Yanga: Tutaivaa Zesco kivingine

12Sep 2019
Faustine Feliciane
DAR ES SALAAM
Nipashe
Yanga: Tutaivaa Zesco kivingine
  • ***Zahera awatoa hofu mashabiki, asema tayari mkakati wa kuibuka na ushindi umekamilika na kwamba...

BAADA ya kushuhudia timu yake ikihitimisha kambi yake jijini Mwanza kwa kuvuna jumla ya mabao 4-1 kufuatia kuibuka na ushindi wa 3-0 dhidi ya Toto Africans ikiwa ni baada ya sare ya bao 1-1-

-dhidi ya Pamba, Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amewataka mashabiki wa timu hiyo kutuliza presha kwa kuwa wataivaa Zesco Jumamosi kivingine kabisa.

Akizungumza baada ya kuichapa Toto Africans juzi, Zahera alisema mbinu atakazotumia katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa dhidi ya Zesco ya Zambia ni tofauti kabisa na kwamba ana uhakika wa kikosi chake kuibuka na ushindi.

Alisema matokeo aliyoyapata jijini Mwanza hayamtii hofu na kwamba kila mechi kwake ina mbinu na ufundi tofauti katika kukabiliana nayo.

"Siangalii matokeo haya kwenye mechi hizi za kirafiki, kwani hata wachezaji watakaocheza mechi dhidi ya Zesco ni tofauti, kikubwa kwangu naangalia namna wachezaji wanavyocheza nakutazama nani nimtumie wapi na kwa muda gani, haya yote ni maandalizi kuelekea mchezo wetu wa Ligi ya Mabingwa," alisema Zahera.

Alisema namna walivyocheza kwenye michezo hiyo ya kirafiki sivyo watakavyocheza kwenye mchezo wa Jumamosi dhidi ya Zesco.

"Naifahamu Zesco, najua ubora wao na udhaifu wao..., nimeshaandaa namna ya kuwakabili, mashabiki wafahamu tunavyocheza sasa kwenye michezo ya kirafiki, sivyo tutakavyocheza na Zesco, tutaingia uwanjani kivingine," alisema.

Aidha, amewataka mashabiki wa timu hiyo kujitokeza kwa wingi uwanjani kuwapa hamasa wachezaji wao ili kuhakikisha wanaibuka na ushindi siku hiyo.

Katika ushindi huo wa juzi dhidi ya Toto Africans, mabao yalifungwa na David Molinga aliyetupia mawili dakika ya 37 na 41, huku la tatu lilifungwa na kiungo mpya, Mzanzibari Abdulaziz ‘Bui’ Makame dakika ya 51.

Na katika mechi dhidi ya Pamba bao la Yanga lilifungwa na Molinga ambaye hata hivyo hatacheza mechi dhidi ya Zesco kutokana na kuendelea kusubiri kibali chake cha kimataifa kutoka Shirikisho la Soka barani Afrika (Caf).

Ushindi kwenye mchezo huo wa kwanza utawaweka Yanga katika nafasi nzuri kuelekea mechi ya marudiano wiki mbili zijazo nchini Zambia.

Hata hivyo, endapo Yanga itashindwa kupata matokeo ya jumla katika mechi hizo mbili nyumbani na ugenini, itaangukia kucheza mechi ya mchujo na timu zitakazovuka raundi ya kwanza kutoka Kombe la Shirikisho Afrika ili kuwania nafasi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa utajiri kwa ngazi ya klabu barani Afrika.

Habari Kubwa