Zahera ahisi kitu Balinya, Molinga kukosa mabao 

12Sep 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Zahera ahisi kitu Balinya, Molinga kukosa mabao 

LICHA ya kuanza kuonyesha cheche zake za kucheka na nyavu, Kocha Mkuu wa Yanga, Mkongomani Mwinyi Zahera amehoji kuna nini kwa washambuliaji wake wawili, raia mwenza David Molinga aliyefunga mabao mawili wakati wakishinda-

-3-0 kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Toto Africans juzi pamoja na Mganda Juma Balinya.

Molinga ambaye mashabiki wanaamini Yanga imeingia 'chaka' kutokana na kushindwa kuonyesha uwezo wa kufunga kwenye mechi za kirafiki anazopewa nafasi, katika mechi hiyo ya kirafiki iliyopigwa Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza alifunga mabao mawili kabla ya Zahera kumtoa, lakini pia Balinya naye akiandamwa na ukame wa mabao tangu ajiunge na timu hiyo msimu huu akitokea Polisi FC ya Uganda.

Akizungumza baada ya mechi hiyo juzi, Zahera alionyesha kushangazwa na washambuliaji hao akiwataka wanaowabeza wajiulize kuna nini nchini kwa kuwa walipotoka walikuwa ni miongoni mwa wafungaji bora.

"Sijui kuna nini hapa, mchezaji kama huyu Falcao (David Molinga) kule Congo alikuwa namba mbili kwa ufungaji akiwa na mabao 15 baada ya Jackson (Muleka) wa TP Mazembe na huyu Juma (Balinya) aliongoza Uganda kwa kufunga mabao 21, sasa jiulize kuna nini hapa," Zahera alihoji.

Hata hivyo, Zahera alisema ni suala la muda tu kabla ya washambuliaji wake hao kuanza kutupia huku akiwatoa hofu mashabiki wa timu hiyo kuhusu kufanya vizuri kwenye mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Zesco Jumamosi.

Zahera bado anaamini uwezo wa washambuliaji wake huku akijipanga kutatua tatizo hilo sugu la kushindwa kutumia vema nafasi wanazotengenezewa.

Katika ushindi huo wa juzi dhidi ya Toto Africans, mbali Molinga aliyetupia mawili dakika ya 37 na 41, bao la tatu lilifungwa na kiungo mpya, Mzanzibari Abdulaziz ‘Bui’ Makame dakika ya 51.

Mbali na Molinga na Balinya, safu ya ushambuliaji ya Yanga inaundwa pia na Patrick Sibomana, Sadney Urikhob na Maybin Kalengo.

Habari Kubwa