Ugonjwa unaomsumbua Askofu Ruwa’ichi watajwa

12Sep 2019
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ugonjwa unaomsumbua Askofu Ruwa’ichi watajwa

DAKTARI Bingwa wa Upasuaji wa Ubongo, Uti wa Mgongo na Mishipa ya Fahamu wa Tasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Prof. Joseph Kahamba, ameeleza ugonjwa uliompata Askofu Mkuu wa  Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mhashamu Yuda Thadeus Ruwa’ichi hadi kusababisha kufanyiwa upasuaji.

Askofu Mkuu Ruwa’ichi alifanyiwa  upasuaji  usiku wa manane kuamkia juzi katika Taasisi ya Mifupa (MOI).

Alieleza ugonjwa uliompata ni damu kuvimbia kwenye ubongo ambao  kitaalam unaitwa ‘Chronic Subdural Haematoma’.

Alisema alifanyiwa upasuaji mkubwa wa ubongo na kuondoa uvimbe huo, uliochukua saa nne chini ya madaktari bingwa watatu, na kwamba hali yake inaendelea vizuri wakati akiendelea kuwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU).

Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Prof. Kahamba, alisema hali ya kiongozi huyo wa Kanisa, inaendelea vizuri na anaweza kuzungumza.

“Tunashukuru hali ya mgonjwa inaendelea vizuri tofauti na kabla hatujamfanyia upasuaji. Alifika hapa juzi usiku (Septemba 9) akitokea Hospitali ya Rufani ya KCMC mkoani Kilimanjaro, na tulipewa taarifa na wenzetu kuwa walimfanyia upasuaji, lakini hali yake ikaendelea kuwa mbaya,” Prof. Kahamba alisema.

Alisema walipomfikisha MOI walianza kumfanyia vipimo na kubaini tatizo hilo na walianza kumfanyia upasuaji saa 7:00 usiku hadi saa 10:00 alfajiri.

 “Leo (jana) hali yake inaendelea vizuri, ameshaamka anajitambua na anafuata maelekezo anayopewa, na anazungumza taratibu baadhi ya maneno,” Prof. Kahamba alisema.

Aidha, alisema wameunda timu ya wataalamu saba ambao wanamfanyia uchunguzi wa kina katika kuhakikisha afya yake inarejea kama ilivyokuwa awali.

Aliwataja wataalamu ambao wanamfanyia uchunguzi ni madaktari bingwa watatu wa magonjwa ya ubongo, dawa za usingizi na magonjwa ya ndani.

Alisema wataamu wanne ni wa masuala ya chakula na lishe, mazoezi tiba, watalaamu wa uchunguzi na wauguzi.

“Wataalam hawa saba wa uchunguzi watafanya kazi hiyo ili kuhakikisha afya ya Askofu inarejea katika hali yake ya kawaida na huwa tunafanya kwa wagonjwa wengine wanaopata tatizo kama hili,” Prof. Kahamba alisema.

SABABU ZA UGONJWA

Prof. Kahamba alisema sababu za ugojwa huo hazijulikani, lakini ni tatizo linalotokea mara kwa mara kwa watu wengi.

Alitaja baadhi ya mambo yanayosababisha ni kuumia kichwani, shinikizo kubwa la damu linaloweza kusababisha mishipa ya damu kupasuka na matumizi ya dawa zikiwamo za kupunguza maumivu ambazo zinasababisha damu kulainishwa na kuvimbia kichwnai.

Prof. Kahamba alisema mgonjwa asipopata matibabu ya haraka, damu inaendelea kuvunja kichwani, ujazo wa damu unapoendelea kuzidi unapeleka mgandamizo kwenye ubongo na athari kuongezeka na kusababisha mgonjwa kupoteza maisha.

“Mgonjwa wa namna hii inapaswa kupata matibabu ya haraka iwezekanavyo na mtu akishagundua ugonjwa huu unapaswa kupata matibabu ya dharura,” Prof. Kahamba alisema.

Alitaja dalili za kuwa na ugonjwa huo ni kulingana na tatizo lipo upande upi wa kichwa, lakini dalili za kawaida ni kuumwa kichwa, kizunguzungu, dalili za kutapika na kukosa nguvu kwenye mkono na mguu mmoja.

VIONGOZI WAMIMINIKA KUMUONA

Alisema idadi ya viongozi wa Serikali wakitanguliwa na Rais John Magufuli walienda kumjulia hali juzi na Mwakilishi wa Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Fancis, Askofu Mkuu, Marek Solczynski  ambaye alienda jana.

Wengine ni Askofu Mkuu mstaafu, Muadhama Polycarp Kardinali  Pengo, Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigilwa na maaskofu wengine.

Alisema watawashauri ndugu zake watengeneze kitabu cha watu wanaoenda kumuona ili waandike salamu zao za kumtamkia afya njema na kumuombea badala ya kuingia wodini.

Alisema kwa sababu yupo ICU anapaswa kupata muda mzuri wa kupumzika kwa ajili ya kuangalia afya yake na kwamba wanazuia kumuona kwa sababu ya kuhofia maambukizi ya magonjwa.

Prof. Kahamba aliwataka waumini wa kanisa hilo kuwa watulivu na kumuacha kiongozi huyo apumzike wakati akiendela kupatiwa matibabu.

Ni siku 27 tangu Askofu Ruwaichi ashike wadhifa huo, baada ya Muadhama Polycarp Kardinali Pengo kung’atuka Agosti 15, mwaka huu baada ya Papa Francisko kuridhia ombi lake.