Nusu wakazi mkoa Shinyanga hawana vyoo; mbadala porini, mifuko, pagal

12Sep 2019
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
Nusu wakazi mkoa Shinyanga hawana vyoo; mbadala porini, mifuko, pagal
  • Kwanini? Eti uchuro kuchangia na wakwe 
  • Operesheni lazima choo kupita kila nyumba 
  • Magari majitaka manispaa yatapisha porini

 

  •  
  •  
  •  

KAMPENI ya usafi wa mazingira kitaifa nchini Tanzania, ilizinduliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Mei 5. 2012 Mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro

Mkuu wa Mkoa Shinyanga, Zainabu Telack, akiwa na Balozi wa Kampeni ya ‘Nyumba ni Choo,’ Mrisho Mpoto.

 

  •  
  •  
  •  

KAMPENI ya usafi wa mazingira kitaifa nchini Tanzania, ilizinduliwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, Mei 5. 2012 Mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro

Inaelezwa, usafi wa mazingira hauishii katika mazingira, katika kufagia, kufyeka nyasi na kuzibua mitaro michafu tu, bali hata kaya kuwa na choo kuhakikisha magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu hayapewi nafasi kuhatarisha afya za wananchi.

Rais Dk. John Magufuli, mara tu baada ya kuingia madarakani, aliagiza kufanyika usafi nchi nzima kila siku ya Jumamosi ya mwisho wa mwezi, ili kuhakikisha wananchi wanakuwa katika mazingira safi kiafya.

Takwimu za mkoa zinaonyesha nusu pekee (asilimia 50.6) ya wanajamii hao ndio wenye vyoo bora na waliobaki kuviweka kama maonyesho kwa ajili ya kumridhisha bwana afya wakati wa ukaguzi wa vyoo.

Nini tatizo? Kuna mila potofu kuwa wanajamii hawapo tayari kuchangia choo kimoja na wakwe zao, jambo linalomkera zaidi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainabu Telack.

Anaamua kulivalia njuga suala hilo, la ujenzi wa choo na kuzindua kampeni ya ‘nyumba ni choo’ inayolenga kuhakikisha hadi kufikia mwezi Desemba mwaka huu, kila kaya mkoani inakuwa na choo bora kinachotumiwa.

Mkuu wa Mkoa huyo anasema: “Haiwezekani wananchi waendelee kuishi kwenye nyumba zao bila ya kuwa na choo. Ni aibu sana kwenda kujisaidia vichakani; baba, mama, watoto pamoja na wageni wanaofika kwenye familia hiyo, hatimaye kuchafua mazingira.

“Suala la kaya kutokuwa na choo kwenye mkoa wangu sikubaliani nalo, hivyo naagiza maofisa afya wote wa mitaa mniletee mpango wenu kazi, ili tuanze kukagua choo nyumba kwa nyumba, na ambayo tutaikuta haina choo tutaichukulia hatua. Lengo letu hadi kufikia Desemba (2019) kaya zote ziwe na huduma ya choo.”

Anaongeza: “Kwa vile tunaelekea kwenye kipindi cha Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, nawaomba sana wanasiasa wasije wakatuingilia kwenye zoezi hili, hasa pale tutakapokuwa tukiwakamata wananchi wasio na vyoo na kuanza kuwakingia kifua eti tuwaache ni wapiga kura wao, kwani hatutaki mzaha kwenye jambo hili.”

Ofisa Afya

Neema Simba ni Ofisa Afya wa Mkoa wa Shinyanga, anasema kuwapo wakazi milioni 1.8 wanaopatikana katika kaya 284,701, lakini wanaotumia vyoo bora ni kaya 129,820 sawa na asilimia 50.6 na wasio na vyoo kabisa ni kaya 7,195 sawa na asilimia 5.5.

Anataja takwimu za kaya zenye vyoo bora kwa kila halmashauri sita za mkoa huo, katika Mji Kahama, kuna kaya 55,708 lakini wenye vyoo ni asilimia 75; Msalala kuna kaya 42,920 na wanaotumia vyoo ni asilimia 57,3 na wasio na vyoo asilimia 4.4.

Halmashauri ya Ushetu, wanaotumia vyoo ni asilimia 20.9; Shinyanga Manispaa wenye vyoo ni asilimia 64.7; Shinyanga Vijijini wanaotumia vyoo ni asilimia 19.7; Halmashauri ya Wilaya Kishapu, wanaotumia vyoo ni asilimia 71.

“Kampeni hii ya ‘Nyumba ni Choo’ ya kupita nyumba kwa nyumba kukagua choo, itasaidia kwa kiasi kikubwa kuondokana na tatizo la watu kujenga nyumba zao, bila ya kuwa na huduma ya choo, hatimaye kuondoa wasiwasi mkubwa wa kupatwa na magonjwa ya mlipuko, hasa kwenye kipindi cha mvua,” anasema ofisa afya.

Wakazi wasemavyo

Jonasi Apolo ni mkazi wa Shinyanga, anasema tatizo la nyumba nyingi kutokuwa na choo si vijijini pekee kama baadhi wanavyodhani, bali hata mjini kuna tatizo la kukosekana vyoo, hasa kwenye nyumba za kupanga, ambako wanajisaidia katika mifuko na mapagala ya majengo.

Apolo anafafanua matatizo ya vyoo katika nyumba wanazoishi mijini, akisema: “Hapa mjini kuna nyumba nyingi hazina vyoo kabisa, hasa hizi ambazo tunapanga. Utakuta watu wote wanatoka mmoja mmoja kwenda kujisaidia ambako hakujulikani, pamoja wengine kwenye mapagala.”

Mkazi wa mjini Shinyanga, Protas Nzelano, anaipongeza operesheni hiyo ya Mkuu wa Mkoa, kusaka nyumba kwa nyumba vyoo bora, itasaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uchafuzi wa mazingira.

“Namuomba Mkuu wa Mkoa kwenye kampeni hii ya ujenzi wa vyoo kwenye makazi ya watu aunde kabisa ‘task force’ (kikosi kazi) watu wakamatwe. Haiwezekani mtu unajenga nyumba, halafu hakuna choo, eti unakwenda kujisaidia vichakani. Hii ni dharau kwa kuchafua mazingira kwa makusudi,” anasema Nzelano.

Mrisho Mpoto

Balozi wa Kampeni ya ‘Nyumba ni Choo’ ni msanii, Mrisho Mpoto, anasema wapo mkoani Shinyanga kuungana na serikali kuhakikisha wakazi wote nyumba zao zinakuwa na choo na kuacha tabia ya kujisaidia vichakani wakichafua mazingira.

Anasema mwaka 1961 wakati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, alipowezesha Tanganyika kupata uhuru, alianza kupigana na maadui watatu, ambao ni Ujinga, Umaskini na Maradhi na mwaka 1973 ikaanzishwa kampeni ‘Mtu ni Afya.’

Mpoto analalamika kwamba, hadi sasa imetimu miaka 58 sawa na nusu karne, akilaumu kuwa ni jambo la aibu kubwa.

“Mpango wa Dunia hadi kufikia Mwaka (2030) nyumba zote nchini ziwe na vyoo bora, lakini Mpango wa Tanzania kufikia (2022) nyumba zote zinatakiwa ziwe na vyoo. Ndio maana tunafanya kampeni hii kwenye mikoa yote kuhamasisha wananchi wajenge vyoo kwenye nyumba zao.

 “Kampeni hii ya usafi wa mazingira ya kuhamasisha wananchi wajenge vyoo bora, pia tumeifanya kwenye mikoa ya Tanga, Morogoro, Mbeya, Songea, Kagera, Mwanza, Geita, Mara, na sasa tupo Shinyanga, ambayo tutahamasisha ndani ya siku 21 watu wajenge vyoo kwenye nyumba zao,” anaongeza.

Pia, rai yake ni Watanzania waitikie wito wa kampeni hiyo ya nyumba kwa vyoo, ili nchi iondokane na suala la kujadili ujenzi wa vyoo kila kukicha, jambo ambalo katika sura ta pili, linafungua mlango viongozi kujadili mengine yahusuyo nchi.

Mratibu wizarani

Mratibu wa Uhamasishaji Kampeni ya ‘Nyumba ni Choo’ kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Elizabeth Malingumu, anasema kwenye utoaji wa hamasa hiyo, watazunguka mkoa mzima wa Shinyanga, kutoa elimu ya umuhimu wa kuwa na choo.

Anasema jamii nyingine hasa za maeneo ya vijijini, wengi wameshaathiriwa na mila zilizopitwa na wakati, wakiwamini katika kujisaidia vichakani, jambo linalohitaji juu ya umuhimu wa matumizi ya choo.

“Kampeni yetu hii ya ‘Nyumba ni Choo’ tutazunguka nchi nzima. Kuna baadhi ya mikoa tayari tumeshapita na sasa tupo hapa Shinyanga. Lengo letu ni kuhamasisha usafi wa mazingira, kwa wananchi kujenga vyoo bora kwenye nyumba zao, na kuacha kujisaidia ovyo na kusababisha uchafuzi wa mazingira,” anasema Malingumu.

“Vyoo bora ambavyo tunataka wananchi wavijenge, ni vile ambavyo vina paa juu, mlango, sakafu chini, kuna maji na sabuni ya kunawia mikono, pamoja na bomba la kupumulia, ili kuondoa harufu chooni,” ameongeza.

Mdau Mwakilishi

Elisekile Bwile, Mwakilishi wa shirika la maendeleo kutoka Uholanzi (SNV), wanaohusika na miradi ya uboreshaji mazingira, anasema mkoa Shinyanga wanashirikiana kikamilifu na serikali katika kutunza usafi wa mazingira.

Anasema, katika utunzaji usafi huo wa mazingira, wanatekeleza mradi wa Shinyanga Mjini, ambako hakuna mfumo wa kuhifadhi majitaka, vinyesi vinavyonywa vyooni, badala yake hupelekwa kumwagwa porini, hali inayoangukia uchafuzi wa mazingira.

Ushauri wa ofisa  huyo, ni kwamba wananchi wa mkoani Shinyanga wanapojenga vyoo vyao waweke mfumo mzuri utakaosaidia onyonyaji wa majitaka, vyoo vitakapojaa vinyesi.

Habari Kubwa