Mitihani darasa la saba yafanyika kwa amani 

12Sep 2019
Romana Mallya
DAR ES SALAAM
Nipashe
Mitihani darasa la saba yafanyika kwa amani 

ULINZI na usalama katika mitihani ya kumaliza darasa la saba unaoendelea leo nchini baada ya kuanza jana, umeimarishwa kila kona, huku wananchi wakizuiwa kupita kwenye maeneo ya shule ambazo wanafunzi wanafanya mtihani huo.

Nipashe jana ilishuhudia katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam ulinzi ukiwa umeimarishwa, huku baadhi yake mageti ya kuingilia kwenye shule yakiwa yamefungwa na polisi wakizuia watu wasiohusika kuingia.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mapambano, Yonas Silvester, aliliambia gazeti hili kuwa hali ni nzuri na mitihani ilifika kwa muda uliopangwa.

"Watoto walifika kwa wakati na sasa wako mapumziko wanasubiria kuingia katika mtihani wao wa pili kwa siku hii ya leo. Mitihani hii itafanyika muda wa siku mbili kwa maana kesho (leo) watamaliza," alisema.

Gazeti hili lilipita katika Shule za Msingi Shekilango, Kijitonyama, Kisiwani, Kilimani, Tandale Magharibi, Muhalitani, Msisiri ambapo kote hali ilikuwa shwari na wanafunzi hadi saa 8:30 mchana walikuwa kwenye vyumba vya mitihani.

Katika Shule za Msingi Mchangani na Kisiwani,  geti la kuingilia lilikuwa limefungwa kuhakikisha watoto wanafanya mitihani yao bila mwingiliano wa watu ndani ya shule hizo.

Kwenye shule ambazo hazina uzio, gazeti hili lilishuhudia askari polisi wakiwarudisha walikotoka wananchi waliokuwa wakitaka kukatisha ndani ya shule hiyo.

Juzi, Baraza la Taifa la Mitihani la Tanzania (Necta) lilitangaza kuanza kufanyika kwa mitihani hiyo kwa muda wa siku mbili kuanzia jana na leo huku likitaja idadi ya watahiniwa waliosajiliwa kuufanya kuwa ni 947,221.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Charles Msonde, alisema kuwa kati ya watahiniwa 947,221 waliosajiliwa mwaka huu kufanya mtihani huo ni wa kutoka katika shule 17,051 Tanzania Bara.

Alisema kati yao wavulana ni 451,235 sawa na asilimia 47.64 na wasichana ni 495,986 sawa na asilimia 52.36.

Alisema watahiniwa 902,262 wataufanya mtihani huo kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 44,959 wataufanya kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia.

"Watahiniwa wenye mahitaji maalum ni 2,678 ambapo kati yao 81 ni wasioona, 780 wenye uoni hafifu, 628 wenye ulemavu wa kusikia, 325 ni wenye ulemavu wa akili na 864 ni wenye ulemavu wa viungo vya mwilini," alisema.