Samatta kurejea uwanjani mapema

12Sep 2019
Somoe Ng'itu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Samatta kurejea uwanjani mapema

NAHODHA wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars na mshambuliaji wa Klabu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu Ubelgiji, Mbwana Samatta, atarejea uwanjani hivi karibuni baada ya majibu ya vipimo alivyofanyiwa kuonyesha, mguu wake ulipata mstuko na si jeraha kubwa, imefahamika.

Samatta alipata maumivu wakati akiitumikia Taifa Stars dhidi ya Burundi katika mechi ya kuwania tiketi ya kutinga hatua za makundi kusaka kufuzu fainali zijazo za Kombe la Dunia nchini Qatar 2022, iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam Jumapili iliyopita kwa wenyeji kusonga mbele katika michuano hiyo.

Hata hivyo, Samatta hakuwa tayari kufanyiwa mabadiliko mapema katika mechi hiyo iliyokuwa ya "kufa ama kupona", mpaka pale alipoona hali imekuwa mbaya na hivyo kuliruhusu benchi la ufundi kumtoa nje.

Akizungumza na gazeti hili jana, Samatta, alisema anamshukuru Mungu maumivu aliyopata hayakuwa makubwa na sasa atapata matibabu na kurejea uwanjani ndani ya siku chache.

Mshambuliaji huyo alisema kwamba baada ya kupona, anaamini atarejea uwanjani na kuendelea kupambana ili kuisaidia klabu yake pamoja na taifa lake la Tanzania.

"Asante Mungu, nashukuru baada ya kufanyiwa uchunguzi, daktari amesema sehemu iliyopata majeraha imetokana na mshtuko na si kuvunjika, yaani amesema kama ingekuwa imeumia, muda wa chini ningekaa nje ya uwanja kwa muda wa miezi sita, lakini sasa nitakaa muda mchache na kurejea uwanjani," alisema Samatta.

Mbali na kupambana kwa ajili ya Genk, Samatta pia bado anajiweka sokoni kupata timu ya kuitumikia barani Ulaya na hasa akiitaka Ligi Kuu England, wakati huu akiwa amebakisha miaka miwili katika mkataba wake na klabu hiyo ya Ubelgiji.

Katika mchezo huo, Stars iliwaondoa Burundi kwa penalti 3-0, baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya mabao 2-2 kufuatia sare ya bao 1-1 nyumbani na ugenini.

Habari Kubwa