Nyoni: Moto sasa kwa Sudan Taifa

12Sep 2019
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Nyoni: Moto sasa kwa Sudan Taifa

BEKI wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Erasto Nyoni, amesema kwa kasi ile ile sasa wanapaswa kuelekeza nguvu zao kwenye mchezo dhidi ya Sudan wa kuwania kufuzu fainali za Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).

BEKI wa timu ya Taifa, Taifa Stars, Erasto Nyoni.

Erasto alikuwa sehemu ya kikosi cha Taifa Stars kilichowatupa nje Kenya kwenye mchezo wa kwanza hatua ya awali ya michuano hiyo na pia akawa sehemu ya kikosi cha Stars kilichoitupa nje Burundi kwenye mchezo wa kuwania kufuzu kushiriki hatua ya makundi kusaka tiketi ya kucheza fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika nchini Qatar 2022.

Akizungumza na gazeti hili jana, Nyoni alisema hamasa kubwa iliyokuwapo kuanzia kwa mashabiki waandishi wa habari, viongozi mpaka wao wachezaji ndio imefanikisha matokeo mazuri waliyoyapata kwenye michezo iliyopita.

"Bado tuna kazi ngumu katika mashindano yote tunayoshiriki, mchezo unaofuata ni dhidi ya Sudan, kwa sasa tunapaswa kuelekeza nguvu zetu kwenye mchezo huo na kuunganisha nguvu kama ilivyokuwa katika michezo iliyopita, kikubwa tunataka kufanya vizuri na kufikia malengo yetu na ya kila shabiki na Watanzania kwa ujumla," alisema Nyoni.

Alisema hakuna mchezo mwepesi mbele yao na kila mechi ni ngumu, hivyo lazima wajipange, lakini pia hamasa iwe kubwa.

Stars itaanzia nyumbani Septemba 20, mwaka huu, dhidi ya Sudan katika mechi hiyo ya kuwania kufuzu CHAN itakayochezwa Uwanja wa Taifa.

Habari Kubwa