Watumishi wasiobadilika zama hii itawatumbua, jiangalieni

12Sep 2019
Raphael Kibiriti
DAR ES SALAAM
Nipashe
Watumishi wasiobadilika zama hii itawatumbua, jiangalieni

KUNA mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika uga wa kiserikali tangu awamu ya tano iingie madarakani mwaka 2015.

Mabadiliko haya yanatoa nuru ya kufikia malengo mbalimbali ya kitaifa yanayolenga ustawi wa Watanzania.

Serikali imelenga kuifanya Tanzania kuwa nchi ya kipato cha kati ifikapo mwaka 2025, na ndiyo maana ya jitihada zinazoendelea kufanyika kwa njia tofauti sasa ili kuifikia dhamira hiyo.

Katika hili Muungwana anatoa mifano ya miradi mikubwa ya kimkakati kama ule wa uzalishaji umeme wa Stigler’s Gorge, wenye thamani ya takribani Sh. Trilioni 6.5 hadi kukamilika kwake.

Mradi huo unatarajiwa kuzalisha megawati 2,115 za umeme na hivyo kumaliza mahitaji ya nishati hiyo kwa wananchi, pia kuchagiza Tanzania inayoongozwa na uchumi wa viwanda.

Kuna mradi wa Ujenzi wa Reli ya Kisasa ya (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na Kigoma, ambao tayari umeshaanza kwa vipande viwili.

Kipande cha kwanza kinaanzia Dar es Salaam hadi Morogoro, chenye umbali wa kilometa 300 na kinatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu.

Kipande cha pili kinatoka Morogoro hadi Makutopora (Manyoni), chenye umbali wa kilometa 422, kikitarajiwa kukamilika Februari 2021.

Serikali pia imenunua ndege nane mpya, hatua iliyoliwezesha Shirika letu la ndege la TCL, kufufuka na hivyo kuchagiza sekta ya usafiri wa anga na ya utalii kwa ujumla, hatimaye kuongeza pato la taifa.

Na miradi mingi inayolenga kutoa huduma kwa wananchi ikiwamo ya afya, miundombinu ya barabara, taasisi za kielimu, shule, maji na mingine, yote ni katika dhamira ya kustawisha maisha yao.

Kimsingi miradi mingi inaendelea vizuri, kwa wakati, kwa muda uliopangwa na kwa sehemu kubwa hilo limewezekana kutokana na mabadiliko ya kimtazamo kwa watendaji na watumishi wa serikali, taasisi na mashirika ya umma.

Mabadiliko ambayo yamewezeshwa na msimamo madhubuti wa viongozi wakuu kwa maana ya Rais John Magufuli na wasaidizi wake Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Msimamo unaowasisitiza walio katika ofisi za umma kuwa watumishi wa wananchi badala ya watawala.

Matunda yake ni haya ambayo pamoja na mengine, yamewezesha makusanyo ya serikali kupanda hadi kufikia zaidi ya Sh. Trilioni moja kwa mwezi, hivyo kuijengea serikali uwezo wa kugharimia miradi yake mbalimbali ya kimkakati.

Pamoja na kwamba wizara, idara, taasisi na mashirika mengi ya umma yameweza kuendana na kasi ya zama hizi za serikali ya awamu ya tano, bado kuna mashirika, idara na taasisi ambazo zinaangushwa na baadhi ya watumishi wake katika suala zima la kuhudumia wananchi.

Ninatolea mfano wa Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) na Shirika la Umeme nchini (Tanesco) ambapo baadhi ya wafanyakazi wake wanayaangusha kwa kutoendana na kasi ya awamu hii.

Kwa mfano Muungwana alimshangaa msoma mita mmoja wa Dawasa, Ofisi ya Boko aliyemtishia kumkatia maji mteja mmoja eneo la Tegeta iwapo hatanunua kifaa kinachoruhusu maji kupita kwenye mita ya maji.

Kifaa hicho cha kwenye mita, mali ya Dawasa kilikuwa kimelegea na hivyo kuruhusu maji mengi yavuje, kitu ambacho ni hasara kwa Dawasa.

Kwamba badala ya Dawasa kukirudishia kifaa hicho, msoma mita akamtaka mteja akinunue halafu atoe taarifa kwa Dawasa ili itume mafundi wa kukifunga!

Wakati msoma mita huyo akimtishia kumfungia maji mteja asiyedaiwa bili na Dawasa, bomba ambalo linapeleka maji eneo hilo lina miezi miwili sasa linavuja na taarifa imeshatolewa kwa Dawasa.

Aidha, msoma mita huyo amekuwa akiliona bomba hilo linavuja mara kwa mara, kwa sababu anapita huko.

Sasa badala ya kuchukua hatua ya kuziba bomba hilo linalopeleka maji kwa wateja wengi, anamgeukia mteja mmoja afanye kazi ambayo kimsingi ni ya Dawasa.

Zipo taarifa pia kwa baadhi ya ofisi za Tanesco kutochukua hatua mapema pale zinapojulishwa uwapo wa nguzo za umeme zilizoanguka, zilizooza ama nyaya za umeme wa Tanesco zilizokatika hadi matatizo yakiwamo ya maafa yanapotokea.

Ni rai basi ya Muungwana kwa idara, taasisi na mashirika ya umma ambayo bado baadhi ya watumishi wake wanafanya kazi kwa mapuuza, kuachana na aina hiyo ya utendaji.

Anaasa hivyo kwa sababu zama hizi ni za kitabu kingine na kwamba serikali na Watanzania kwa ujumla wanataka kukimbia katika dhima nzima ya maendeleo badala ya kutembea.

Na hiyo ni katika dhamira ya kuifanya Tanzania nchi ya kipato cha kati ifikapo 2025.

Habari Kubwa