Ziara ya JPM kituo cha Selander neema kwa askari

12Sep 2019
Gwamaka Alipipi
DAR ES SALAAM
Nipashe
Ziara ya JPM kituo cha Selander neema kwa askari

RAIS John Magufuli amefanya ziara ya kushtukiza katika Kituo cha Polisi cha Selander Bridge, jijini Dar es Salaam na kuagiza kupandishwa cheo askari wa kike kutoka koplo hadi kuwa sajenti.

Hatua hiyo ya Rais Magufuli ilifuatia ziara hiyo aliyoifanya juzi na askari huyo aliyekuwa akitoa huduma katika kituo hicho, WP 4160 Beatrice Mlanzi, kuonyesha utimilifu katika kazi yake.

Rais Magufuli amekuwa akifanya ziara za kushtukiza mara kwa mara tangu alipoingia madarakani, Novemba 5, 2015, siku moja baada ya kuapishwa alifanya ziara kama hiyo kwa kutembelea Hazina Kuu.

Novemba 9, 2015 Rais Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) ili kujionea hali ya utoaji huduma, mojawapo ya wagonjwa aliowatembelea na kumjulia hali alikuwa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Helen Kijo Bisimba, ambaye kwa sasa amestaafu.

Mei 28, 2017, akiambatana na mke wake Janeth alifanya ziara nyingine ya kushtukiza MNH na kuwajulia hali wagonjwa waliolazwa katika wodi ya Mwaisela.

Miongoni mwa wagonjwa aliowatembelea ni Mzee Francis Maige (Ngosha) kwa sasa ni marehemu, ambaye ndiye aliyechora nembo ya taifa.

Oktoba 5, 2016 alitembelea Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere (JNIA) sehemu ya kukagulia mizigo na abiria wa uwanja huo eneo la Terminal I na kubaini baadhi ya mashine za ukaguzi zilikuwa hazifanyi kazi.

Pia Mei 15, 2018 alitembelea Bandari ya Dar es Salaam katika matangi ya kuhifadhi mafuta ya kula baada ya kushushwa melini, alikagua uingizwaji na ugawaji wa ulipaji wa ushuru.

Vile vile, Juni 24, mwaka huu alifanya ziara ya kushtukiza katika mradi wa ujenzi wa daraja la baharini eneo la Selander linalokatiza baharini kwa kuunganisha maeneo ya Coco Beach, kujionea maendeleo ya ujenzi wa daraja hilo.

Habari Kubwa