu wa wilaya anasema kwa muda mrefu umekuwa ukiendelea katika vijiji mbalimbali vya Nachingwea, ikiwamo vituo vya afya na lengo ni kusogeza huduma za afya karibu na wananchi waliko.

Rukia anasema, hadi sasa wilaya ina jumla ya zahanati 39 na vituo vitatu vya afya, ambavyo vipo kata za Kilimarondo, Nambambo na Ruponda, huku juhudi zikiendelea kujenga kituo cha afya.

"Nachingwea ina kata 36, lakini ina zanahati 39, kwa hiyo tumevuka malengo ya ujenzi wa zahanati kwa kila kijiji na sasa tunaelekeza nguvu katika kujenga vituo vya afya na wodi ya mama na mtoto," anasema.

Anasema, mbali na ujenzi wa zahanati na vituo vya afya, wameanza kupunguza kero ya maji kwa kuchimba visima 150 kwenye maeneo mbalimbali ya wilaya hiyo kongwe.

"Maji nayo ni afya, watu wakinywa yasiyo salama wanakuwa katika hatari, ndio maana huku kwetu kuna kampuni ya Gain inaendelea kuchimba visima virefu vya maji, lengo ni kupata maji safi na salama," anasema.

Mama Rukia, anasema kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba wanatembea umbali mrefu kufuata maji na kujikuta wakipoteza muda, hivyo hatua ya kuchimba visima ni mkombozi kwao.

Anasema, uhaba wa maji safi na salama ni tatizo ambalo yeye na viongozi wenzake wanaendelea kulitafutia suluhisho ili kuhakikisha vijiji vyote vinapata huduma hiyo muhimu, tena maeneo ya karibu.

 KILIO CHA MABUSHA

Mkuu wa wilaya anasema, mabusha na tezi dume ni magonjwa yanayowasumbua wakazi wa wilaya yake, hususan wanaume, akitoa takwimu, kwamba mwezi Julai mwaka huu, jumla ya watu 150 walifanyiwa upasuaji wa mabusha na wengine waligundulika kuwa na tezi dume.

Anasema matibabu hayo yalitolewa bure na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ili kuwasaidia wakazi wa Nachingwea, ambao ni sehemu ya wakazi wa mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani, wanaosumbuliwa na maradhi hayo.

"Kabla ya upasuaji, madaktari walikuwa wanawapima afya zao, lakini wengi wao walibainika kuwa na magonjwa hayo mawili wakawaacha. Kwa maelezo ya kitaalam ni kwamba, mwenye tezi dume hawezi kupasuliwa busha," anasema.

Rukia anasema tatizo la tezi dume na mabusha ni kubwa na kwa sasa anahangaika kutafuta wadau mbalimbali wamsaaidie kufanikisha kampeni ya kutokomeza magonjwa hayo mawili.

"Nilisimamia kampeni ya upasuaji wa mabusha, sasa sina budi kusimamia hata hilo la ugonjwa wa tezi dume, kwani tatizo hili ni kubwa sana huku kwetu, hivyo ndivyo madaktari walibaini," anasema.

VYOO TATIZO

Akizungumza mjini hapa hivi karibuni, Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi, anasema wilayani Nachingwea kuna watu wengi wasio na vyoo bora, hivyo anaagiza kila mkazi asiye na choo bora ahakikishe anakiboresha haraka iwezekavyo.

Huku akiwanyooshea kidole kinababa ambao ndio vichwa vya nyumba kwa kauli; “Haiwezekani mtu anajiita mwanaume, wakati nyumbani hana choo au ana choo kibovu, ambacho wakati wowote kinaweza kuhatarisha maisha kwa uzembe wake mwenyewe

"Kumbukeni nyumba ni choo na kuna kampeni zimekuwa zinaendelea zinazohusiana na ujenzi wa vyoo bora, lakini inashangaza nyie bado mko nyuma katika ujenzi wa vyoo hata hapa mjini."

Agizo lake wakazi wa Nachingwea wabadilike kuwa watu wa kisasa wanaoenda na wakati kwa kulinda afya zao, badala ya kuridhika na maisha walio nayo kila siku, huku bila ya vyoo bora.

Katika hilo, Mkuu Wilaya Rukia, anasema tatizo hilo na vyoo bora vipo kwa kiwango asilimia 56, akitoa sababu baadhi ya watu ni wagumu kuelewa umuhimu wa vyoo bora.

"Wito wangu ni kwamba choo ni ustaarabu, pia ni afya na ni muhimu kukitumia. Kwa hiyo, kila mmoja wetu awe na choo bora na kukitumia kikamilifu kwa afya yake," anasema.

Katika kufanikisha ujenzi wa vyoo bora, ana mpango wa kumwita Balozi wa Kampeni ya 'Nyumba ni Choo' msanii Mrisho Mpoto, afike Nachingwea kwa ajili ya kuendesha kampeni ya kujenga vyoo bora.

Mkuu wa Wilaya, naamini kwamba ni hatua inayoweza kusaidia kwa kiasi kikubwa kuwabadilisha wakazi wa Nachingwea na hatimaye wakajenga vyoo vinavyotakiwa kwa ajili ya afya bora.

Habari Kubwa