WHO: Kila sekunde 40 yupo anayejiua duniani

12Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
WHO: Kila sekunde 40 yupo anayejiua duniani
  • Wawazidi wanaouawa; wanaume zaidi; vijana  chanzo namba 2

SHIRIKA la Afya Duniani (WHO), limesema karibu wastani wa watu 800,000 hujiua kila mwaka duniani, ikiwa ni kiasi kinachowazidi wanaokufa ama kwa vita na mauaji, akiyataja kuwa mauaji ya mtu dhidi ya mwingine au saratani ya matiti.

Mkurugenzi Mkuu WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Katika ripoti yake mpya, WHO inasema viwango vya wastani wa kujiua duniani vimepungua, ikilinganishwa na kipindi kati ya mwaka 2010 na 2016.

Hata hivyo, ikirejea watu wanaojiua, idadi imeendelea kuwa ileile, kutokana na ongezeko la idadi ya watu duniani.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Tedros Adhanom Ghebreyesus, anasema katika taarifa kuwa licha ya hatua zilizopigwa, wastani uliopo kuna mtu anafariki kila sekunde 40 kutokana na kujiua.

Takwimu za mwaka 2016 ambao ndiyo wa mwisho kutolewa kuhusu kujiua, zilionyesha kuwa kwa kila watu kulikuwapo watu 100,000  wanaojiua na katika vifo hivyo kuna wastani wa vifo 10.5 vinavyotokana na kujiua.

Inagawa inaelezwa wastani wa viwango vya kujiua duniani vilipungua kwa takriban asilimia 10 kuanzia 2010 hadi 2016, Kanda ya Amerika ilionyesha ongezeko la viwango hivyo kwa asilimia sita, katika kipindi cha miaka sita.

Mtaalamu kutoka Kitengo cha Afya ya Akili cha WHO, Alexander Fleischmann, anasema mauaji ya kujiua ni tatizo kubwa la afya ya jamii na kutoa wito wake ni hatua zichukuliwe kushughulikia tatizo hilo.

"Ni muhimu wakati wote katika kuzuia vifo vya kujiua, kwamba tunawashikilia watu wanaotuzunguka. Tunapaswa kuchukulia kwa uzito mtu anaposema hataki tena kuishi au hata wanaposema kwa uthabiti kwamba wanataka kujitoa uhai wao.

“Kila moja wetu ana jukumu katika kuzuia vifo vya kujiua. Hivyo, sote tunaweza kujitolea kuwasikiliza watu wanaotuzunguka wanapokuwa kwenye huzuni au wanataka msaada wetu,” anasema.

Ripoti hiyo ya WHO, inasema idadi ya mataifa yaliyo na mikakati kuzuwia watu kujiua imeongezeka katika kipindi cha miaka mitano tangu kuchapishwa ripoti ya kwanza ya dunia ya WHO.

Idadi ya jumla ya mataifa yaliyo na mikakati hiyo, ambayo ni 38, inalaezwa  kuwa bado ndogo sana na kuongeza kuwa serikali zinahitaji kujifunga kuanzisha mikakati hiyo.

Kujiua kulishika nafasi ya pili katika vyanzo vya kusababisha vifo vingi miongoni mwa vijana wenye umri kati ya miaka 15-29, baada ya majeraha yanayotokana na ajali za barabarani.

Mbinu zinazotumiwa zaidi katika kujiua ni pamoja na kujinyonga na kujipiga risasi, hususani katika maeneo ya vijini, kunywa dawa za sumu za kuulia wadudu.

Ripoti inabainisha kuwa, mauaji zaidi yanatokea katika mataifa maskini na yenye maendeleo ya kati, ambako idadi kubwa ya watu duniani wanaishi, pia viwango ni vikubwa zaidi katika mataifa tajiri.

Baada ya Guyana, Russia inatajwa kuwa ya pili kwa idadi kubwa ya watu wanaojiua. Mataifa mengine yaliyoko kwenye orodha hiyo ni pamoja na Lithuania, Lesotho, Uganda, Sri Lanka, Korea Kusini, India, Japan na Marekani.

Katika nchi nyingi, wanaume wana uwezekano mkubwa zaidi wa kujiua kuliko wanawake. Ni katika mataifa matano tu ya Bangladesh, China, Lesotho, Morocco na Myanmar, ambako wanawake zaidi wanajiua kuliko wanaume. DW